KITWANGA AIKALIA KOONI SERIKALI , ATISHIA KUZIMA MTAMBO WA MAJI ULIOKO ZIWA VICTORIA | BONGOJAMII

KITWANGA AIKALIA KOONI SERIKALI , ATISHIA KUZIMA MTAMBO WA MAJI ULIOKO ZIWA VICTORIA

Bonyeza HAPA kudownload applicationi ya Bongojamii Blog kwenye simu yako ili kupata habari zetu Haraka
BONYEZA HAPA KU-DOWNLOAD
Mbunge wa Misungwi, Charles Kitwanga (CCM), amewapiga mkwara mawaziri bungeni kuwa atahamasisha wananchi wa jimbo lake kwenda kuzima mtambo wa maji ulioko Ziwa Victoria.

Kitwanga ambaye alikuwa Waziri wa Mambo ya Ndani wa kwanza katika serikali ya awamu ya tano, alilieleza Bunge jana kuwa mtambo huo upo kwenye chanzo cha maji cha Iherere, kilichoko jimboni kwake Misungwi mkoani Mwanza.


Katika mjadala wa makadirio ya bajeti ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji bungeni mjini Dodoma jana mchana, mbunge huyo aliyekuwa wa kwanza kupewa nafasi ya kuchangia, alitoa onyo hilo kwa Waziri Gerson Lwenge na msaidizi wake, Mhandisi Isack Kamwele, kwamba yuko mbioni kuuzima mtambo huo ikiwa wananchi wake hawatakuwa sehemu ya mradi huo wa maji.


“Mheshimiwa Naibu Spika, jimboni kwangu hakuna maji ya uhakika na tangu mwaka 2008 wananchi wamekuwa wakiyasubiri bila mafanikio,"Kitwanga alisema.


“Kwa hiyo, nitakachokifanya safari hii, sitatoa shilingi kwenye bajeti, bali nitakwenda kuwahamasisha wananchi wa Misungwi wapatao 10,000, twende tukazime mtambo katika kile chanzo cha maji ili wote tukose.


“Wanamchi wa Misungwi hawana maji na katika bajeti yenu leo (jana) mmesema Nyang’omango kuna maji wakati hakuna, sasa nawaambia, sitatoa shilingi 'nita-mobilize' (nitahamasisha) wananchi tukazime ule mtambo.


“World Bank' (Benki ya Dunia) walifika pale kijijini, wakasema hawa wananchi walioko kwenye kile chanzo wanatakiwa kupata maji, lakini nyie hamuoni, hivi nyie mkoje?


“Nakipenda chama changu (CCM), nampenda Rais wangu (John) Magufuli, lakini lazima tutendeane haki kwa sababu hii nchi ni yetu sote.


“Hamuwezi kupeleka maji sehemu nyingine kwa gharama ya Sh. bilioni 600 halafu mkashindwa kuwapa wananchi wangu hata mradi wa Sh. bilioni 10.


“Mshukuru kwamba nilipokuwa waziri, nilikuwa siwezi kusema kitu, lakini sasa nimetoka, tutapambana kwa sababu lazima tuwe na mipango mizuri ya kuwapelekea wananchi wetu maji kama inavyofanyika katika umeme kupitia REA (Wakala wa Umeme Vijijini).”


Kitwanga alitumbuliwa na Rais Magufuli Mei 20, mwaka jana kwa tuhuma za kuingia bungeni na kujibu swali linalohusu Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi akiwa amelewa.


Kitwanga pia alilalamikia kile alichokiita tabia ya baadhi ya viongozi wa wizara hiyo kukwamisha upatikanaji wa maji kupitia kwa marafiki zake kutoka nchini Austria.


“Rais alipokuja Misungwi, aliwaambia wananchi, kwamba nina marafiki zangu huko nje wanaoweza kunisaidia kupata maji," alisema. "Ule mradi ulipokuja, nikawekewa figisu wakasema mimi nina 'interest' (maslahi) nao.


"Ni kweli nina 'interest' nao kwa sababu wananchi wangu wa Kolomije wanahitaji maji, wananchi wa Bukumbi wanahitaji maji.


“Kwa hiyo, Mheshimiwa Naibu Spika, narudia tena, safari hii sitatoa shilingi, nitakwenda kuwahamasisha wananchi wangu tukazime ule mtambo wa maji ili wote tukose,” alisisiza Kitwanga.


Hata hivyo, muda mfupi kabla ya kusitisha shughuli za Bunge jana mchana, Naibu Spika wa Bunge, Dk. Tulia Ackson, alimtahadharisha Kitwanga kuwa, uamuzi wake huo huenda ukamsababishia matatizo kwa kuwa unakiuka sheria za nchi.


Dk. Tulia alisema kuwahamasisha wananchi ili wavunje sheria ni kosa la jinai, hivyo mbunge huyo anapaswa kuwa makini kwa kuwa anaweza kuchukuliwa hatua kabla hata hajawahamasisha wananchi wa maeneo ya Kolomije na jimbo zima la Misungwi.

Bonyeza HAPA kudownload applicationi ya Bongojamii Blog kwenye simu yako ili kupata habari zetu Haraka

Featured Posts