Mahakama Kuu Kuamua Dhamana ya Lema Ijumaa Hii... | BONGOJAMII

Mahakama Kuu Kuamua Dhamana ya Lema Ijumaa Hii...

Bonyeza HAPA kudownload applicationi ya Bongojamii Blog kwenye simu yako ili kupata habari zetu Haraka
BONYEZA HAPA KU-DOWNLOAD
Hatima ya dhamana ya Mbunge wa Arusha Mjini, Godbles Lema (Chadema), itajulikana Ijumaa wiki hii baada ya shauri hilo kurudishwa Mahakama Kuu Kanda ya Arusha kwa utekelezaji wa uamuzi wa Mahakama ya Rufaa.


Hatua hiyo imekuja baafa ya jopo la majaji watatu wa Mahakama ya Rufaa Tanzania kufuta rufaa mbili za Mkurugenzi wa Mashitaka(DPP), dhidi ya mbunge huyo juzi mjini hapa.


Mmoja wa mawakili anaomtetea mbunge huyo, Adam Jabir, alisema shauri hilo litaamuliwa Machi 3, mwaka huu mbele ya Jaji Salma Maghimbi kutokana na rufaa ya Jamhuri namba 135 ya mwaka jana, inayopinga uamuzi wa Novemba 11, mwaka jana wa Hakimu wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha, Desderi Kamugisha kumpa Lema haki ya dhamana.


Novemba 11 mwaka jana, Wakili Mwandamizi wa Serikali Paul Kadushi, alisimama wakati hakimu huyo akijiandaa kuandika masharti ya dhamana na kuieleza mahakama hiyo kuwa wameshasajili notisi ya kusudio la kukata rufaa Mahakama Kuu wakipinga uamuzi wa hakimu huyo kumpa Lema dhamana.


Hata hivyo,uamuzi huo wa dhamana haukuweza kutekelezwa kwa sababu ya nia ya kukata rufaa waliyoitoa mawakili hao wa Serikali.


Hakimu Kamugisha alishindwa kuendelea na mahsarti ya dhamana kwa mshitakiwa huyo ambapo,alikubaliana na upande wa Jamhuri na kusema kuwa notisi ina hadhi sawa na maombi ya rufaa yaliyowasilishwa Mahakama Kuu hivyo mwenendo na uamuzi wake utasimama mpaka uamuzi utakapotolewa na Mahakama Kuu.


Januari 4 mwaka huu, Jaji Maghimbi alitarajiwa kusikiliza na kutoa uamuzi kuhusiana na dhamana ya Lema ila ilikwama baada ya mawakili wa Serikali kukata Rufaa Mahakama ya Rufaa Tanzania,kupinga Jaji huyo kusikiliza rufaa yao wenyewe.


Jaji Magimbi alitarajiwa kutoa uamuzi juu ya rufaa iliyowasilishwa na upande wa Jamhuri wakipinga Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha kumpa Lema haki ya dhamana.


Uamuzi huo ulikuwa ukisubiriwa kwa hamu na wakazi wengi wa jiji la Arusha,hasa ikizingatiwa mbunge huyo anashikiliwa katika mahabusu ya Gereza Kuu la Kisongo kwa zaidi ya miezi mitatu,tangu akamatwe na polisi nje ya viwanja vya Bunge mjini Dodoma, Novemba 2, mwaka jana.


Aidha uamuzi huo ulikuwa unatarajiwa kutoa tafsiri ya kisheria ya notisi ya nia ya kukata rufaa iliyowasilishwa na na mawakili hao wa Jamhuri,notisi iliyosababisha Mahakama hiyo ya Hakimu Mkazi kutokuendelea na hatua ya kuweka masharti ya dhamana.


Akiahirisha uamuzi huo mahakamani hapo,Jaji huyo alisema kuwa mikono yake imefungwa na hawezi kusikiliza na kutoa uamuzi kutokana na mawakili wa Serikali,kusajili nia ya kusudio la kukata rufaa Desemba 30 mwaka jana,katika Masijala ya Mahakama ya Rufaa Tanzania iliyopo mkoani hapa, kupinga asisikilize rufaa hiyo.


Awali kabla ya mawakili wa serikali kukata rufaa Mahakama ya Rufaa Tanzania kupinga kusikilizwa kwa rufaa yao Mahakama Kuu, Jaji Maghimbi,aliwataka mawakili wa Jamhuri kuwasilisha hoja zao za rufaa Disemba 29,huku mawakili wa Lema wakitakiwa kujibu hoja hizo Disemba 30 kabla ya mahakama hiyo kutoa uamuzi wa rufaa hiyo jana.


Lema anakabiliwa na kesi mbili za uchochezi dhidi ya Rais Dk. John Magufuli, katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha kesi namba 440 na 441.

Bonyeza HAPA kudownload applicationi ya Bongojamii Blog kwenye simu yako ili kupata habari zetu Haraka

Featured Posts