NDESAMBURO ASABABISHA MPASUKO CHADEMA KASKAZINI | BONGOJAMII

NDESAMBURO ASABABISHA MPASUKO CHADEMA KASKAZINI

Bonyeza HAPA kudownload applicationi ya Bongojamii Blog kwenye simu yako ili kupata habari zetu Haraka
BONYEZA HAPA KU-DOWNLOAD
Wiki iliyopita kulikuwa na uchaguzi ndani ya Chadema ulilenga kuwapata viongozi wa Kanda ya Kaskazini lakini ukahirishwa ghafla na siku ya mwisho.

Kuahirishwa kwa huo, licha ya kunaonekana kama ni tukio la kawaida kulizingira na mambo mengi yaliyojificha nyuma ya pazia.

Chadema imekuwa ikiendelea na mipango yake ya kupanga safu za uongozi kwa kuzingatia sera yake ya kugatua madaraka ya chama kitaifa kwa ngazi za Kanda na wiki iliyopita ilikuwa zamu ya Kanda ya Kaskazini – yaani mikoa ya Arusha, Kilimanjaro na Tanga ambako uchaguzi huo ulikuwa ufanyike.

Uchaguzi huo kulingana na vyanzo mbalimbali ndani ya chama hicho uliahirishwa kutokana na mvutano ulioibuka ndani ya Kamati Kuu ya Chadema iliyoketi Tanga, baada ya kuwapo shinikizo la kutaka mwenyekiti wa Chadema Kilimanjaro, Philemon Ndesamburo asigombee nafasi ya mwenyekiti wa Kanda.

Ndesamburo ambaye amekuwa mbunge wa Jimbo la Moshi mjini (2000-2015) alipoamua kutogombea, aliamua kuwania nafasi hiyo ya juu zaidi katika kanda akibebwa na rekodi yake ya kukijenga chama hicho mkoani Kilimanjaro na kuwa na nguvu kubwa.

Kilichozua sintofahamu ni juu ya mwanasiasa huyo maarufu kama Ndesa Pesa kuambiwa aondoe jina lake kutokana na uzee huku kukiwapo tuhuma za kukivuruga chama, madai yanayoelezwa kuanzia ndani ya Kamati Kuu ya chama iliyoketi Tanga.

Nyuma ya pazia
Taarifa zilizovuja kutoka ndani ya chama hicho zinadai katika kikao hicho kilichohudhuriwa na wajumbe wa Kamati Kuu na wabunge wa Kanda ya Kaskazini, Ndesamburo alihojiwa na Kamati Kuu kwa madai ya kukivuruga chama mkoani Kilimanjaro.

“Ndesamburo alihojiwa hasahasa madai kuwa yeye ndiye anakivuruga chama pale Moshi, kwamba ameshindwa kukisaidia na ndiye analea migogoro Kilimanjaro,” kilidokeza chanzo chetu.

Mbali na madai hayo, Ndesamburo aliombwa aondoe jina lake kwa sababu ya kile wajumbe wa Kamati Kuu walidai kuwa umri umemtupa, lakini inadaiwa mwanasiasa huyo alikataa kuondoa jina lake.

“Ndesamburo alikataa kuondoa jina lake kwa sababu miongoni mwa watu walioijenga Chadema Kilimanjaro ni yeye na katiba haijatoa kigezo cha umri wa kugombea uenyekiti.”

Imedokezwa kuwa baada ya kukataa kwake, iliundwa kamati ndogo yenye wajumbe wanne ikapewa jukumu la kwenda kumshawishi Ndesamburo aondoe jina.

“Hiyo kamati ilimfuata Ndesamburo na kumuomba aondoe fomu yake kwa ahadi kuwa wangempa nafasi ya mjumbe wa kudumu wa Kamati Kuu ya Chadema, lakini alikataa,” kilidokeza chanzo kingine.

Baada ya hatua hiyo kukwama, ndani ya kikao cha Kamati Kuu kuliibuliwa madai mengine kutoka kwa meya mmoja kuwa fomu za kugombea nafasi hiyo zilifichwa na alipewa Ndesamburo peke yake.

Inaelezwa kuwa meya huyo ambaye inadaiwa alikuwa na kundi linalomuunga mkono mgombea mwingine, Daniel Porokwa alipendekeza uchaguzi uahirishwe ili wanachama wengi wapate fursa ya kugombea.

Hata hivyo, habari zinasema madai hayo yalipingwa na uongozi wa Chadema na kueleza kuwa matangazo ya uchukuaji fomu yalitangazwa kwa uwazi na bila kificho na ilitolewa miezi minne.

Mbali na hoja hiyo, inadaiwa kuwa Mbunge wa Rombo, Joseph Selasini alisimama na kuwatuhumu Mbunge wa Moshi Mjini, Jaffar Michael na Lazaro kuwa ndiyo wanavuruga uchaguzi kwa vile hawamtaki Ndesamburo.

“Hiyo kauli ilichafua hali ya hewa kwa vile Jaffar alisimama na kurushiana maneno makali na (Joseph) Selasini (mbunge wa Rombo). Kama wangekuwa wenyewe ngumi zingelia mle ndani,” alidokeza mjumbe mmoja.

“Mgogoro wote huu ni uchaguzi wa 2020. Jaffar na Anthony Komu (mbunge wa Moshi Vijijini) wanaona kama Ndesamburo atakuwa mwenyekiti wa Kanda, nafasi yao ya kupitishwa itakuwa ndogo,” kilidokeza chanzo chetu.

Inadaiwa kuwa hofu hiyo inajengeka kwa sababu Ndesamburo na Jaffar hawaivi chungu kimoja na hawasalimiani, wakati Komu ana hofu inayotokana na kuenguliwa jina la binti wa Ndesamburo, Lucy Owenya kwenye ubunge na nafasi kupewa yeye.

Katika kura za maoni zilizopigwa, Owenya alipata kura 266 wakati Komu alipata kura 25, lakini Kamati Kuu ya Chadema baadaye ilimwengua Owenya na kurejesha jina la Komu na akashinda ubunge.

Mmoja wa watu waliokuwa viongozi wa Chadema mkoani Tanga ambaye aliomba jina lake lisitajwe, alidai kiongozi pekee wa kumlaumu kwa hicho kinachotokea ni Mwenyekiti wa Taifa, Freeman Mbowe.

“Binafsi namlaumu mwenyekiti wangu. Aliruhusije mzee Ndesamburo adhalilishwe vile ndani ya kikao cha Kamati Kuu? Hivi leo tunamlipa mzee wa watu yule wema kwa ubaya?” alihoji.

Hata hivyo, kiongozi mwingine alidai kuna mpasuko mkubwa ndani ya Chadema katika Manispaa ya Moshi unaochangiwa na kutokuelewana kati ya Ndesamburo na Jaffar.

Ndesamburo, Komu watoa ya moyoni
Ndesamburo alipotafutwa na gazeti hili kuzungumzia hatua ya yeye kutakiwa asigombee uenyekiti wa kanda, alisema yaliyojitokeza ndani ya kikao hawezi kuyazungumzia kwa sababu ni faragha.

“Unataka nikueleze nini? Mimi yote yanayoendelea namwachia Mungu na wala sitaongeza neno zaidi ya hapo. Mchango wangu kwenye chama unajulikana. Namwachia Mungu,” alisema Ndesamburo.

Alipoulizwa kuhusu mtafaruku huo, Komu alisema ni kweli hamuungi mkono Ndesamburo kuwa mwenyekiti wa kanda na hilo amelisema hata ndani ya kikao.

“Mimi ni kweli simuungi mkono mzee Ndesamburo kuwa mwenyekiti wa Kanda, lakini sina kundi ambalo nakaa nalo eti kufanya mikakati ya kumkataa. Mimi siyo mnafiki na ni muwazi. Kwenye hicho kikao nilitoa hoja ya umri. Hata kwenye Kanisa Katoliki ukiwa na umri wa miaka 75 unaacha uaskofu, lakini mzee Ndesamburo ana umri wa miaka 84,” alisisitiza Komu.

Mbali na hoja ya umri, mbunge huyo alisema anapinga Ndesamburo kuwa mwenyekiti kwa sababu katika uongozi wake wa mkoa wa Kilimanjaro kumekuwapo na vurugu na mpasuko ndani ya chama.

“Kila mahali hapo (Kilimanjaro) kuna vurugu watu hawaelewani, kwa hiyo mnataka tuhamishie vurugu zihamie kwenye kanda? Huu ndiyo msimamo wangu wala simpingi kwa sababu nyingine,” alisema.

Hata hivyo, mbunge mmoja kutoka moja ya mikoa ya Kaskazini ambaye alikataa kutajwa alitaka suala la umri lisiwe kigezo kwani siyo la kikatiba, hivyo wapigakura ndiyo wapewe fursa ya kuchagua kiongozi wanayemtaka.

“Tusimbebeshe Ndesamburo migogoro kwenye majimbo ya Hai, Moshi Vijijini, Moshi Mjini na Rombo, tena huko kuna viongozi wa kitaifa. Migogoro ni kielelezo taasisi iko hai,” alisema.

Selasini alipotafutwa aeleze tafrani iliyotokea kati yake na Jaffar alisema hawezi kuzungumza lolote na anaheshimu taratibu za vikao.

Akizungumzia mtafaruku huo, Jaffari alisema hayo ni mambo ya ndani ya chama hawezi kuyazungumzia nje.

Bonyeza HAPA kudownload applicationi ya Bongojamii Blog kwenye simu yako ili kupata habari zetu Haraka

Featured Posts