BILLION 200 ZATENGWA KWA AJILI YA KUHAMIA DODOMA RASMI | BONGOJAMII

BILLION 200 ZATENGWA KWA AJILI YA KUHAMIA DODOMA RASMI

Bonyeza HAPA kudownload applicationi ya Bongojamii Blog kwenye simu yako ili kupata habari zetu Haraka
BONYEZA HAPA KU-DOWNLOAD
RAIS Dk.John Magufuli amesema serikali imetenga Sh. Bilioni 200 kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu Dodoma, ikiwamo ujenzi wa ofisi na nyumba za viongozi wa serikali.


Akizungumza jana wakati wa maadhimisho ya miaka 53 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar katika Uwanja wa Jamhuri mjini hapa, alisema hatua za kuhamia Dodoma zimeshaanza na kwamba viongozi wakuu wa serikali na zaidi ya watumishi 3,000 wameshahamia.


“Katika awamu ya pili na ya tatu ya kuhamia Dodoma imepangwa kutekelezwa mwaka ujao wa fedha. Serikali imetenga fedha takriban Sh.bilioni 200 kwa ajili ya kujenga ofisi na nyumba za viongozi,” alisema


Alisema kwa mara ya kwanza maadhimisho hayo yamefanyika Dodoma kwa kuwa serikali ya awamu ya tano imedhamiria kuhakikisha makao makuu ya serikali yanahamia Dodoma na kwamba serikali sasa imefika Dodoma na hatutarudi tena.


“Tunaendelea kujenga miundombinu ya usafiri wa kuja na kutoka Dodoma, tumepanua uwanja wa ndege na tutaendelea kupanua zaidi na tumeshaweka jiwe la msingi la ujenzi wa reli ya kisasa itakayopita Dodoma na tunaendelea na ujenzi wa barabara.


“Tuna mipango kabambe ya kuboresha upatikanaji wa umeme na maji na huduma za afya na elimu. Maandalizi ya uwanja mkubwa wa michezo yanaendelea chini ya ufadhili wa serikali ya Morocco,”alisema.


Kuhusu Muungano, Rais Magufuli alionya kuwa kuwa mtu yeyote atakayetaka au kujitahidi kuvunja Muungano asithubutu badala yake atavunjika mwenyewe.


Sambamba na hilo, Rais Magufuli ameataka Watanzania kujivunia mafanikio ya Muungano kwa kuwa yamepatikana kutokana na uwepo wa amani ni lazima idumishwe na kutunzwa.


Pia amewataka kutafakari mahali walikotoka, walipo na wanakokwenda na kuwaomba kuulinda na kuudumisha ili jina la Tanzania liendelee kudumu katika maisha yote ya Watanzania.


Akizungumza wakati wa maadhimisho ya miaka 53 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini hapa, alisema kwa kutambua kuwa Muungano ndiyo silaha, jembe na ushindi, atahakikisha anaulinda kwa gharama yeyote.


Kuhusu mafanikio ya Muungano, Rais Magufuli alisema nchi imefanikiwa kupata mafanikio makubwa ikiwamo kuunganisha mataifa mawili na kuunda taifa moja lenye nguvu, hivyo kuwezesha kulinda uhuru, amani na umoja.


Alisema mafanikio mengine ni katika nyanja za kiuchumi, kisiasa na kijamii katika serikali zote mbili ambazo zimefanya kazi kubwa ya kukuza uchumi na kukabiliana na matatizo ya umaskini na ukosefu wa ajira.


Rais Magufuli alitaja pia kujengwa kwa miundombinu ya usafiri wa anga, majini, nchi kavu, umeme na kuboresha upatikanaji wa huduma za kijamii. Alisema shule na hospitali zimeongezeka, maji na demokrasia imepanuka.


“Naweza kusema Tanzania ya sasa si ile ya mwaka 1964. Nchi yetu pia imeheshimika kimataifa na imetoa mchango mkubwa katika Ukanda, bara na duniani kote na tumeshiriki katika harakati za ukombozi wa bara letu na tumeendelea kushiriki katika shughuli za kutafuta amani sehemu mbalimbali,”alisema.


Hata hivyo, alisema kuulinda Muungano si jambo rahisi, hivyo kuna usemi usemao ‘Ukiona vyelea ujue vimeundwa’ na kwamba mafanikio ya Muungano yaliyopo sasa,viongozi wameyapigania kwa kufanya kazi mchana na usiku.


“Zipo nchi nyingi zimejaribu lakini zimeshindwa. Kitu kinachoitwa Muungano ni kigumu kwa sababu hata kulinda ndoa zetu tu imekuwa ni vigumu,” alisema.

Bonyeza HAPA kudownload applicationi ya Bongojamii Blog kwenye simu yako ili kupata habari zetu Haraka

Featured Posts