Bonyeza HAPA kudownload applicationi ya Bongojamii Blog kwenye simu yako ili kupata habari zetu Haraka
BONYEZA HAPA KU-DOWNLOAD
Figisufisu na ugomvi kati ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Christian Makonda na Askofu Mkuu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima (GCTC), Josephat Mathias Gwajima, zimepamba moto na joto lake linapanda na kushuka kila kukicha.
CHANZO CHA UGOMVI WA MAKONDA NA GWAJIMA
Nyuma ya ugomvi huo unaotajwa kuwa wa kihistoria huku mmoja akimwaga mboga na mwingine anamwaga ugali, duru za kisiasa zinadai kwamba, chanzo cha yote hayo ni Ubunge wa Jimbo la Misungwi mkoani Mwanza, Uwazi limedokezwa.
Jimbo la Misungwi kwa sasa linaongozwa na aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Charles Muhangwa Kitwanga.
KITWANGA NA UWAZI
Akizungumza na Uwazi katika mahojiano maalum na kutoa la moyoni juu ya sakata hilo mwishoni mwa wiki iliyopita, Kitwanga aliwavaa wawili hao akiwashangaa kusikia kwamba wanalitaka jimbo lake hilo.
Kitwanga alikiri kuwa, amezisikia habari hizo lakini kinachomshangaza ni kwamba, ni mapema mno kwani ni mwaka wa pili tu, tangu uchaguzi ulipomalizika mwaka 2015 na uchaguzi mwingine upo mbali kwani ni hadi mwaka 2020.
KITWANGA AFUNGUKA
“Taarifa hizo nimezisikia lakini kinachonishangaza ndiyo kwanza tumetoka kwenye uchaguzi na uchaguzi mwingine bado sana.
“Kwani tayari umeshafika muda wa kugombea?
Wameshapitishwa na vyama vyao?
Ninachojua ni kwamba, sisi tumemaliza uchaguzi na sasa tunafanya kazi, mimi natekeleza ilani ya chama changu (CCM).
WAACHE KUVURUGA WANANCHI
“Kama wanagombana na wao wanataka jimbo langu, wasubiri muda utakapofika tufanye kampeni na siyo kuvuruga wananchi wangu. Katika taratibu zetu ndani ya chama ziko tofauti sana.
“ Najua Gwajima ni mwanachama wa Chadema na Makonda anaiami n i CCM, wao wana taratibu zao lakini wasivuruge wananchi wangu ninaowatumikia, wao waendelee na hayo mambo yao.
WANAKARIBISHWA ULINGONI
“Hata hivyo, simzuii mtu kugombea katika jimbo langu, wanakaribishwa ulingoni lakini wafuate taratibu za vyama vyao muda utakapofika tutajua, huu ni muda wa kuchapa kazi kama ilivyo kauli mbiu ya Rais Magufuli ya Hapa Kazi Tu na ndicho ninachokifanya kwa wananchi wangu na si vingine na wala sitaki kuwaingilia kwenye huo ugomvi wao,” alisema Kitwanga.
YATOKANAYO
Katika uchunguzi wake, Uwazi lilidokezwa na vyanzo vyake kuwa, Makonda anatajwa kutaka ubunge wa jimbo hilo ili kupandisha kiwango chake cha kisiasa na hata kufikia ngazi ya uwaziri baada ya 2020.
Hata hivyo, suala la wawili hao kuhusishwa na jimbo hilo iliwahi kuelezwa na Askofu Gwajima siku chache baada ya kutajwa na Makonda kwenye kuhusika na mambo ya dawa za kulevya hivyo kudai kuwa ni vita ya kisiasa.
Gwajima anayetoka kijiji kimoja na Makonda cha Koromije jimboni Misungwi alikaririwa kanisani kwake akisema kuwa zipo taarifa za Makonda kumsakama kwa sababu anadhani na yeye (Gwajima) analitaka jimbo hilo.
“Nilipata msiba nyumbani Koromije nilikozaliwa, kwa kuwa nilitoka muda mrefu huko hivyo nilikwenda msibani kwa helikopta.
“Kule kuna shangazi yangu, nilitua kwa ndugu wengine na kama unavyojua helikopta ikitua kijijini, lazima watu waje wengi kuitazama.
GWAJIMA NA KITWANGA
“Nilipoondoka, watu wakabaki wakiita Gwajima… Gwajima. Baada ya wiki tatu, nne, kaka yangu ambaye ni mtoto wa shangazi alifariki dunia, nikaona safari hii nikiwa ninakwenda kule nimpigie Mbunge wa Misungwi (Kitwanga), nikamweleza kuwa nitakwenda kule tena kwenye jimbo lako, naomba ukiwa na nafasi twende wote… sitaki unione ninakwenda kwa madhumuni ya kisiasa.
“Nilipokwenda, Kitwanga alikuwa bize, akasema nenda na katibu wangu, nikamchukua na mbunge mwingine wa zamani wa jimbo hilo nikasema twende wote ili wasifikiri kwamba Gwajima anataka kufanya kitu.
“Nikatua na helikopta pale msibani, si unajua tena, wakaniambia ongea lakini sikuhutubia lolote. Nikakaa na mapailoti wetu na baada ya msiba nikaondoka.
GWAJIMA NA MAKONDA
“Sasa baadaye ndiyo watu wakasema yule kiumbe (Makonda) alikuwa anataka lile jimbo, ulipokwenda wewe alihisi unataka kulichukua mwaka 2020, nikasema angeniuliza, kwa mimi siwezi kuwa mbunge, nikiwa mbunge ni kujishusha, mimi ni mtumishi wa Bwana ambaye ni zaidi ya mbunge, waziri na rais, siwezi kugombea urais uwaziri au ubunge, nitakuwa nimejishusha, mimi ni mtumishi wa Mungu aliye hai.
“Kwa hiyo Makonda alidanganyika na kujikuta akinitaja kwenye madawa ya kulevya akijua atakuwa amenimaliza kwa wananchi bila kujua sina ndoto hiyo,” alidai Gwajima lakini Makonda yeye hajawahi kulizungumzia hilo.
Jumapili iliyopita Uwazi lilimtafuta Makonda ili kusikia upande wake lakini simu yake iliita bila kupokelewa.
KINACHOENDELEA
Jumapili iliyopita Gwajima aliendelea kutumia kanisa lake kumshambulia Makonda juu ya suala ya vyeti feki huku akiweka hadharani ‘document’ aliyodai ni cheti cha kidato cha nne cha Makoda cha Shule ya Sekondari ya Pamba iliyopo Mwanza.
Hata hivyo, Makonda wiki iliyopita akiwa na watu waliokuwa wakitumia madawa ya kulevya alizungumzia elimu yake kwa kujigamba kwamba akiwa rais wa wanafunzi wa vyuo vikuu alifanya makubwa na hakuzungumza chochote kuhusu vyeti feki anavyodai Askofu Gwajima.
Bonyeza HAPA kudownload applicationi ya Bongojamii Blog kwenye simu yako ili kupata habari zetu Haraka