Bonyeza HAPA kudownload applicationi ya Bongojamii Blog kwenye simu yako ili kupata habari zetu Haraka
BONYEZA HAPA KU-DOWNLOAD
SASA unaweza kusema ahadi ya Serikali ya Awamu ya Tano ya kuboresha huduma za afya siyo siasa maneno matupu tena bali vitendo.
Kinachothibitisha hilo, ni kusainiwa kwa makubaliano na Kampuni ya Zipline ya Marekani, kwa ajili ya kuleta ndege 120 zisizotumia rubani ambazo zitatumika kusambaza vifaa tiba na dawa katika maeneo yasiyofikika kwa urahisi nchini.
Makubaliano hayo yalisainiwa jana kati ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Bohari Kuu ya Dawa (MSD) na Kampuni ya Zipline na ndege hizo zitaanza kusambaza dawa, vifaa tiba na nyaraka muhimu kuanzia mwakani katika Mkoa wa Dodoma.
Akizungumza wakati wa kusaini makubaliano hayo, Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dk. Mpoki Ulisubisya, alisema kampuni ya Zipline italeta ndege 120 kwa ajili ya nchi nzima.
Alisema pia ndege hizo zitahudumiwa na wizara hiyo na zitaanza pia katika mikoa ya Nyanda za Juu Kusini na Mkoa wa Pwani na baadaye maeneo yote nchini.
“Tunaishukuru Kampuni ya Zipline kwa kutuletea huduma hii nchini, baada ya kusaidia Uganda. Ndege hizo zitasaidia kutoa huduma za dawa maeneo ambako hakufikiki kirahisi,” alisema.
Alifafanua zaidi mbali na kusambaza dawa, ndege hizo zitasaidia kutoa ajira kwa Watanzania ambao watafanya kazi katika kampumi hiyo.
“Wametuahidi kuwa kampuni itakayoanzishwa nchini itaajiri Watanzania wengi ambao pia, watapata mafunzo mbalimbali juu ua shughuli zitakazofanywa. Nawasihi vijana ambao wataajiriwa wawe na mawazo mazuri yatayosaidia kupanua huduma zinazotolewa na kukuza uchumi wa Taifa letu,” alisema.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa MSD, Laurean Bwanakunu, alisema mpango huo unaenda sambamba na lengo la serikali la kupunguza gharama za dawa na kuzisambaza kwa wingi maeneo mbalimbali nchini.
Alisema ndege tano hadi 10 ndizo zitakazoanza kutoa huduma nchini na baadaye zitasambazwa nchi nzima na kufikia 120.
Alisema ndege hizo zina uwezo wa kubeba damu na chanjo za mbwa pamoja na huduma nyingine muhimu zitabebwa na ndege hizo.
Bwanakunu alisema wanashirikiana na Taasisi ya Ifakara ambayo inafanya utafiti, ili kujua maeneo ambako watazielekeza ndege hizo kupeleka huduma katika siku za baadaye.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Zipline, Keller Rinaudo, alisema huduma hiyo ya ndege ni rahisi kwa ajili ya kutolea huduma za afya maeneo yasiyofikika hususani vijijini.
Alisema baada ya kutoka Uganda, wameamua kuleta huduma hiyo nchini na lengo lao ni kuhakikisha wanaziwezesha nchi za Afrika Mashariki, ili nchi zilizoendelea zijifunze teknolojia hiyo Afrika.
Bonyeza HAPA kudownload applicationi ya Bongojamii Blog kwenye simu yako ili kupata habari zetu Haraka