TUNDU LISSU AONGEA MANENO MAZITO BAADA YA KUKAMATWA NA POLISI | BONGOJAMII

TUNDU LISSU AONGEA MANENO MAZITO BAADA YA KUKAMATWA NA POLISI

Bonyeza HAPA kudownload applicationi ya Bongojamii Blog kwenye simu yako ili kupata habari zetu Haraka
BONYEZA HAPA KU-DOWNLOAD
ANAANDIKA TUNDU LISSU
Kwa wananchi wote wa Tanzania. Nimekamatwa tena na serikali ya Bwana Mtakatifu Rais John Pombe Magufuli. Nimekamatiwa mahakamani Kisutu mara tu baada ya waendesha mashtaka wa serikali hii kunifutia kesi iliyotokana na kukamatwa kwangu bungeni Dodoma mwezi uliopita. Hiyo kesi wameifuta kwa maelezo kwamba serikali haina nia tena ya kuendelea na kesi hiyo. Sikutoka hata nje ya mahakama nikakamatwa tena. Wamenileta Central kwa mahojiano. Mapolisi walionikamata wamekataa kuniambia wananikamata kwa kosa gani. Kwa hiyo sijui kosa nilofanya hadi sasa. Nadhani sababu ina uhusiano wa moja kwa moja Uchaguzi wa Rais wa TLS unaofanyika wiki ijayo. Serikali hii, kwa kutumia mawakili wao vibaraka, imekuwa na mkakati mkubwa wa kunizuia kugombea urais wa TLS. Walikuwa wanapanga kwenda kupinga kugombea kwangu mahakamani. Tumewasema hadharani na kuzianika njama zao. Sasa wameamua kutumia rungu lao la siku zote: Jeshi la Polisi. Hofu yao ni kubwa sana. Natabiri watataka kuniweka ndani hadi baada ya Uchaguzi huo wa wiki ijayo. Natabiri mawakili vibaraka wao wataleta hoja kwenye TLS kwamba mgombea asiyekuwapo ukumbini wakati wa Uchaguzi aondolewe kwenye kinyang'anyiro hicho. Nawataka mawakili wanaotaka mwanzo mpya katika TLS wasikubali njama hizi. Hakuna makatazo yoyote katika kanuni za uchaguzi yanayozuia mgombea aliyeteuliwa kuondolewa kwenye uchaguzi kwa sababu tu hayupo ukumbini. Nawaomba washikilie msimamo kwamba wote walioteuliwa kugombea wapigiwe kura na wanachama wa TLS. Iwe mwisho kwa serikali hii kutuchagulia viongozi wetu. Iwe mwanzo wa TLS kutimiza wajibu wake kwa wanachama wake na kwa waTanzania. Nimekamatwa asubuhi na mapema. Hakuna sababu ya kutokunipeleka mahakamani leo hii hii. Kama hawatanipeleka mahakamani nawataarifu kwamba nitaanza mgomo wa kula chakula na sitakula chakula hadi hapo nitakapopelekwa mahakamani. Nawaombeni wapenda haki kokote mliko, ndani na au nje ya nchi, mchukue hatua zozote zile mtakazoona zinafaa ili kukabiliana na vitendo hivi vya kidikteta. Tutashinda. Utawala huu wa kiimla na wa kidikteta utashindwa. Aluta continua.

Bonyeza HAPA kudownload applicationi ya Bongojamii Blog kwenye simu yako ili kupata habari zetu Haraka

Featured Posts