Watu Wanamjaribu Rais Magufuli Kupitia Makonda.... | BONGOJAMII

Watu Wanamjaribu Rais Magufuli Kupitia Makonda....

Bonyeza HAPA kudownload applicationi ya Bongojamii Blog kwenye simu yako ili kupata habari zetu Haraka
BONYEZA HAPA KU-DOWNLOAD
Rais John Magufuli alipata kueleza kuwa yeye hajaribiwi, hata mimi naamini kuwa Rais wangu hajaribiwi. Rais wangu Magufuli yupo tofauti sana, mwenyewe alishasema hivyo.

Ninachompendea Magufuli wetu ni kuwa hajui kuremba. Hana kawaida ya kulazimisha nyekundu ionekane kijani. Hapana Rais Magufuli yupo tofauti sana. Kwake nyekundu ni nyekundu na kijani ni kijani.

Lipo jambo linalotawala sasa hivi, ni kuhusu uhalali wa cheti cha kidato cha nne ambacho Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda alikitumia kusomea elimu ya juu.

Hapa ndipo watu wanataka kumjaribu Rais wangu Magufuli. Kwamba afunike kombe mwanaharamu apite ili watu waseme Makonda ni invulnerable prince, yaani mwanamfalme asiyeguswa.

Rais Magufuli siyo kwamba hajui haya, anajua sana, amekaa kimya kama mtu mzima. Bila shaka yupo kwenye kipindi cha kujiridhisha, lipi linalosemwa ni la ukweli na lipi ni la uongo?

Watu wasimjaribu Rais Magufuli, naye hajaribiwi! Rais Magufuli alimtosa swahiba wake kabisa, Charles Kitwanga, kwa kosa moja tu la kuingia bungeni kalewa. Bila hata kuzungumza naye alimtumbua juu kwa juu.

Kitwanga akastaajabu. Akapata mpaka akili ya kwenda kufanya sala ya kuvuka mitihani Israel. Kitwanga kwa kushibana kwake na Magufuli, inadaiwa alianza kujiona Sir Alan Fredrick, aliyekuwa msaidizi wa Mfalme George VI kisha Malkia Elizabeth II.

Sir Alan Fredrick aliogopwa kwa sababu alikuwa karibu mno na mfalme kisha malkia. Na aliaminika kuwa ndani ya kichwa chake kulikuwa na siri nyingi za Uingereza. Unamgusa vipi Sir Alan Fredrick?

Aaah wapi! Rais Magufuli akasema yeye kwenye Serikali yake hana Sir Alan Fredrick, akamtumbua Kitwanga kisha nafasi yake akaijaza. Huyo ndiye Rais wangu Magufuli ninayemfahamu. Yeye anasimama kwenye hasi au chanya, hana katikati.

Rais Magufuli hana hizo za kuchekeana, kwa hiyo Makonda siyo untouchable prince. Rais Magufuli alimpumzisha msaidizi wake wa karibu aliyekuwa anafanya naye kazi Ikulu, Ombeni Sefue, itakuwa Makonda?

TUZUNGUMZE LILILO SAHIHI

Tumeshakubaliana kuwa Rais Magufuli hana tabia ya upendeleo na hana katikati. Hivyo tunakubaliana kuwa Rais Magufuli hawezi kumlinda Makonda kisha ajivunjie sifa yake njema aliyojiwekea.

Baada ya hapo tuzungumze; je, kinachosemwa ni sahihi? Hapo ndipo tunaweza kuuchimba mzizi wa fitina. Basi sasa, kinachozunguzwa kichunguzwe na haki itendeke.

Jina lake halisi ni Paul Christian Makonda au Daud Albert Bashite? Je, ni kweli alisomea elimu ya juu cheti cha kidato cha nne cha Paul Christian Muyenga? Maswali hayo ndiyo yatakayokata na kuuchimbua kabisa mzizi wa fitina.

Makonda asionewe, kwamba watu wenye visasi vyao wasiamue kumpakazia ili kumchafua. Kama kweli yeye ni Paul Christian Makonda na hilo la Daud Albert Bashite anazushiwa, inabidi Makonda awashitaki wanaomchafua.

Ikiwa anasingiziwa, hata Rais Magufuli itabidi awe mkali, maana watu watakuwa wanataka kumyumbisha yeye na utawala wake kisha kupoteza muda kwa vitu vya uzushi.

Ni kweli kuwa Makonda anachukiwa na watu wengi. Sababu ni aina ya ufanyaji kazi wake na uthubutu mkubwa alionao. Ndiyo maana nasema, kama hili la kutumia cheti cha Muyenga anasingiziwa, ni vizuri wanaomsingizia wakashughulikiwa kisheria.

Hata kama Makonda aliwahi kufanya makosa huko nyuma au siku za karibuni kutokana na utekelezaji wake mbaya wa majukumu yake, si sawa kuandamwa kwa tuhuma za uongo. Siku zote uongo haujengi, bali hubomoa.

Jamii nzuri tunayoitaka kwa nchi yetu, ni haki kutendeka na uonevu usipewe nafasi, kuanzia kwa raia wa kawaida chini kabisa mpaka kwa viongozi wao. Mtu akikosea ashughulikiwe kwa haki, siyo kwa kuzushiwa.

HAKI LAZIMA IDHIHIRIKE

Je, ni kweli Makonda anatumia cheti cha Muyenga? Kama ni kweli, siyo sawa kujificha kwenye mwavuli wa kuchukiwa na kudai anachafuliwa na wabaya wake. Haki itendeke na idhihirike.

Suala la Makonda kuwa jina lake ni Daud Albert Bashite na alitumia cheti cha Paul Christian M, kwamba ile M ni Muyenga kisha yeye akaigeuza kuwa Makonda, limeshakuwa mjadala mkubwa. Haupaswi kuachwa hivi! Jipu litumbuliwe.

Hizi tuhuma zimekuwa kubwa na zinazungumzwa mpaka na watu wenye hadhi na ushawishi mkubwa. Zinazungumzwa na watu wenye wafuasi wengi mbele ya wafuasi wao. Hivyo, hili si jambo la chumbani.

Kwa hali ilipofikia, tiba ya jambo hilo ni moja tu; Makonda kutokeza hadharani na kueleza ukweli wa mapito yake ya kielimu. Athibitishe kuwa yeye ni Paul Christian Makonda kwa kuzaliwa na kusoma.

Hata kama ni kweli awali aliitwa Daud Albert Bashite, atokeze na kueleza uhalali wake wa kubadili jina na kuanza kuitwa Paul Christian Makonda. Hivyo ndivyo kukata mzizi wa fitina.

NITATOA MFANO

Mwaka 2005, Mbunge wa Kigoma Mjini (ACT-Wazalendo), Zitto Kabwe, akiwa kijana mdogo, alipewa changamoto kuhusu elimu, wakati akigombea jimbo la Kigoma Kaskazini, kwa tiketi ya Chadema.

Aliyempa changamoto hiyo ni aliyekuwa mgombea kwa tiketi ya NCCR-Mageuzi, Lazaro Matete. Katika mikutano yake, Matete alisema Zitto hajasoma na kwamba alikuwa anawadanganya wapigakura wa Kigoma Kaskazini.

Zitto alikata mzizi wa fitina kwa kuweka wazi vyeti vyake. Matete alikosa hoja nyingine na baada ya Zitto kuanika ukweli wake, haujawahi kuwepo mjadala mwingine wowote kuhusu elimu ya Zitto.

Hivi ndivyo Makonda anatakiwa kuwakata vilimilimi wote wanaomsema kuwa yeye siyo Paul Christian bali jina lake halisi ni Daud Albert Bashite. Makonda akifanya alivyofanya Zitto mbona mambo yatakuwa kimya? Wanaomsema leo hawatakuwa na hoja nyingine.

Upo mfano wa pili; mwaka jana Rais Magufuli alipoteua wakurugenzi wa halmashauri mbalimbali nchini, aliyeteuliwa kuwa mkurugenzi wa Halmashauri ya Itigi, Luhende Pius, alisemwa kuwa aliishia kidato cha nne na kwamba alikuwa meneja wa Hoteli ya City Style, Sinza, Dar es Salaam.

Hivyo ndivyo ilivumishwa. Ikawa gumzo hasa kwenye mitandao ya kijamii. Hata hivyo, Rais Magufuli alikata mzizi wa fitina na kuuchimbua kabisa kwa kuonesha hadharani vyeti vya Luhende.

Rais Magufuli alisema: “Huyo mnayemsema ni wa kwenu, ninayemfahamu na niliyemteua ana master (shahada ya uzamili).” Baada ya hapo Luhende aliweka wazi cheti chake, kamera za vyombo vya habari zikarekodi. Ubishi ukaishia hapo.

Ndivyo ambavyo Makonda anapaswa kufanya. Unajua njia ya uongo ni fupi. Ikiwa yote yanasemwa ni kumsingizia, basi atokeze aweke wazi vyeti vyake. Aseme alisomea wapi darasa la kwanza mpaka alipofikia na kwa majina yapi. Akate mzizi wa fitina.

Rais Magufuli hana kupindapinda, ndiyo maana suala la Luhende japo halikuwa kubwa, lakini aliamua kulitolea ufafanuzi. Hili la Makonda limekuwa kubwa mno. Ufafanuzi wake unahitajika.

TUELEWE MANTIKI

Mjadala wa Makonda na vyeti vyake lisichukuliwe kishabiki. Wale wanaomshambulia na hata wanaomtetea. Hili jambo linahusu maadili ya utumishi wa umma, vilevile makosa ya kisheria.

Hivyo basi, washambuliaji wasipayuke tu, bali wawe wanatoa vielelezo vyenye kuthibitisha hoja zao. Na wanaomtetea, nao wasirushe maneno mithili ya wanaopiga ngumi hewani, bali nao watoe vielelezo.

Unamtetea Makonda? Unakuja ni jibu, Makonda unamfahamu vipi? Ulikutana naye wapi? Unajua shule alizosoma? Alikuwa anatumia majina gani? Kwa nini unaamini Paul Makonda uliyemjua ndiye huyu Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam? Unazungumza kwa kunyoosha maneno.

Unataka Makonda awajibike? Unasema Makonda unamfahamu vipi? Ulianza kumjua lini? Shule alizosomea ni zipi? Alikuwa anatumia majina yapi? Na kwa nini unasema Paul Makonda alitumia cheti cha mtu mwingine? Kwa nini unaamini Daud Bashite wako ndiye Paul Makonda? Majibu yawe na ujazo.

Narudia tena hili suala halitaki ushabiki. Ni suala nyeti kabisa. Makonda ni kiongozi, anayo dhamana kubwa ambayo ameibeba, kwa hiyo kumsingizia jambo la kughushi cheti ni kumvunjia heshima na kumdhalilisha kwa watu anaowaongoza na taifa kwa jumla.

Hili pia lieleweke; kama ni kweli Makonda alighushi cheti cha kidato cha nne ili apate uhalali wa kujiunga na masomo ya elimu ya juu, hapaswi kutetewa wala kuhurumiwa, maana ni mdanganyifu. Mtu mdanganyifu hapaswi kuhurumiwa.

Inapotokea mtu huyo mdanganyifu anakuwa kiongozi, hatari yake ni kubwa mno. Hivyo suala hili litafutiwe tiba. Makonda ndiye tibabu wa suala hili. Tiba ni kutoka hadharani na kujibu kila kinachozungumzwa.

Na hapa tatizo siyo kufeli. Wengi walifeli na wakajituma kusafisha vyeti vyao. Mjadala wa Makonda ni udanganyifu. Kufeli siyo kuvunja sheria za nchi. Udanganyifu wa cheti ni kosa kisheria.

Je, Makonda ni Jitender Singh Tomar wa Tanzania? Tomar alipata kuwa Waziri wa Sheria wa Delhi, nchini India. Aliwahi kusema yeye ni msomi wa shahada ya sayansi, kutoka Chuo Kikuu cha Avadh. Baadaye Avadh wakatoa taarifa hujasoma kwao.

Alipokataliwa Avadh, Tomar akasema alisoma Chuo Kikuu cha Chaudhary Charan Singh. Huko nako alikataliwa. Waziri Mkuu wa Delhi, Arvind Kejriwal, baadaye aliingilia kati kumlinda Tomar na kumbakiza kazini.

Hata hivyo, baada ya uchaguzi mwaka juzi, Tomar aliondolewa kwenye Baraza la Mawaziri lakini bado ni mbunge.

Makonda naye aseme, halafu shule ambazo atazitaja zitathibitisha. Zisipothibitisha au zikimkana tutajua ni yaleyale ya Tomar. Na akichwa kazini, basi Rais Magufuli atakuwa Kejriwal.

MAKONDA AMASAIDIE MAGUFULI

Kila mmoja anaona sasa, kwamba Rais Magufuli ndiye ambaye anatazamwa katika hili suala la Makonda. Watu wanaulizana, je, atamchukulia hatua au atamlinda kijana wake mpendwa?

Mimi msisitizo wangu upo palepale, Rais Magufuli hana tabia ya kulindana. Kama aliweza kumwondoa kazini aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Anne Kilango Malecela ndani ya siku 27 kwa ripoti ya watumishi hewa, atamwachaje Makonda kama atathibitisha ni kweli alighushi cheti?

Rais Magufuli ndiye mwanzilishi wa uhakiki wa vyeti bandia. Kuna watumishi wengi wa umma wamepoteza kazi kwa sababu ya kuhakikiwa vyeti vyao. Rais Magufuli anachukia tabia ya kughushi, kwa hiyo hili la Makonda hawezi kuliacha hivihivi.

Hivyo, shaka ondoa, Rais Magufuli atamalizana vizuri tu na Makonda kama atambaini kweli alighushi cheti. Rais Magufuli hachezewi.

Hata hivyo, Makonda anatakiwa amsaidie Rais Magufuli. Msaada wenyewe ni kwa kufanya mambo moja kati ya mawili. Bila shaka hapo ataweza kumfanya Rais wetu apumue.

Mosi; kutokeza mbele na kuwajibu wote wanaomsakama kuhusu mapito yake ya kielimu. Akiweza kuondoa utata, atamsaidia Rais Magufuli na haya maneno kuwa anamlinda.

Njia hiyo ndiyo ambayo Luhende aliitumia kumsaidia Rais Magufuli kwa kutokeza na cheti chake Ikulu. Na Rais Magufuli akakitumia cheti cha Luhende kufunga mjadala.

Pili; kama yote yanayosemwa ni sahihi kuwa alighushi cheti, basi anapaswa kuwajibika kwa kujiuzulu. Makonda akijiuzulu atamsaidia Rais Magufuli ili asichukue uamuzi wa kumfukuza kazi.

Kujiuzulu kwa Makonda kisha kuchukuliwa hatua za kisheria kwa kufanya udanganyifu, itakuwa hatua muhimu ya kuijengea heshima ya Rais Magufuli na Serikali yake kuwa inaukabili uovu wa aina zote bila woga wala haya.

Vinginevyo, kukaa kimya watu wataona Makonda analindwa. Na itaonekana nchi haina haki, maana kuna watu walilitumikia taifa hili kwa miaka, lakini wamepoteza kazi na stahiki zao kwa sababu ya ukakiki wa vyeti. Kwa nini wao yawakumbe na Makonda aachwe? Haki itendeke na ionekane imetendeka.

Ndimi Luqman MALOTO

Bonyeza HAPA kudownload applicationi ya Bongojamii Blog kwenye simu yako ili kupata habari zetu Haraka

Featured Posts