Bonyeza HAPA kudownload applicationi ya Bongojamii Blog kwenye simu yako ili kupata habari zetu Haraka
BONYEZA HAPA KU-DOWNLOAD
WAKATI kikosi cha timu ya MC Alger ya Algeria kikitarajiwa kutua nchini leo usiku kwa ndege maalum ya kukodi, Kocha Mkuu wa Yanga, George Lwandamina amesema ili timu yake iwe kwenye nafasi salama ya kusonga mbele katika mashindano ya Kombe la Shirikisho Afrika, anahitaji kumaliza kazi nyumbani,
Kwa kupata ushindi wa kuanzia mabao 2-0.
Akizungumza na gazeti hili jana, Mzambia Lwandamina alisema matokeo ya sare yoyote au ushindi wa bao 1-0 utawaweka kwenye nafasi ya "hatari" ya kusonga mbele katika mashindano hayo ya Kombe la Shirikisho Afrika.
Lwandamina alisema ili kupata matokeo mazuri dhidi ya Waarabu unahitaji kuwa na wachezaji ambao wako tayari kucheza soka la ushindani dakika zote 90 na wanaofahamu vizuri mbinu za wapinzani hao.
"Unapokuwa na majeruhi unalazimika kubadilisha mfumo, halafu kucheza na Waarabu kunahitaji nguvu za ziada na matokeo mazuri ya kufurahisha, kinyume cha hapo nafasi ya kusonga mbele inakuwa ndogo, hatutaki hili litokee," alisema Lwandamina.
Kocha huyo aliongeza kuwa anataka kumaliza "kazi nyumbani" na ugenini iwe ni kumalizia dakika 90 zilizosalia ambazo watacheza bila presha.
Katibu Mkuu wa Yanga, Boniface Mkwasa, alisema jana maandalizi ya mechi hiyo ya Jumamosi yanaendelea vyema na msafara wa MC Alger utawasili saa tatu usiku ukiwa na watu 40.
"Watakuja na ndege ya kukodi ambayo itawasubiri kwa ajili ya kurejea kwao, pia wametueleza mchezo wetu wa marudiano hautafanyika Algiers, ni mji mwingine wenye umbali zaidi ya kilomita 10," alisema Mkwasa.
Aliwataja waamuzi ambao wamepangwa na Shirikisho ya Soka Afrika (Caf), kuchezesha mechi hiyo kuwa ni Louis Hakizimana atakayepuliza filimbi ya kati akisaidiwa na Theogene Ndagijimana na Jean Bosco Niyitegeka wote kutoka Rwanda.
Yanga na MC Alger zitarudiana kati ya Aprili 14 na 16, mwaka huu na mshindi wa jumla atafuzu kucheza hatua ya makundi ya michuano hiyo.
Mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Bara wamefika hatua hiyo ya mtoano baada ya kutolewa katika michuano ya Ligi ya Mabingwa na Zanaco ya Zambia kutokana na matokeo ya sare ya 1-1 nyumbani na sare tasa ugenini.
Bonyeza HAPA kudownload applicationi ya Bongojamii Blog kwenye simu yako ili kupata habari zetu Haraka