SAKATA LA ZIWA NYASA KATI YA TANZANIA NA MALIWI LAIBUKA TENA | BONGOJAMII

SAKATA LA ZIWA NYASA KATI YA TANZANIA NA MALIWI LAIBUKA TENA

Bonyeza HAPA kudownload applicationi ya Bongojamii Blog kwenye simu yako ili kupata habari zetu Haraka
BONYEZA HAPA KU-DOWNLOAD
SERIKALI imesema mazungumzo ya kutafuta suluhu ya mgogoro wa mpaka katika Ziwa Nyasa kati ya Tanzania na Malawi yanatarajiwa kuanza tena wakati wowote kuanzia sasa.


Hayo yalisemwa bungeni mjini hapa jana na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dk. Augustine Mahiga, alipowasilisha makadirio ya bajeti ya wizara yake kwa mwaka ujao wa fedha.


Alisema mazungumzo hayo yatafanyika chini ya usuluhishi wa Rais Mstaafu wa Msumbiji na Mwenyekiti wa Jukwaa la Viongozi na Wakuu wa Nchi Wastaafu wa Umoja wa Afrika, Joaquim Chissano, akisaidiwa na Rais Mstaafu wa Afrika Kusini, Thabo Mbeki.


”Wizara inasubiri kupata tarehe rasmi ya kuanza kwa mazungumzo hayo kutoka Ofisi ya Rais Mstaafu, Mheshimiwa Chissano," alisema.


Balozi Mahiga alisema mkutano wa Tume ya Pamoja ya Kudumu ya Ushirikiano kati ya Tanzania na Malawi ulifanyika Lilongwe, Malawi Februari mwaka huu.


Alisema kuwa katika mkutano huo, masuala mbalimbali ya ushirikiano katika nyanja za kiuchumi, siasa, usalama, usafirishaji, nishati, uendekezaji wa Bonde la Mto Songwe na biashara yalijadiliwa na makubaliano kufikiwa.


Alisema Tanzania na Malawi zilitia saini mikataba miwili ya Huduma za Anga na Mashauriano ya Kidiplomasia na kwamba mkutano huo ulizidi kuimarisha uhusiano uliopo kati ya Tanzania na Malawi.


Waziri huyo pia alilieleza Bunge jinsi Tanzania inavyonufaika na uhusiano mzuri kati yake na nchi zingine zikiwamo Qatar, Kuwait, Morocco, Irael Iran, China, India, Zambia, Kenya, Uganda, Ethiopia, Afrika Kusini, Cuba, Czech, Finland, Uswisi, Canada, Uturuki, Japan, Jamhuri ya Korea na Umoja wa Falme za Kiarabu.


MKATABA WA EPA
Balozi Mahiga pia alisema uchambuzi uliofanyika kuhusu Mkataba wa Ubia wa Kiuchumi baina ya Jumuiya ya Afrika Mashariki na Jumuiya ya Ulaya (EAC-EU Economic Partinership Agreement - EPA) si rafiki kwa ustawi wa Tanzania hasa katika utekelezaji wa azma ya serikali ya awamu ya tano ya kuifanya Tanzania kuwa nchi ya uchumi wa viwanda.


Alisema mkutano wa 18 wa Viongozi Wakuu wa Nchi za Afrika Mashariki ulofanyika Dar es Salaam mwezi huu ulijadili suala hilo na kukubaliana Rais wa Uganda ambaye ni Mwenyekiti wa jumuiya, kuongoza ujumbe kwenda Umoja wa Ulaya kwa lengo la kutafuta mwafaka wa namna ya kuondoa changamoto ya changamoto zilizopo katika mkataba huo.


Alisema ujumbe huo pia unalenga kuushawishi Umoja wa Ulaya kutoiadhibu Kenya wakati majadiliano ya kutafuta mwafaka yakiendelea.


Ili kutekeleza majukumu yake kwa mwaka ujao wa fedha, Balozi Mahiga aliliomba Bunge kuidhinisha Sh. bilioni 150.845 kwa ajili ya bajeti ya wizara yake. Kati yake, Sh. bilioni 142.845 ni za matumizi ya kawaida na Sh. bilioni nane ni kwa ajili ya miradi ya maendeleo.


Balozi Mahiga pia alisema kuwa kati ya Sh. bilioni 142.845 zilizotengwa kwa ajili ya matumizi ya kawaida, Sh. milioni 410 ni kwa ajili ya Mpango wa Kujitathmini Kiutawala Bora Tanzania.


Katika mwaka wa fedha 2016/17, wizara hiyo iliidhinishiwa Sh. bilioni 162.109. Kati yake, Sh. bilioni 154.109 ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida na Sh. bilioni nane kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo.


Mahiga alisema kuwa hadi, Aprili 30, mwaka huu, wizara yake ilikuwa imepokea Sh. bilioni 95.038 sawa na asilimia 56 ya fedha zote zilizoidhinishwa na Bunge. Kati yake, Sh. bilioni 83.039 ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida na Sh. bilioni 3.489 ni za miradi ya maendeleo.

Bonyeza HAPA kudownload applicationi ya Bongojamii Blog kwenye simu yako ili kupata habari zetu Haraka

Featured Posts