Bonyeza HAPA kudownload applicationi ya Bongojamii Blog kwenye simu yako ili kupata habari zetu Haraka
BONYEZA HAPA KU-DOWNLOAD
HATIMAYE wanafunzi watatu wa Shule ya Msingi ya Lucky Vincent mkoani Arusha waliojeruhiwa katika ajali ya basi lililoua wenzao 32, Mei 6, mwaka huu, wanatarajia kuwasili nchini Ijumaa kutoka Marekani walikokuwa wakipata matibabu.
Wanafunzi hao ni Dorin Mshana, Sadia Awadhi na Wilson Tarimo ambao walipelekwa nchini humo Mei 14, mwaka huu kupatiwa matibabu katika Hospitali ya Mercy Medical iliyoko Sioux City.
Ajali ya wanafunzi hao ilitokea Mei 06, mwaka huu, eneo la Malera wilayani Karatu na kusababisha vifo vya wanafunzi 32, walimu wawili na dereva wakati wakienda kufanya mtihani wa kijipima kitaaluma na wanafunzi wenzao wa Shule ya Tumaini Junior ya Karatu.
Wanafunzi hao walikuwa kwenye gari mali ya shule hiyo lenye namba za usajili T871 BYS aina ya Mitsubishi Rosa, ambalo lilishindwa kufunga breki likiwa kwenye mteremko, kuserereka na kutumbukia katika mto Marera ulioko katika mlima Rhotia.
Majeruhi hao watatu walipelekwa Marekani kwa matibabu zaidi ya mifupa wakitokea nchini kwa ndege maalum ya Samaritan Purse.
Kwa mujibu wa taarifa iliyoandikwa na Mbunge wa Singida Kaskazini, Lazaro Nyalandu, kwenye ukurasa wake wa Facebook, watoto hao wanatarajiwa kuwasili nchini Agosti Ijumaa saa 3 asubuhi katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA).
Nyalandu ambaye ni mmoja wa waasisi wa Taasisi ya Stem iliyoratibu safari ya majeruhi hao kwenda Marekani, aliwaomba Watanzania kujitokeza kwa wingi kuwapokea watoto hao.
“Ijumaa, Agosti 18 saa 3 asubuhi tunatarajia watu wajitokeze KIA kuwapokea hawa watoto, Mungu ibariki Tanzania, ratiba ya hafla hiyo itatolewa Jumatatu (leo),” alisema Nyalandu.
Doreen alifanyiwa upasuaji na madaktari bingwa wanne huku upasuaji wa kwanza akifanyiwa kwenye paja na bega kwa takribani saa nne kwa mafanikio makubwa.
Pia, Doreen alifanyiwa upasuaji mwingine wa taya na daktari bingwa, Jeff Dean, kwa saa tano pamoja na upasuaji wa uti wa mgongo uliofanywa na madaktari watatu.
Kwa upande wake, Sadia alifanyiwa upasuaji wa mfupa wa mbele wa kulia wa paja, kiganja cha kulia cha mkono na shingo yake kuwekewa kishikizio maalum alichokaa nacho kwa wiki sita.
Naye Wilson alifanyiwa upasuaji kwenye maeneo mbalimbali ya mwili wake ambao aliwekewa chuma chembamba maalumu mguu wa kulia pamoja na kupasuliwa kiwiko cha mkono wa kulia na wa kushoto.
Bonyeza HAPA kudownload applicationi ya Bongojamii Blog kwenye simu yako ili kupata habari zetu Haraka