SERIKALI YAANIKA SIRI YA KUBORONGA KWENYE MICHEZO | BONGOJAMII

SERIKALI YAANIKA SIRI YA KUBORONGA KWENYE MICHEZO

Bonyeza HAPA kudownload applicationi ya Bongojamii Blog kwenye simu yako ili kupata habari zetu Haraka
BONYEZA HAPA KU-DOWNLOAD
SERIKALI imeeleza sababu za Tanzania kufanya vibaya kwenye sekta ya michezo kwa kipindi cha zaidi ya miaka 3O iliyopita.

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Harrison Mwakyembe, akiwasilisha bungeni mjini hapa jana hotuba ya bajeti ya wizara yake, alisema sababu kuu ya kutofanya vizuri katika sekta hiyo ni matarajio ya mafanikio bila kujenga mazingira stahili ya mafanikio yanayosubiriwa.

"Ni miaka 37 imepita tangu nchi yetu ifanikiwe kufika ngazi ya nusu fainali za AFCON, mara zote tunaishia raundi ya kwanza au ya pili. Sababu ni matarajio ya mafanikio bila kujenga mazingira stahili ya mafanikio. Sasa tumefungua ukurasa upya," alisema.

Alibainisha kuwa miaka zaidi ya 30 imepita toka Tanzania ing’are kimataifa katika medani za riadha kupitia wanariadha wake mashuhuri wakati huo, wakiwamo Francis Naali, Samson Ramadhan, Gidamis Shahanga, Juma Ikangaa, Suleiman Nyambui na Filbert Bayi ambaye aliweka rekodi mpya ya dunia katika mbio za mita 1,500 mwaka 1974 huko Christchurch, New Zealand.

Mbali na riadha, Mwakyembe alisema Tanzania imeyumba kwenye michezo mingine ukiwamo mpira wa miguu ambao kwa kiasi kikubwa nchi imepotea kwenye ramani ya michezo duniani.

Alisema nchi inajivunia mwanariadha Alphonce Simbu, aliyeshika nafasi ya tano katika mashindano ya Olimpiki nchini Brazil mwaka jana upande wa mbio ndefu na baadaye mwaka huu, akashinda na kupata medali ya dhahabu kwenye mashindano ya Mumbai Marathon, India.

Alisema nchi pia inajivunia mwanariadha Cecilia Ginoka Panga, aliyekuwa mshindi wa kwanza kwenye mashindano ya Beijing International Half Marathon, Magdalena Crispin Shauri aliyeshika nafasi ya tano katika mbio za Hamburg na Emmanuel Giniki Gisamoda alikuwa mshindi wa kwanza kwenye Shanghai International Half Marathon huku pia ikiipongeza Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa kwa kuibua na kuendeleza vipaji vya michezo nchini kwani wanariadha wote hao wanne wapo JKT.

Naye Mbunge wa Mafinga Mjini, Cosato Chumi (CCM), ameanika kile alichokiita kiini cha Tanzania kuboronga kwenye viwango vya soka vinavyotolewa kila mwezi na Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa ) huku akidai kuwa Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Jamal Malinzi ambaye alikuwa miongoni mwa wageni waalikwa anahusika kwa kiasi kikubwa.

Mbunge huyo msomi alisema kuporomoka huko kwa Tanzania kwenye viwango cha soka hadi kuzidiwa na nchi zinazokabiliwa na vita ikiwamo Afghanistan kumesababishwa na uongozi wa sasa wa TFF.

Alisema kuwa katika uongozi huo wa Malinzi, timu ya taifa (Taifa Stars) imekuwa ikicheza mechi chache za kimataifa zilizopo kwenye kalenda ya FIFA, akidokeza kuwa mwaka 2016 timu hiyo ilicheza mechi tatu za kwenye kalenda hiyo wakati Rwanda walicheza mechi sita.

"Vifungo ni vikubwa mno. Unamfungia mtu miaka 10. Hata kwenye soka la kina (Lionel) Messi na (Cristiano) Ronaldo hakuna kitu kama hicho." alisema.

Baada ya mbunge huyo kuchangia, Mwenyekiti wa Bunge, Mussa Zungu, alimtambulisha Malinzi bungeni huku Mbunge wa Sumbawanga Mjini na Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), Aeshi Hilaly (CCM), akisikika akisema "ametunyang'anya pointi huyo".

Bonyeza HAPA kudownload applicationi ya Bongojamii Blog kwenye simu yako ili kupata habari zetu Haraka

Featured Posts