Bonyeza HAPA kudownload applicationi ya Bongojamii Blog kwenye simu yako ili kupata habari zetu Haraka
BONYEZA HAPA KU-DOWNLOAD
KAIMU Mwenyekiti wa klabu ya Simba, Salim Abdallah ‘Try Again’, amesema jumla ya Sh. bilioni 1.3 zimetumika kwa ajili ya usajili wa kikosi cha Simba msimu huu.
Abdallah alitoa kauli hiyo katika mkutano wa kawaida wa kila mwaka wa klabu hiyo uliofanyika jana kwenye Ukumbi wa Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Mwalimu Nyerere (MNICC) jijini Dar es Salaam.
Akitoa ufafanuzi wa namna fedha hizo zilizotumika, Kaimu Mwenyekiti huyo, alisema wamesajili kikosi madhubuti kwa gharama kubwa, lengo likiwa ni kurejesha heshima ya klabu yao na kwamba wachezaji wa kigeni pekee wamegharimu Sh. milioni 679, zikiwamo Sh. milioni 226 zilizotumika katika dirisha dogo Desemba mwaka jana.
“Usajili wetu Simba mwaka huu umegharimu Sh. bilioni 1.35 kati ya hizo Sh. milioni 679.5 zimetumika kwa usajili wa wachezaji wa kigeni pekee, zikiwamo Sh. milioni 226.5 zilizotumika katika dirisha dogo,”alisema Abdallah.
Kaimu Mwenyekiti huyo alisema mwaka huu klabu imetenga bajeti ya Sh. billioni 4.7 na hadi sasa wana uhakika wa kupata Sh. bilioni 3.3 tu kupitia vyanzo vyao mbalimbali vya mapato, huku Uwanja wa Bunju akieleza kuwa utawagharimu Sh. milioni 200.
Katika hatua nyingine, Simba imemsimamisha uanachama mchezaji na kiongozi wake wa zamani, Mzee Hamisi Kilomoni ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza la Wadhamini.
Salim Abdallah alipendekeza mbele ya wanachama 927 Kilomoni aondolewe katika Baraza la Wadhamini kwa kitendo chake cha kufungua kesi Mahakama ya Kisutu wiki hii kupinga mkutano wa jana.
“Mzee Kilomoni amevunja Katiba ya Simba Ibara ya 18 kifungu cha 15 (b) ambayo haitaki kupeleka mambo ya soka mahakamani, ikiwa wana chombo cha kusimamia matatizo,”alisema Abdallah.
Aidha, Kilomini ametakiwa kuandika barua ya utetezi na kufuta kesi aliyofungua Kisutu, tofauti na hivyo atafutwa kabisa uanachama.
Katika hatua nyingine, Mkutano huyo umepitisha Waziri wa zamani wa Michezo, Profesa Juma Athumani Kapuya ameteuliwa kuziba pengo la Ally Sykes katika Baraza la Wadhamini, huku Mkuu wa Wilaya ya Kilosa, Alhaj Adam Mgoyi akiteuliwa kuziba nafasi ya Kilomoni.
Bonyeza HAPA kudownload applicationi ya Bongojamii Blog kwenye simu yako ili kupata habari zetu Haraka