Bonyeza HAPA kudownload applicationi ya Bongojamii Blog kwenye simu yako ili kupata habari zetu Haraka
BONYEZA HAPA KU-DOWNLOAD
MAWAKILI wa wafanyabiashara watatu, akiwamo Ali Haji, maarufu kama Shikuba, jana waliwasilisha kusudio la kukata rufani kupinga uamuzi wa kuwa kizuizini uliotolewa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, juzi.
Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu ilikubali maombi ya Waziri wa Katiba na Sheria ya kumsafirisha Shikuba na wenzake kwenda Marekani kujibu tuhuma za kujihusisha na biashara ya dawa za kulevya.
Kusudio hilo la kukata rufani Mahakama Kuu Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam liliwasilishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu na mawakili Hudson Ndusypo na Majura Magafu.
"Ni kweli tumewasilisha kusudio la kukata rufani kupinga wateja wetu kuwekwa kizuizini," alisema Ndusyepo wakati akizungumza na Nipashe kwa njia ya simu. "Tunasubiri mwenendo wa maombi ili tukate rufani."
Mbali na Shikuba walalamikiwa wengine ni, Idd Mfuru na Lwitiko Emmanuel maarufu kama Tiko.
Mahakama ya Kisutu iliyoketi chini ya Hakimu Mkazi Mkuu Mfawidhi, Cyprian Mkeha, ilitoa uamuzi kwamba imekubali kuwaweka kizuizini wafanyabiashara hao hadi waziri atakapotoa kibali cha kusafirishwa kwenda Marekani.
Katika uamuzi huo, wafanyabiashara hao watakuwa kizuizini hadi pale waziri atakapotoa kibali cha kuwasafirisha kwenda Marekani kujibu tuhuma za kusafirisha na kuingiza dawa za kulevya aina ya heroine kilo 100.
Hakimu alisema baada ya kusikiliza hoja za pande zote mbili mahakama yake imeona maombi ya waziri yamekidhi vigezo vya kisheria na kwamba imekubali kuwaweka kizuizini walalamikiwa hadi kibali cha kupelekwa ugaibuni kitakapotolewa.
“Mahakama hii inatoa amri hii chini ya kifungu cha 8 kidogo cha (3) cha Sheria ya Usafirishaji wahalifu nje ya nchi…” alisema Hakimu Mkeha.
Hata hivyo, Mahakama iliamuru ikitokea walalamikiwa hao wakakaa kizuizini kwa mwezi mmoja bila kusafirishwa, wana haki ya kuhoji ama kuomba kuachiwa huru mpaka pale mlalamikaji atakapochukua hatua nyingine dhidi yao.
KILO 210
Shikuba juzi alilishangaa Jeshi la Polisi kwa kumshitaki kwa kesi yenye uzito mdogo.
Akizungumza kabla ya kuanza kwa kikao cha mahakama kizimbani, Shikuba alisema amekaa mahabusu mkoani Lindi kwa tuhuma za kusafirisha kilo 210 za dawa za kulevya lakini anashangaa Polisi kumshtaki kwa kesi nyingine yenye uzito mdogo wa dawa.
Shikuba, alikamatwa kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere Machi, 2014 baada ya kuwindwa kwa miaka miwili kabla ya kuhamishiwa mkoani Lindi.
Anatuhumiwa kuwa kiongozi wa genge lenye makao yake Afrika Mashariki lakini likiwa na uhusiano wa kibiashara mpaka China, Brazil, Canada, Japan, Marekani na Uingereza.
“Ntafanyaje? Nasubiri kwenda Marekani bila viza, hapa tulipo tuko kama wahujumu uchumi," alisema Shikuba na kulalamika, "hatujabadilisha nguo siku ya tatu leo... labda kwa kuwa kwenye picha uchafu hauonekani."
Shikuba alisema hakuna lisilokuwa na mwisho na kwamba anamwomba Mungu huko Marekani haki ikatendeke dhidi yao kwa tuhuma zinazowakabili.
Upande wa Jamhuri katika maombi hayo uliongozwa na Wakili wa Serikali Mkuu, Edwin Kakolaki akisaidiana na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Veronika Matikila na Wakili wa Serikali Costantine Kakula.
Bonyeza HAPA kudownload applicationi ya Bongojamii Blog kwenye simu yako ili kupata habari zetu Haraka