MAWAZIRI WAKERWA NA KAULI YA MBOWE | BONGOJAMII

MAWAZIRI WAKERWA NA KAULI YA MBOWE

Bonyeza HAPA kudownload applicationi ya Bongojamii Blog kwenye simu yako ili kupata habari zetu Haraka
BONYEZA HAPA KU-DOWNLOAD
Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe 
WAKATI hotuba ya bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu inaendelea kujadiliwa leo, tayari bajeti hiyo imetoa majibu kuhusu dhana kwamba mhimili wa Serikali umekuwa unaingilia uhuru wa mihimili mingine ya Bunge na Mahakama.

Hotuba ya ofisi hiyo iliyosomwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa wakati akiwasilisha hotuba yake kwa mwaka wa fedha wa 2017/18, imetoa taswira ya wazi ya serikali kutoa ushirikiano wa kutosha wa kuifanya mihimili hiyo kufanya kazi kwa uhuru na ufanisi.

Mathalani akiwasilisha maoni ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kuhusu hotuba hiyo ya bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu, Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe (Chadema) alilazimika kukatizwa mara kwa mara kutokana na kutoa kauli kwamba mhimili wa Mahakama haupo huru.

Huku akitumia mifano kadhaa, Mbowe alisema hivi sasa mhimili wa Mahakama haupo huru na kwamba Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais John Magufuli inauendesha mhimili huo itakavyo, hatua aliyosema itawafanya wananchi kupoteza imani kwa chombo hicho na hivyo kuwepo kwa uwezekano wa kutoweka kwa amani na utulivu.

Miongoni mwa viongozi waliosimama ili kupinga hoja hiyo ya Mbowe kuwa serikali hususani Rais Magufuli anaingilia mhimili wa Mahakama ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na wenye Ulemavu, Jenista Mhagama aliyesema anayeweza kusema mhilimili wa Mahakama haupo huru ni Mahakama yenyewe.

Naye Waziri wa Katiba na Sheria, Profesa Paramagamba Kabudi ambaye pia alipinga madai hayo na kusema hakuna ushahidi wowote unaoonesha kuwa Rais au Serikali imeingilia uhuru wa Mahakama.

Kauli hiyo ya Mbowe ilipingwa pia na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, George Simbachawene aliyesema Mbowe anatumia jina la Rais vibaya kwa kusema kuwa anaingilia mhimili wa Mahakama, jambo ambalo si la kweli.

Hata hivyo katika hotuba yake; Waziri Mkuu Majaliwa ameeleza namna ambavyo serikali imetoa ushirikiano mkubwa kwa lengo la kuvijengea uwezo vyombo vya Bunge na Mahakama kwa lengo la kuviboresha kwa rasilimali watu na miundombinu, hatua ambayo bila shaka itaimarisha uwajibikaji.

Kulingana na hotuba hiyo maeneo yanayotoa taswira ya wazi ya Mahakama kujiimarisha na kuzidi kuwa na uwezo mkubwa zaidi ni pamoja na eneo la kusikiliza kesi ambapo chombo hicho kimedhihirika kuimarika na si kudhoofu.

Eneo linalothibitisha hilo ni pale Waziri Mkuu aliposema; “Katika mwaka 2016/2017, Mahakama imesikiliza na kukamilisha mashauri 279,331 kati ya 335,962 katika ngazi zote za Mahakama sawa na asilimia 83.1 ya mashauri yote.”

Ukiondoa eneo jingine ni kitendo cha mahakama kusogeza huduma zake karibu na wananchi kwa kujenga au kukarabati majengo ya Mahakama katika mikoa mbalimbali, jambo linatoa ishara ya wazi ya chombo hicho kuzidi kuimarika.

Waziri Mkuu alisema pamoja na kazi kubwa ya kusikiliza mashauri, Mahakama imekamilisha ukarabati na ujenzi wa majengo ya Mahakama Kuu katika Mikoa ya Tanga na Dar es Salaam huku kazi ya ukarabati wa Mahakama Kuu katika Mkoa wa Mbeya ukiwa unaendelea.

Pia ujenzi wa Mahakama ya Wilaya na Mahakama ya Mwanzo katika maeneo mbalimbali ukiendelea. Eneo lingine pia ambalo hotuba hiyo ya Waziri Mkuu inadhihirisha nia ya serikali ya kutaka Mahakama kutekeleza kazi kwa ufanisi na kuwa huru ni pale anaposema;” Ili Mahakama ifanye kazi zake vizuri, shughuli za upepelezi wa kesi na uendeshaji wa mashitaka zinatakiwa pia kuimarishwa zaidi.

“Serikali itafanya kila liwezekanalo kuimarisha taasisi zote zinazohusika katika mlolongo wa utoaji haki ili wananchi wapate haki zao kwa wakati,” alisema Waziri Mkuu Majaliwa.

Akizungumzia mhimili mwingine wa Bunge, Waziri Mkuu alisema; “Ofisi ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, inatekeleza majukumu yake kwa ufanisi mkubwa.”

Pamoja na kueleza namna Bunge lilivyoweza kutekeleza majukumu yake ipasavyo, Waziri Mkuu aliahidi kuwa Serikali itaendelea kuliwezesha Bunge kutekeleza majukumu yake Kikatiba.

Katika kuonesha Bunge kutimiza wajibu wake; chombo hicho kimeweza kuratibu na kusimamia shughuli za mikutano mitatu ya Bunge ambapo maswali 1,054 ya kawaida, nyongeza na ya papo kwa hapo kwa Waziri Mkuu yaliulizwa.

Aidha Miswada 10 ya Sheria ilijadiliwa na kupitishwa na Bunge.

Bunge liliweza pia kuratibu na kusimamia shughuli za mikutano ya Kamati za Kudumu za Bunge kutoa huduma za utawala na kutoa mafunzo kwa wabunge huku kazi ya kukarabati jengo la Bunge na ukarabati na ujenzi wa ofisi za wabunge ukifanyika kikamilifu.

Bonyeza HAPA kudownload applicationi ya Bongojamii Blog kwenye simu yako ili kupata habari zetu Haraka

Featured Posts