MJAMZITO ACHOMWA MKUKI , WAWILI WACHOMWA MOTO | BONGOJAMII

MJAMZITO ACHOMWA MKUKI , WAWILI WACHOMWA MOTO

Bonyeza HAPA kudownload applicationi ya Bongojamii Blog kwenye simu yako ili kupata habari zetu Haraka
BONYEZA HAPA KU-DOWNLOAD
Watu watatu wameuawa kwenye Bonde la Yaeda Chini katika matukio tofauti, ikiwamo wawili kuteketezwa kwa moto, huku mjamzito akichomwa mkuki.

Mkuu wa Wilaya ya Mbulu, Chelestino Mofuga alisema jana kuwa matukio hayo yalitokea juzi kwenye vijiji vya Dumanga na Mongo wa mono vilivyopo katika Bonde la Yaeda Chini.

Mofuga alisema katika tukio la kwanza watu watatu waliodaiwa kuwa majambazi walipora pikipiki na wakati wanakimbia mmoja aliyejulikana kwa jina la Makafo Elia alishindwa kukimbia akakamatwa na wananchi baada ya mafuta ya pikipiki kwisha na wananchi hao kumuua kwa kumchoma moto na kuteketea hadi kuwa majivu.

Alisema katika tukio la pili Martin Boay (25) alimchoma mkuki mjamzito Elizabeth Elias (35) na kufariki dunia, lakini naye aliuawa na wananchi wenye hasira walioamua kumfunga mikono na miguu na kumtupa kwenye moto ambako aliungua hadi kubakia majivu. “Hadi hivi sasa bado polisi wanaendelea na uchunguzi wa matukio hayo matatu ili kuhakikisha mambo ya kujichukulia sheria mkononi yanakomeshwa,” alisema Mofuga.

Aliongeza kuwa kamati ya ulinzi na usalama imekemea tabia ya watu kujichukulia sheria mikononi. Pia, mkuu huyo wa wilaya amemuagiza mkuu wa polisi wa wilaya kuchukua hatua za kisheria dhidi ya wahusika ili iwe fundisho kwa wengine.

“Bonde la Yaeda Chini lina historia ya matukio ya uhalifu hasa mauaji, ujangili wa nyara za Serikali na wizi wa mifugo. Tunaanzisha harambee kwa kuhamasisha wananchi na wadau wengine ili kujenga kituo cha polisi katika bonde hilo,” alisema.

Mofuga aliongeza kuwa, ujenzi wa kituo na nyumba za familia 12 utagharimu Sh435 milioni na unatakiwa kuanza mara moja.

Alisema ameanza harakati za kuwaomba wadau, wananchi na Serikali kuchangia ujenzi huo ili kutafuta amani ya kudumu katika eneo hilo.

Bonyeza HAPA kudownload applicationi ya Bongojamii Blog kwenye simu yako ili kupata habari zetu Haraka

Featured Posts