TRA Yamkalia kooni Mbowe Yamwita Mahakamani Kisa Hakutumia Mashine ya EFD Club ya Bilcanas. | BONGOJAMII

TRA Yamkalia kooni Mbowe Yamwita Mahakamani Kisa Hakutumia Mashine ya EFD Club ya Bilcanas.

Bonyeza HAPA kudownload applicationi ya Bongojamii Blog kwenye simu yako ili kupata habari zetu Haraka
BONYEZA HAPA KU-DOWNLOAD

Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) iliyodai kuwa imeshindwa kuwapata kwa kutumia hati za wito za Mahakama, Freeman Mbowe, mkewe Dk Lilian Mtei na aliyekuwa Meneja wa Klabu ya Bilicanas, Steven Mligo kujibu mashtaka yanayowakabili, jana ilisaidiwa namna ya kuwafikia watu hao.

Mahakama ya Wilaya ya Ilala, ilitoa barua ya wito wa kuwataka wahudhurie mahakamani Machi 21, baada ya kufikia uamuzi wa kutoa wito huo kupitia magazeti.

Mbowe ambaye ni Mbunge wa Hai na Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni na mkewe, Dk Mtei ni wakurugenzi wa Kampuni ya Mbowe Hotels Ltd.

Wawili hao pamoja na Mligo, Katika kesi hiyo namba 402 ya mwaka 2016, wanakabiliwa na mashtaka matatu ya kushindwa kutumia mashine za kielektroniki (EFD) kutoa risiti kinyume na kifungu cha 86 cha Sheria ya Usimamizi wa Kodi ya mwaka 2015.

Mashtaka mengine ni kuipotosha mamlaka kwa kutoa nyaraka za uongo kinyume na kifungu cha 84 na kushindwa kutekeleza masharti ya Sheria ya Usimamizi wa Kodi kinyume na kifungu cha 82 cha sheria hiyo. Wanadaiwa kutenda makosa hayo Mei, 2016 jijini Dar es Salaam.

Imedaiwa kuwa tangu kesi hiyo ilipofunguliwa mwishoni mwa mwaka jana, imeshatajwa mara nne bila washtakiwa kufika mahakamani.

Wakili wa TRA, Marcel Busegano aliieleza Mahakama kuwa wamejaribu kuwapelekea washtakiwa hati za wito wa kufika mahakamani mara nne lakini wameshindwa kuwapata.

Alidai Meneja wa TRA Mkoa wa Ilala alijaribu kumpigia simu ya mkononi Mbowe lakini hakumpata na, hata walipokwenda katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) anakofanya kazi mkewe, Dk Mtei pia hawakumpata.

Kutokana na hali hiyo, TRA iliiomba Mahakama iamuru watumie tangazo gazetini kuwaita washtakiwa mahakamani na iwapo korti itakubali ombi hilo, tangazo litolewe kabla ya tarehe nyingine ya kutajwa kwa kesi hiyo.

Shauri hilo linalosikilizwa na Hakimu Mkazi Mfawidhi, Ritha Tarimo litatajwa Machi 21.

Kutokanana na ombi hilo, tangazo hilo linapaswa kutangazwa gazetini kabla ya tarehe hiyo.

Bonyeza HAPA kudownload applicationi ya Bongojamii Blog kwenye simu yako ili kupata habari zetu Haraka

Featured Posts