LOWASA AMPONGEZA RAIS MAGUFULI KWA KAZI NZURI ANAYOFANYA | BONGOJAMII

LOWASA AMPONGEZA RAIS MAGUFULI KWA KAZI NZURI ANAYOFANYA

Bonyeza HAPA kudownload applicationi ya Bongojamii Blog kwenye simu yako ili kupata habari zetu Haraka
BONYEZA HAPA KU-DOWNLOAD
Aliyekuwa Waziri Mkuu wa Tanzania, Edward Lowassa amempongeza Rais Magufuli kwa hatua anazozichukua kuhusu madini ya nchi yetu. 


Lowassa aliyayasema hayo jana alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu sakata la mchanga wa madini (makinikia) ambalo limeonyesha kuwa Tanzania impoteza zaidi ya trilioni 100 tangu mwaka 1998 hadi Machi mwaka 2017.


“Nimpongeze sana Mhe Rais John Pombe Magufuli kwa uamuzi na hatua ambazo amechukua kuhusu jambo hili, na hasa pale anapowashirikisha wananchi, ni jambo muhimu sana." Alisema Lowassa


Lowassa ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya CHADEMA alisema anampongeza Rais Magufuli kwa kutekeleza maamuzi ambayo ni ya UKAWA kwani kipindi anazunguka kuomba kura kwa wananchi alipopita maeneo yenye madini aliyazungumza haya yanayotekelezwa leo.


“Nampongeza kwa kutekeleza yale maamuzi ambayo ni ya UKAWA. Nilipokuwa kwenye kampeni ya kuomba kura, hata pale Geita, nilieleza jambo hilo, nikasema hivyo hivyo alivyosema yeye kwamba nikiingia madarakani nitaunda tume ya kuchunguza jambo hili ili mtanzania awe ndiye anapata sehemu kubwa ya faida kuliko mgeni.”


Aidha, Lowassa amesema kuwa, ni kweli mikataba ya madini ina matatizo na hata yeye alipoteuliwa kuwa Waziri Mkuu aliwaita wawekezaji hao wakakaa na kuzungumza, lakini jambo gumu lilikuwa ni kwamba, mikataba ukishaiweka saini inakuwa migumu sana kubadilisha.


Lowassa alieleza kwamba baada ya kuongea nao kwa muda walikubali na kuongeza kidogo mirahaba lakini haikutosha.


“Matumaini yangu ‘figure’ (namba) hizo ni za kweli, kama ni za kweli, tumeliwa kweli kweli,” alisema Lowassa alipokuwa akizungumzia mahesabu yaliyowasilishwa katika ripoti za uchunguzi kuhusu kiasi cha fedha ambazo Tanzania imepoteza.

Aidha, Lowassa alisema kuwa sera za Chama cha Mapinduzi (CCM) ndiyo zimefikisha nchi hapa kwani wakati wabunge wa CCM wanapiga kura kukubali mikataba hiyo walikuwa wakitimiza sera za chama hicho. kwahiyo vyama pinzani havina tatizo.

Hivyo alieleza kuwa kikubwa kinachohitajika ni kupatikana kwa katiba mpya ambayo itazingatia mambo hayo ya msingi na haki za raia.

Bonyeza HAPA kudownload applicationi ya Bongojamii Blog kwenye simu yako ili kupata habari zetu Haraka

Featured Posts