HII NDIO MBINU MPYA YA WASAMBAZAJI DAWA ZA KULEVYA | BONGOJAMII

HII NDIO MBINU MPYA YA WASAMBAZAJI DAWA ZA KULEVYA

Bonyeza HAPA kudownload applicationi ya Bongojamii Blog kwenye simu yako ili kupata habari zetu Haraka
BONYEZA HAPA KU-DOWNLOAD
HUENDA wauzaji na wasambazaji wa dawa za kulevya sasa wamebuni mbinu mpya ya kuingiza dawa hizo nchini, kutokana na udhibiti mkali uliowekwa na Serikali.

Badala ya kuingiza kete ambazo zimetengenezwa tayari kwa ajili ya matumizi, wanaingiza kemikali ambazo zina uwezo wa kutengeneza dawa hizo hapa hapa nchini.

Hayo yalielezwa jana na Kamishna Msaidizi Ukaguzi wa Sayansi ya Jinai, Betha Mamuya, alipozungumza na waandishi wa habari katika Bandari kavu ya AMI, iliyopo Tabata Relini.

Katika bandari hiyo jana, maofisa wa Mamlaka ya Kuzuia na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA), Wakala wa Mkemia Mkuu wa Serikali (GCLA) na Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) walifanya ukaguzi na kubaini makontena mawili yenye zaidi ya lita 5,000 za kemikali bashirifu zinazodaiwa kuingizwa nchini kinyume cha sheria.

Mamuya alisema kemikali hizo zina uwezo wa kutengeneza dawa aina ya heroin na cocaine.

Alisema mzigo huo ni mali ya Kampuni ya Tecno Net Scientific, inayomilikiwa na Benedict Assey na kwamba umeingizwa nchini ukitokea Ufaransa na India.

“Hili ni tatizo la dunia, serikali imedhibiti uingizwaji wa dawa hizi nchini, lakini kwa ‘trend’ hii tunayoiona, tunadhani wamebadili mbinu na kuanza kuzitengeneza nchini na pengine zinasafirishwa kwenda nje,” alisema.

Aliongeza: “Ndiyo maana tunafanya ukaguzi huu, tumeanzia Dar es Salaam, lakini tutakwenda nchi nzima, tutafanya uchunguzi wa kina kujua mzigo huu uliwasili lini nchini.

“Na kwa kuwa mmiliki wa mzigo huu hivi karibuni tulimkuta akiwa na mzigo mwingine, huku taarifa za Wakala wa Mkemia Mkuu wa Serikali zikionesha kibali chake kimekwisha muda, tutachunguza kujua huu wa leo (jana) aliingiza lini, baada ya ukaguzi wa kwanza au kabla.

“Na tutachunguza pia katika maeneo yote ambayo alikuwa akisambaza kemikali hizi, mahitaji halisi yalikuwa kiasi gani na kama zilikuwa nyingi, wapi ambapo walikuwa wakipeleka kiasi kinachobaki,” alisema.

Aliwataka wafanyabiashara ambao wanazileta kihalali kwa mujibu wa sheria wasizichepushe matumizi yake, kwani sheria itachukua mkondo wake.

“Lazima tudhibiti, maana vijana wanaharibiwa kutokana na matumizi ya dawa hizi,” alisisitiza.

Kamishina wa Operesheni wa Mamlaka hiyo, Msekela Mihayo, alisema ukaguzi huo umefanyika baada ya kupata taarifa juu ya uwapo wa mzigo huo katika bandari hiyo.

“Hivyo tunawasihi wananchi waendelee kushirikiana na sisi ili kwa pamoja tuweze kukabiliana na uingizwaji huu tunusuru jamii yetu,” alisema.

Hivi karibuni, Mkemia Mkuu wa Serikali, Profesa Samwel Manyele, alisema ofisi yake kwa kushirikiana na DCEA na TFDA wamewasilisha taarifa ya pamoja ya ukaguzi kwa vyombo vya dola ili kufanya uchunguzi wa shughuli zinazofanywa na kampuni hiyo.

“Taratibu za uchunguzi zitakapokamilika tunakusudia kuifikisha kampuni hii mahakamani kujibu tuhuma za kuendesha shughuli za kemikali huku ikitambua kuwa kibali chake kimekwisha tangu Aprili 30, mwaka jana,” alisema.

Alisema zipo taarifa kuwa, kampuni hiyo imekuwa ikighushi vibali na njia nyingine za udanganyifu kuingiza kemikali nchini.

“Kwa mujibu wa sheria, baada ya muda wa usajili kwisha kampuni husika hutakiwa kusitisha shughuli zake hadi hapo itakapopata kibali.

“Baada ya muda wa kibali kwisha kampuni hii iliwasilisha maombi ya kuhuisha usajili wake, lakini ilitakiwa kusubiri kibali, lakini iliendelea na shughuli zake, jambo ambalo ni kinyume cha sheria,” alisema.

Profesa Manyele aliwataka wafanyabiashara wa kemikali kuzingatia sheria za uingizaji, usafirishaji, uhifadhi na utumiaji wa kemikali, ikiwamo bashirifu.

Hivi karibuni, Assey alikamatwa kwa kuingiza kemikali bashirifu zenye ujazo wa lita 6,494 kwa kukiuka sheria na taratibu.

Bonyeza HAPA kudownload applicationi ya Bongojamii Blog kwenye simu yako ili kupata habari zetu Haraka

Featured Posts