YANGA KUIVAA MC ALGER BILA TAMBWE WALA CHIRWA LEO | BONGOJAMII

YANGA KUIVAA MC ALGER BILA TAMBWE WALA CHIRWA LEO

Bonyeza HAPA kudownload applicationi ya Bongojamii Blog kwenye simu yako ili kupata habari zetu Haraka
BONYEZA HAPA KU-DOWNLOAD
TAMBWE
WAWAKILISHI pekee wa Tanzania waliobakia kwenye mashindano ya kimataifa, Yanga, leo wanatarajia kushuka ugenini kuwavaa wenyeji MC Alger katika mechi ya marudiano kuwania nafasi ya kucheza hatua ya makundi ya mashindano ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Mechi hiyo kati ya MC Alger dhidi ya Yanga itafanyika kuanzia saa 4:00 usiku saa za hapa nyumbani na mabingwa hao watetezi wataingia uwanjani wakiwa mbele kwa bao 1-0, shukrani kwa kiungo Thabani Kamusoko aliyefunga bao hilo.

Kocha Msaidizi wa timu hiyo, Juma Mwambusi, alisema jana kuwa watashuka uwanjani kumalizia kazi waliyoianza katika mchezo wa kwanza uliofanyika wiki iliyopita kwenye Uwanja wa Taifa jijini, Dar es Salaam huku wakicheza kwa tahadhari.

Mwambusi alisema kuwa tayari wameshazijua mbinu za wapinzani wao na sasa jukumu ambalo wamejiandaa ni kuhakikisha wanazuia wapinzani wao kupata nafasi ya kumiliki na kutawala mpira ili wasitengeneze mashambulizi kuelekea langoni mwao.

"Mechi ni ngumu, lakini tunashuka kuwavaa wapinzani wetu huku tukiamini hakuna lisilowezekana, tumewaona na tumejiandaa vizuri kuwakabili, kikubwa ni kuwa makini kwa kiwango cha juu, hawa ukifanya kosa moja ujue umewaruhusu kukujeruhi," alisema Mwambusi.

Yanga katika mechi ya leo itamkosa mshambuliaji wake Mzambia, Obrey Chirwa aliyeachwa nchini huku Donald Ngoma bado kiwango chake kikiwa haijaimarika wakati straika Mrundi Amissi Tambwe hakuwa hata kwenye orodha ya akiba katika mechi ya kwanza.

Mwaka jana Yanga ilitinga hatua ya makundi ya michuano hiyo baada ya kuitoa Sagrada Esperanca ya Angola, ilitolewa katika mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika na Al Ahly ya Misri.

Bingwa mtetezi wa michuano hiyo inayofanyika kila mwaka ni TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) ambayo pia mwaka huu ilianzia kwenye mashindano ya Ligi ya Mabingwa wa Afrika.

Wakati huo huo uongozi wa Yanga umesitisha uamuzi wake wa kwenda mahakamani kupinga hatua ya mahasimu wao Simba kupewa pointi tatu baada ya kushinda rufani waliyokata dhidi ya Kagera Sugar iliyomtumia Mohammed Fakhi ambaye alikuwa na kadi tatu za njano.

Bonyeza HAPA kudownload applicationi ya Bongojamii Blog kwenye simu yako ili kupata habari zetu Haraka

Featured Posts