Bonyeza HAPA kudownload applicationi ya Bongojamii Blog kwenye simu yako ili kupata habari zetu Haraka
BONYEZA HAPA KU-DOWNLOAD
Serikali ya Israel imeahidi kujenga jengo la wagonjwa mahututi (ICU) katika Hospitali ya Benjamin Mkapa Mkoani Dodoma kuanzia mwishoni mwa mwaka huu.
Hayo yamebainishwa na Balozi wa Israel hapa nchini Mhe. Yahel Vilan alipokutana na kufanya mazungumzo na Rais wa Tanzania Dkt. John Magufuli Ikulu Jijini Dar es Salaam, ambapo amemhakikishia kuwa Israel itaendelea kushirikiana kwa karibu na Tanzania.
Balozi Yahel Vilan pamoja na ujumbe wake amemueleza Mhe. Rais Magufuli kuwa wamefurahishwa na ziara waliyoifanya hapa nchini iliyowawezesha kukutana na viongozi mbalimbali na ameahidi kuwa Israel itaendelea kuunga mkono juhudi mbalimbali za maendeleo ikiwemo ujenzi wa viwanda, kilimo na kuimarisha huduma za matibabu kwa wananchi zinazofanywa na serikali ya Tanzania.
Kwa upande wake Rais Magufuli amesema ili kufanikisha dhamira hiyo Tanzania imefungua ubalozi nchini Israel na amemuomba Mhe. Yahel Vilan kupeleka ujumbe kwa Waziri Mkuu wa Israel Mhe. Benjamin Netanyahu kuwa Tanzania itafurahi kuona Israel inafungua ubalozi wake hapa nchini.
“Naamini uhusiano na ushirikiano wetu utaongeza manufaa zaidi kwa nchi zetu na watu wake, nimefurahishwa sana na taarifa kuwa watalii wataanza kuja kwa ndege moja kwa moja kutoka Tel Aviv Israel na hivi karibuni ndege yenye watalii zaidi ya 200 itakuja nchini kwetu, nawakaribisha sana watalii na wawekezaji kutoka Israel” amesema Rais Magufuli.
Wakati huo huo Rais Magufuli leoamefanya mazungumzo na Balozi wa Umoja wa Ulaya hapa nchini Mhe. Roeland Van de Geerna kuushukuru umoja wa nchi hizo kwa kutoa msaada wa Euro Milioni 205 sawa na takribani Shilingi Bilioni 500 kwa ajili ya kuunga mkono juhudi za maendeleo hapa nchini kwa kipindi cha miaka 4 kuanzia mwaka huu.
Bonyeza HAPA kudownload applicationi ya Bongojamii Blog kwenye simu yako ili kupata habari zetu Haraka