Makonda Yupo Hatarini Kuuawa, Vigogo wa Madawa ya Kulevya Wapanga Mikakati ya Kummaliza kwa Gharama Yeyote Ile. | BONGOJAMII

Makonda Yupo Hatarini Kuuawa, Vigogo wa Madawa ya Kulevya Wapanga Mikakati ya Kummaliza kwa Gharama Yeyote Ile.

Bonyeza HAPA kudownload applicationi ya Bongojamii Blog kwenye simu yako ili kupata habari zetu Haraka
BONYEZA HAPA KU-DOWNLOAD


Wakati vita dhidi ya madawa ya kulevya jijini Dar vikipanuka na kugeuka kuwa suala la kitaifa, kuna kila dalili kuwa usalama wa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda upo hatarini, Risasi Mchanganyiko limebaini.


Juzi Jumatatu, Paul Makonda alijitokeza tena hadharani na kutoa ufafanuzi wa mambo kadhaa yanayohusiana na vita alivyovianzisha, huku ikiwa ni mara yake ya tatu kutaja majina ya wanaojihusisha na madawa ya kulevya, safari hii, akitoa orodha ya watu 97.


HATARI YAKE IKOJE?


Biashara ya ‘unga’ ni moja kati ya biashara chache zenye fedha nyingi duniani, ambayo bahati mbaya inapigwa vita na serikali nyingi. Watu wanaojihusisha na shughuli hii, wana fedha nyingi na wako tayari kufanya lolote linalowezekana kuifanya biashara yao kuwa salama.


Kwa Paul Makonda kutangaza vita hadharani, tena akitaja majina ya watu na njia zinazotumika kuuleta, kuusambaza na kuusafirisha, anajiweka katika nafasi mbaya ya kuwa mlengwa wa wafanyabiashara hao, hasa kwa kuwa kukamatwa kwao siyo tu kutaharibu biashara yao hiyo, bali pia wao wenyewe watapotea.


Mfano mmojawapo wa jinsi watu wanaojihusisha na biashara hiyo walivyo na uwezo mkubwa, ni kesi ya bilionea wa unga wa Colombia, Pablo Escobar, aliyeuawa Disemba 2, 1993, baada ya mahakimu zaidi ya 30 waliosimamia shauri hilo kuuawa, licha ya kuendesha kesi hiyo wakiwa mafichoni, tena sauti zao zikiwa zimewekwa mawimbi ya kutofahamika.


MAADUI ZAKE WAMEONGEZEKA


Awali, ilionekana ni wauza madawa ya kulevya pekee ndiyo ambao wanaweza kusemwa kuwa ni maadui zake, lakini baada ya mazungumzo yake na vyombo vya habari Jumatatu iliyopita, watu ambao watafurahia kuona kiongozi huyo kijana anapatwa na matatizo, wameongezeka.


Watu hao ni pamoja na wamiliki wa maduka ya kubadilishia fedha maarufu kama Bureau de Change, wafanyabiashara wa mitungi ya gesi, wamiliki wa mahoteli na klabu za kamari (Casino), achilia mbali watoto wa viongozi wakubwa tokea serikali ya awamu ya tatu, chini ya Benjamin Mkapa.


KWA NINI HAWA?


Licha ya kushangazwa na wingi wa maduka ya kubadilishia fedha (alisema yapo zaidi ya 200 kwa Dar pekee), lakini pia aliyatuhumu kufanya miamala inayozidi kiwango kinachotakiwa kisheria, hivyo kuufanya mzunguko wa fedha zinazopitia hapo kuwa mkubwa.


Alisema wingi huo wa fedha, unatia shaka kuwa huenda unatumiwa na watu wa biashara ya madawa ya kulevya katika kutakatisha fedha. Kwa vyovyote, wenye maduka hawa hawajapendezwa na tuhuma dhidi yao na hivyo nao kuingia vitani kimyakimya.


Biashara ya mitungi ya gesi nayo ilitajwa kuwa ni mojawapo ya njia zinazotumiwa na wafanyabiashara hao kuficha madawa hayo wakati wakisafirisha kutoka au kwenda ughaibuni.


Aidha, alidai kuna hoteli kadhaa kubwa zenye wakazi wa kudumu, ambao wanatambuliwa na wamiliki wake, hivyo atahakikisha anawafanyia kazi, kitu ambacho kinaongeza idadi ya maadui, kama ilivyo kwa wamiliki wa nyumba 200 waliosemwa kuwa wanaruhusu biashara hiyo kufanywa ilhali wakijua ni kosa kisheria.


MBINU ZINAZODAIWA KUANDALIWA


Baadhi ya wanaharakati wanaopinga biashara ya madawa ya kulevya, ambao waliomba hifadhi ya majina yao, wamesema mbinu mbalimbali zinaweza kutumika ili kumdhuru kiongozi huyo, aliyewahi kuwa mkuu wa wilaya ya Kinondoni.


Mbinu hizo ni pamoja na kumwinda na kumuua kwa risasi, kitu ambacho ili kukidhibiti, wameomba kuimarishwa kwa ulinzi wake, nyumbani, kazini na hata awapo barabarani.


VIDOSHO, AJALI ZA KUTENGENEZWA


Eneo lingine alilotahadharishwa kujihadhari nalo ni pamoja na wasichana warembo, kwani wanaweza kutumiwa na maadui ili kumtia matatizoni, ikiwemo kumwekea sumu katika chakula, kinywaji au hata kumdhuru kwa namna nyingine.


Wadau hao wamelitaja eneo lingine la hatari linalopaswa kuangaliwa zaidi, ni kwa maadui zake hao kuweza kumtengenezea ajali ya kumdhuru, ili mradi wafanikiwe kuzima harakati zake za madawa ya kulevya alizoanzisha na kuungwa mkono na watu wengi.


KUHUSU ULINZI, HUYU HAPA SIRRO


Kamanda wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Simon Sirro alizungumza na Risasi Mchanganyiko juu ya ulinzi wa kiongozi huyo. Akionyesha mshangao, alisema suala hilo siyo jambo la kuuliza kwa sababu wao wanaelewa nini kinapaswa kufanyika.


“Tunajua ukubwa wa vita hivi na madhara yake pia tunajua, huyu ndiye Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa, tunampatia ulinzi imara kabisa na kwa hili wala watu wasiwe na wasiwasi.”

source: udakuspecially

Bonyeza HAPA kudownload applicationi ya Bongojamii Blog kwenye simu yako ili kupata habari zetu Haraka

Featured Posts