Bonyeza HAPA kudownload applicationi ya Bongojamii Blog kwenye simu yako ili kupata habari zetu Haraka
BONYEZA HAPA KU-DOWNLOAD
NAIBU KAMISHNA (DCP) LUCAS MKONDYA.
KAIMU Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Naibu Kamishna (DCP) Lucas Mkondya, amepelekwa kuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mtwara katika mabadiliko yaliyofanywa na Mkuu wa Jeshi hilo, Inspekta Jenerali (IGP) Simon Sirro.
Mkondya alipata umaarufu usio wa kujivunia jijini Dar es Salaam mapema mwezi huu baada ya amri yake ya kupiga marufuku magari yenye vioo vya giza (tintend) kwenye Kanda Maalum, kutenguliwa na Mkuu wa Mkoa saa chache kabla ya kuanza utekelezaji.
Badala ya Mkondya, Dar es Salaam sasa itakuwa chini ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Kamishna Msaidizi Mwandamizi (SACP) Lazaro Mambosasa.
Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari jana, jijini Dar es Salaam na msemaji wa Jeshi la Polisi, Barnabas Mwakalukwa, ilisema pia aliyekuwa Kamanda wa Mkoa wa Mtwara, SACP Neema Mwanga, anarudishwa Makao Makuu, Dar es Salaam na atapangiwa kazi nyingine.
Sambamba na mabadiliko hayo, taarifa imeeleza, IGP Sirro amemteua DCP Juma Yusuf Ally kuwa Kaimu Kamishna wa Polisi Zanzibar.
Taarifa hiyo ilieleza kuwa uteuzi wa DCP Ally unatokana na kustaafu kwa mujibu wa sheria kwa aliyekuwa Kamishna wa Polisi Zanzibar, Hamdani Omari Makame, baada ya kutimiza umri wa miaka 60.
“Kabla ya uteuzi huo, DCP Ally alikuwa Mkuu wa Utawala na Fedha Makao Makuu ya Polisi Zanzibar,” taarifa hiyo ilieleza.
Aidha, IGP Sirro amemteua Kamanda wa Polisi Mkoa wa Temeke, SACP Gilles Mroto, kuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma na Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Emmanuel Lukula kuwa Kamanda wa Polisi mkoa wa Temeke.
Kabla ya uteuzi huo, ACP Lukula alikuwa Ofisa Mnadhimu wa Polisi Mkoa wa Mbeya.
USUMBUFU WANANCHI
Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam alifuta agizo la DCP Mkondya Agosti 6, kwa kuagiza Polisi jijini kusitisha utekelezaji wa amri iliyowataka wananchi wenye magari kuondoa 'tint' kwenye vioo vya magari yao.
Agizo hilo ambalo utekelezaji wake ulikuwa uanze siku inayofuata, lilielezwa na Mkuu wa Mkoa kuwa ni lenye uwezekano mkubwa wa kuzua usumbufu kwa wananchi kwani "sababu za utekelezaji wake hazina mashiko".
"Tafsiri yake ya kwanza ambayo agizo hilo inapeleka kwenye jamii ni kuwa wenye tinted kwenye vioo vya magari yao, kama sio wao basi wanaoyatumia, ni wahalifu," alisema mkuu huyo, "jambo ambalo si kweli."
Mkuu huyo alifafanua kuwa yapo magari yanakuja nchini kutoka viwandani yakiwa na vioo tinted na kwamba baadhi ya wamiliki wa magari hutumia vioo vya giza hivyo kama njia ya kujilinda dhidi ya wahalifu, na hasa kina mama.
"Aidha, mkoa wa Dar es Salaam siyo kisiwa, kuna watu wanaingia kila siku; Je, magari yao tunataka wayapaki Chalinze?"
DCP Mkondya alishauriwa kutafuta njia sahihi ya kupambana na wahalifu badala ya kutumia mbinu ambazo zinaweza kusababisha usumbufu kwa wananchi.
Aidha, DCP Mkondya aliiambia Nipashe kwa njia ya simu Jumapili iliyopita kuwa taarifa alizonazo juu ya kuwapo kwa miili 15 iliyoopolewa kwenye Bahari ya Hindi jijini Dar es Salaam na wavuvi katika siku za karibuni, ni mitatu na haikuwa kwenye viroba.
“Hadi sasa taarifa za miili mingi kama hiyo kuokotwa nazisikia kwako," alisema Kamanda Mkondya. "Hao watu watueleze nasi tutachukua hatua, hatuna taarifa za miili iliyofungwa kwenye viroba au sandarusi.
"Miili mitatu iliyookotwa Kunduchi iko Hospitali ya Taifa (MNH) na haijatambuliwa, wananchi wafike kuitambua.”
Lakini akizungumza na kituo cha Redio One juzi, IGP Sirro alikiri kuzagaa kwa maiti hizo zinazookotwa na wavuvi na kusema kwamba zinafanyiwa uchunguzi wa vinasaba ili kujua kama ni Watanzania.
"Jeshi la Polisi tayari lishachukua hatua za awali za utambuzi kwa kuchuliwa vina saba maiti hizo ili kufahamu ni raia wa wapi na tukishakamilisha zoezi hilo tutatangaza watu waliopotelewa na ndugu zao kuja kufanya utambuzi," alisema IGP Sirro.
Alisema ingawa watu wanadhani kwamba mauaji hayo yamefanywa na Polisi, jeshi lake huwa halina kificho pindi linapokabiliana na wahalifu kwenye mapambano.
Alisema inapotokea polisi ikaua majambazi katika mapigano ya kurushiana risasi, huweka wazi tukio hilo na siyo kwenda kuwatumbukiza baharini.
Mwanaharakati Sheikh Issa Ponda Jumatatu aliitaka serikali kutoa kauli kuhusu maiti hizo ambazo zilifichuliwa na Nipashe kwa mara ya kwanza siku hiyo.
Bonyeza HAPA kudownload applicationi ya Bongojamii Blog kwenye simu yako ili kupata habari zetu Haraka