MAZITO HAYA, MATAJIRI WAJENGA MAHANDAKI KUJIANDAA NA MWISHO WA DUNIA | BONGOJAMII

MAZITO HAYA, MATAJIRI WAJENGA MAHANDAKI KUJIANDAA NA MWISHO WA DUNIA

Bonyeza HAPA kudownload applicationi ya Bongojamii Blog kwenye simu yako ili kupata habari zetu Haraka
BONYEZA HAPA KU-DOWNLOAD
UKITAMKA “handaki la kujificha kwa ajili ya mwisho wa dunia” watu wengi watadhani kuwa ni chumba kilichojengwa kwa uimara wa hali ya juu kikiwa kimesheheni vyakula vilivyosindikwa na vitu vingine ili kuwezesha watu kuishi kwa muda mrefu.


Tishio la kuangamia kwa dunia kwa sasa ni kubwa kama ilivyokuwa wakati wa Vita Baridi, lakini mahandaki haya ya leo ni tofauti kabisa na zile za karne ya 20.


Kampuni nyingi duniani kote zimekuwa zikishughulikia kuongezeka kwa mahitaji ya majengo yenye uwezo wa kuwalinda watu dhidi ya hatari ya aina yoyote, iwe ni magonjwa hatari ya kuambukiza, dunia kugongana na sayari au kitu chochote kutoka anga za juu, Vita ya Tatu ya Dunia – lakini wakati huo huo jengo hilo liwe ni sehemu yenye starehe.


“Mahandaki wakati wa baba au babu yako hayakuwa yanakalika,” anasema Robert Vicino, mfanyabiashara wa majengo na Afisa Mtendaji Mkuu wa Vivos, kampuni ambayo hujenga na kusimamia majumba ya kifahari duniani kote.


“Hayakuwa yanavutia. Yalikuwa yanajengwa kwa chuma, kama ilivyo meli au kifaa cha kijeshi. Na ukweli ni kwamba, binadamu hawezi kuishi kwa muda mrefu katika mazingira ya namna hiyo.


Mahitaji ya mwisho wa dunia


Matajiri wengi duniani, wakiwemo mameneja wa mifuko ya fedha, nyota wakubwa wa michezo mbalimbali na matajiri katika nyanja ya teknolojia (kuna uvumi kuwa Bill Gates amejenga handaki kwenye kila sehemu ambapo ana mali isiyohamishika kama ardhi) wamechagua kubuni makazi yao ya siri kwa ajili ya familia na wafanyakazi wao.


Gary Lynch, meneja mkuu wa kampuni ya Rising S Company ya huko Texas nchini Marekani, anasema kuwa mauzo kwa ajili ya majengo ya chini ya ardhi yameongezeka kwa asilimia 700 mwaka 2016, ukilinganisha yalivyokuwa mwaka 2015, wakati kwa ujumla mauzo hayo yameongezeka kwa asilimia 300 tangu uchaguzi mkuu wa Marekani Novemba mwaka jana.


Majengo ya chuma ya kampuni hiyo, ambayo yamebuniwa kwa ajili ya kudumu kwa vizazi kadhaa, yanaweza kuchukua chakula cha kutosha matumizi ya mwaka mzima kwa kila mkazi wa majengo hayo na pia yana uwezo wa kuhimili matetemeko makubwa ya ardhi.


Lakini wakati wengine wanataka kukaa kwenye majengo hayo peke yao, wengine wanataka kukaa huko na jamii zao ili kuwa na mfano wa maisha yanayofanana na yalivyo sasa.


Wabunifu wa majengo maalumu kwa ajili ya jamii mara nyingi hununua mahandaki ambayo hapo awali yalikuwa yakitumiwa kijeshi au mahandaki maalumu ambayo yalijengwa na serikali ya Marekani kwa ajili ya kuficha silaha kali – maeneo ambayo yanaweza kugharimu mamilioni ya dola kwa ajili ya kuyajenga leo hii.


Majengo hayo ambayo yameimarishwa, yamebuniwa kuweza kuhimili shambulio la kinyuklia na yamewekewa mifumo maalumu ya umeme, mifumo ya kusafisha maji, mifumo kwa ajili ya kuhimili matetemeko makubwa ya ardhi, na pia kuhimili mashambulizi ya silaha za kibiolojia na kikemikali. Lakini pia, majengo hayo yana mifumo kwa ajili ya kusafisha hewa.


Majengo hayo yanaweza kuchukua kiasi cha chakula cha kuweza kukaa kwa mwaka mzima au zaidi, na mengi ya majengo hayo yana bustani maalumu ambazo zinaweza kutumiwa kupanda mimea kwa kutumia madini fulani ambayo huwekwa kwenye maji, hivyo kuondoa umuhimu wa kutumia udongo, na hivyo kuweza kuwapatia wakazi wa majengo hayo virutubisho maalumu ambavyo vinapatikana kwenye mimea.


Wajenzi wa majengo hao pia wanafanya kazi ili kuhakikisha kuwa jumuiya ambazo zitakuwa zinaishi kwenye majengo wanakuwa na vipaji mbalimbali ili kuhakikisha kwamba watu wataweza kuishi katika majengo hayo kwa muda mrefu, kuanzia madaktari hadi walimu.


Vicino anasema Vivos imepokea maombi mengi kwa ajili ya majengo yake wakati wa uchaguzi nchini Marekani mwaka jana.


Safina ya mbunifu


Moja ya makazi hayo, Vivos xPoint, yapo karibu na Black Hills huko South Dakota nchini Marekani, na lina jumla ya mahandaki 75 ya kijeshi ambalo zamani lilikuwa ni sehemu maalumu kwa ajili ya kuhifadhi silaha za jeshi hadi mwaka 1967.


Sehemu hiyo sasa inabadilishwa ili kuwa ni sehemu yenye uwezo wa kuchukua jumla ya watu 5,000. Marekebisho ndani ya mahandaki hayo yanafanywa kwa gharama ya kazi ya dola 25,000 hadi 200,000 kwa kila moja. Bei ya handaki hutegemea ukubwa wake.


Jengo lenyewe litawekwa starehe zote ambazo hupatikana kwenye mji mdogo, zikiwemo ukumbi wa burudani, madarasa, bustani maalumu, kliniki na sehemu ya kufanya mazoezi ya mwili.


Kwa wateja ambao wanatafuta vitu adimu na vya starehe zaidi, kampuni hiyo inauza Vivos Europa One, ambayo imepewa jina la “safina ya kisasa ya Nuhu” katika ghala za zamani za kuhifadhi silaha wakati wa vita baridi nchini Ujerumani.


Jengo hilo, ambalo limejengwa kwenye jabali, lina makazi 34 binafsi, kila moja likiwa na ukubwa wa futi za mraba 2,500, na likiwa na uwezekano wa kuongeza ghorofa hivyo kufikia ukubwa wa futi za mraba 5,000.


Nyumba zilizoimarishwa kuhimili nyuklia


Majumba kwa ajili ya matajiri yaliyojengwa na Larry Hall zinazofahamika kama Survival Condo huko Texas nchini Marekani zinatumia maeneo mawili yaliyokuwa yanatumiwa kuhifadhi makombora ya masafa marefu, ambayo yalijengwa na mainjinia wa Jeshi la Marekani ili kuhifadhi vichwa vya mabomu ya nyuklia wakati wa miaka ya 1960.


“Wateja wetu wanapewa faida ya kuwa na nyumba ya kifahari na ambayo inakuwa imeimarishwa kuhimili shambulizi la kinyuklia,” anasema Hall, ambaye tayari amesjaanza kazi ya ujenzi wa nyumba nyingine ya aina hiyo sehemu nyingine.

Bonyeza HAPA kudownload applicationi ya Bongojamii Blog kwenye simu yako ili kupata habari zetu Haraka

Featured Posts