KILICHOTOKEA KABLA YA AJALI ILIYOUA WAPAMBE 3 WA CUF | BONGOJAMII

KILICHOTOKEA KABLA YA AJALI ILIYOUA WAPAMBE 3 WA CUF

Bonyeza HAPA kudownload applicationi ya Bongojamii Blog kwenye simu yako ili kupata habari zetu Haraka
BONYEZA HAPA KU-DOWNLOAD

MAJERUHI wa ajali ya Noah na lori iliyoua wanachama watatu wa Chama cha Wananchi (CUF), papo hapo juzi usiku mkoani Pwani wakati wakitoka mkoani Dodoma, wametaja chanzo cha ajali hiyo.


Katika ajali hiyo iliyotokea eneo la Ubena Zomozi, Barabara ya Morogoro wilaya ya kipolisi ya Chalinze, ilisababisha vifo vya watu watatu na wengine nane kujeruhiwa vibaya. Wamelazwa katika Hospitali ya Tumbi, Kibaha.


Wanachama hao walikuwa wanatoka Dodoma katika sherehe za kuapishwa kwa wabunge wapya saba wa viti maalum wa CUF, wakielekea Muheza mkoani Tanga ambako ndiko wanakoishi.


Taarifa ya Kamanda wa Polisi mkoani Pwani, Jonathan Shana alisema ajali hiyo, ilitokea saa nane usiku na ilihusisha gari aina ya Toyota Noah yenye namba za usajili T968 CKS iliyokuwa ikiendeshwa na Uledi Sarumaa (41) mkazi wa Muheza.


Alisema Noah hiyo, iligongana na lori aina ya Scania yenye namba za usajili T929 CBK na tela T472 CAX lililokuwa likiendeshwa na Yasini Kanoni (32), mkazi wa Dar es Salaam.


Kwa mujibu wa taarifa kutoka Hospitali ya Tumbi, waliofariki katika ajali hiyo ni Sarumaa ambaye mkurugenzi wa uchumi na fedha wa CUF wilaya ya Muheza, Mary Komba (40) mwenyekiti wa mtaa wa Shembekeza wilayani humo na mwingine aliyejulikana kwa jina moja la Isack.


Miili yao yote imehifadhiwa katika hospitali hiyo na ndugu walikuwa wakiendelea na taratibu za kuichukua kwa ajili ya mazishi jana.


Akizungumza huku akiwa na maumivu makali na akiwa amelazwa hospitalini hapo, Juma Nindi (41) ambaye ni katibu mwenezi wa CUF wilaya ya Muheza alisema dereva wa Noah waliyokuwa wamepanda, marehemu Sarumaa aliyumba barabarani baada ya kupigwa mwanga mkali wa taa za lori hivyo kusababisha magari hayo kugongana.


“Tulishtukia magari yamegonga na wakati nachukuliwa kuwahishwa hospitali nilikuwa najitambua," alisema Nindi. "Baada ya matibabu najisikia vizuri kiasi japo bado nina maumivu kwenye kifua na maeneo mengine mwilini.”


Ibrahimu Mohamed (41) ambaye ni mkurugenzi wa siasa wa CUF wilaya ya Muheza alisema wakiwa majeruhi nane walipelekwa kituo cha afya Chalinze na kutoka huko, yeye, Nindi na majeruhi mwingine mmoja walihamishiwa Tumbi kwa kuwa hali zao zilikuwa mbaya.


Taarifa za ndani kutoka katika Hospitali ya Tumbi zimetaja majeruhi wa tatu huyo kuwa ni Chausiku Mohamed (40) na kwamba hali yake ni mbaya huku madaktari wakiendelea kushughulikia afya yake jana.


SUSIA KUAPISHWA
Shughuli ya kuapishwa kwa wabunge wapya wa CUF hao ambao wameteuliwa na upande wa mwenyekiti wa chama hicho anayetambuliwa na Msajili wa Vyama vya Siasa Prof. Ibrahim Lipumba, kulisusiwa na wabunge wa kambi ya upinzani juzi.


Wabunge walioapishwa ni Alfredina Kahigi, Kiza Mayeye, Nuru Ahmed Kassim, Shamsia Aziz Mtamba, Sonia Magogo na Zainab Mndolwa Amir.


Kaimu Naibu Mkurugenzi wa Habari, Uenezi na Mahusiano wa Umma wa Chama cha Wananchi (CUF) upande wa Maalim Seif Shariff Hamad, Mbarala Maharagande alisema wafuasi wa Profesa Lipumba walioapishwa waliandaliwa dhifa usiku na wabunge wa CCM.


Katika zoezi la kuapishwa wabunge hao, wabunge waliokuwapo ndani ya ukumbi ni Mbunge wa Kaliua Magdalena Sakaya, Mbunge wa Mtwara mjini Maftaha Nachuma na Mbunge wa Kinondoni Maulid Mtulia wote wa CUF huku wengine wakiwa nje ya ukumbi wakiwa wamevaa mavazi meusi.


Akizungumza nje ya bunge, Katibu wa Wabunge wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), David Silinde alisema waliamua kuvaa mavazi hayo kuonyesha kifo cha demokrasia na kwamba walisusa kuingia ndani ya ukumbi kushiriki zoezi la kuapishwa wabunge hao kwasababu wanapinga kitendo hicho.


“Tunapinga bunge kutumika na hatutashirikiana nao hadi kesi ya msingi iliyopo mahakamani ikamilike," alisema Silinde. "Hatutaki Bunge liendelee kutumika kwa upendeleo, tunataka liwe huru kama mahakama nchini Kenya ilivyo huru.”


Baadhi ya wabunge wa CCM, akiwamo Mbunge wa Ulanga, Goodluck Mlinga, na Juliana Shonza na Catherine Magige wa viti maalum kutoka chama tawala waliwasindikiza wabunge hao kuapishwa huku wengine wakishangilia.

Bonyeza HAPA kudownload applicationi ya Bongojamii Blog kwenye simu yako ili kupata habari zetu Haraka

Featured Posts