CCM WAPO TAYARI KUKAA MEZA MOJA NA CUF | BONGOJAMII

CCM WAPO TAYARI KUKAA MEZA MOJA NA CUF

Bonyeza HAPA kudownload applicationi ya Bongojamii Blog kwenye simu yako ili kupata habari zetu Haraka
BONYEZA HAPA KU-DOWNLOAD
Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Dk Abdalla Juma Abdalla
CHAMA Cha Mapinduzi Zanzibar (CCM) kimesema kipo tayari kukaa katika meza moja na Chama cha Wananchi (CUF) kwa ajili ya utekelezaji wa Ilani ya chama hicho na sera zake kwa mwaka 2015-2020, lakini sio kujadili suala la uchaguzi uliopita wa mwaka 2015 ambao ulifutwa na Tume ya Uchaguzi (ZEC) kwa mujibu wa sheria.

Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Dk Abdalla Juma Abdalla maarufu Mabodi, alisema hayo wakati akizungumza na ujumbe kutoka Marekani ukiongozwa na Ofisa wa kusimamia masuala ya sera za kijamii na kisiasa Ukanda wa Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara, Gregory Simpkims, katika Ofisi Kuu Kisiwandui mjini Unguja.

Dk Abdalla alisema Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25, 2015 ulifutwa na ZEC baada ya kujitokeza kwa kasoro mbalimbali na ndipo ulipoitishwa uchaguzi wa marudio Machi 20, 2016.

Naibu Mkuu wa CCM Zanzibar alisema maamuzi yaliyochukuliwa na Tume ya uchaguzi kufuta Uchaguzi Mkuu yalikuwa halali kwa sababu ndiyo chombo kilichopewa mamlaka hayo kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar.

“Msimamo wa Chama Cha Mapinduzi upo wazi ni kwamba ipo tayari kushirikiana na Chama cha Wananchi kwa ajili ya kutekeleza Ilani ya CCM pamoja na sera zake kwa maslahi ya wananchi, lakini sio kukaa pamoja kujadili Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25 ambao ulifutwa,” alieleza Dk Abdalla.

Alisema ujumbe huo kwamba Serikali ya Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein inaendelea na majukumu yake ya kusimamia utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya kuleta maendeleo na kukuza uchumi wa wananchi na ustawi wake kwa ujumla.

Alisema mambo makubwa yamefanyika katika kipindi cha mwaka mmoja tu kipindi cha pili cha uongozi wa Dk Shein ikiwemo kuanzisha pensheni kwa wananchi waliofikisha umri wa miaka 70 huku uchumi na ukusanyaji wa mapato ukiimarika kwa kiwango cha kuridhisha.

Naye Ofisa kutoka Marekani, Simpkims alisema wameridhishwa na kasi ya maendeleo iliyofikiwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na kusema nchi hiyo ipo karibu zaidi kusaidia miradi ya maendeleo.

Alisema mafanikio hayo yamefikiwa kutokana na ukomavu wa CCM katika kuongoza na uzoefu wake kwa kuwa na viongozi wenye busara na hekima kubwa.

“Marekani imeridhishwa na juhudi zinazochukuliwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kutekeleza ahadi zake kwa wananchi zinazotokana na kipindi cha Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25 wa kampeni kwa wapiga kura na ndiyo maana sisi tupo tayari kushirikiana na Zanzibar,” alisema.

Ujumbe huo miongoni mwa masuala uliotaka kupata ufafanuzi wa kina ni kuhusu uwezekano wa kuwepo kwa mazungumzo ya kuleta muafaka wa kisiasa kati ya CCM na CUF ambao ulitokana na Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25 ambao ulifutwa.

Bonyeza HAPA kudownload applicationi ya Bongojamii Blog kwenye simu yako ili kupata habari zetu Haraka

Featured Posts