MANENO YA LOWASA BAADA YA KUMTEMBELEA TUNDU LISSU HOSPITALI | BONGOJAMII

MANENO YA LOWASA BAADA YA KUMTEMBELEA TUNDU LISSU HOSPITALI

Bonyeza HAPA kudownload applicationi ya Bongojamii Blog kwenye simu yako ili kupata habari zetu Haraka
BONYEZA HAPA KU-DOWNLOAD

Waziri mkuu wa zamani, Edward Lowassa
Dar es Salaam. Wakati mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu akiendelea kupata matibabu jijini Nairobi, waziri mkuu wa zamani, Edward Lowassa amemtembelea na kutamka maneno manane.

Katika akaunti yake ya mtandao wa kijamii wa Tweeter iliyosambaa katika mitandao mbalimbali ya kijamii Lowassa aliandika, ‘Ni wakati mgumu kwa Tanzania wote tunapaswa kuomba.”

Mwanasiasa huyo aliongeza kuwa “mapema leo (jana) nilitembelea Hospitali ya Nairobi na kumwona mbunge na Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), rafiki kipenzi Tundu Lissu anaendelea vizuri.”

Lissu, ambaye pia ni mwanasheria mkuu wa Chadema, alishambuliwa kwa risasi Alhamisi iliyopita wakati akiwa katika gari lake lililoegeshwa nje ya majengo ya nyumba anayoishi Area D mjini Dodoma muda mfupi baada ya kutoka bungeni.

Katika picha aliyoiweka kwenye mtandao wa Tweeter, Lowassa anaonekana akiwa na mke wa Lissu, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na dereva wa mbunge huyo anayejulikana kwa jina la Simon Bakari.

Dk Mashinji ahojiwa

Wakati hayo yakiendelea, Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Vincent Mashinji amehojiwa na Jeshi la Polisi kuhusiana na kupigwa risasi mbunge huyo.

Dk Mashinji alihojiwa jana makao makuu ya Jeshi la Polisi katika ofisi za Mkurugenzi wa Upelelezi wa Jinai (DCI) jijini Dar es Salaam kama alivyoelekezwa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Gilles Muroto.

Kamanda Muroto alimtaka Dk Mashinji afike ofisi ya upelelezi wa makosa ya jinai mkoani Dodoma au ofisi kama hiyo iliyopo Kituo Kikuu cha Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam ili kutoa ushirikiano kwa jeshi hilo kuhusu tukio la kushambuliwa kwa risasi Lissu.

Alipomaliza kuhojiwa, Dk Mashinji alisema polisi walitaka kujua kuhusu kauli zake za watu wasiojulikana kama anaweza akawajua.

“Watu wasiojulikana ambao tulikuwa tunawaongelea ni kwamba imezoeleka kwa polisi kuna tukio kubwa wanasema watu wasiojulikana, kwa hiyo lengo langu lilikuwa ni kuita wananchi sasa kurudi kwenye polisi jamii ili kuondokana na hii watu wasiojulikana,” alisema Dk Mashinji.

Mbunge aomba mwongozo

Mbunge wa Baraza la Wawakilishi (CCM), Jaku Hashim Ayoub jana aliomba mwongozo wa Spika akitaka Bunge liteue wabunge wa kwenda kumuona Lissu.

Akizungumza baada ya kipindi cha matangazo ya wageni bungeni jana, Jaku alisema Naibu Spika, Dk Tulia Ackson alifanya kitendo cha kibinadamu kuruhusu gari la ndugu zake limpeleke Lissu hospitali.

Alisema kwa ubinadamu, anaomba mwongozo wa Spika wateuliwe wabunge kwenda kumuona Lissu jijini Nairobi.

Akijibu mwongozo huo, Dk Tulia alisema wapo wabunge waliopo Nairobi ambao humpelekea taarifa Spika kila wakati juu ya hali ya mbunge Lissu. Aliwataja wabunge hao kuwa ni Freeman Mbowe ambaye ni mbunge wa Hai na mwenyekiti wa Chadema, pia Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni.

Mwingine ni Mbunge wa Iringa Mjini (Chadema), Mchungaji Peter Msigwa.

Maaskofu wasema ni aibu

Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), limelaani shambulio lililotekelezwa na watu wasiojulikana dhidi ya Lissu.

Baraza pia limeungana na Watanzania kulaani kwa nguvu zote matendo yote ya vurugu, mauaji na uvunjifu wa amani nchini.

Tamko la baraza hilo lililosainiwa na Makamu wa Rais wa TEC, Askofu Beatus Kinyaiya lilitolewa baada ya kikao cha kawaida kilichofanyika kwa siku mbili Septemba 9 na 10 jijini Dar es Salaam.

“Katika Taifa letu sasa tunashuhudia matendo ya mauaji ya watu wasio na hatia kama ilivyokuwa kule Mkuranga, Rufiji na Kibiti; utekwaji wa watu na kuteswa, utekaji wa watoto, ulipuaji wa ofisi za watu na hivi karibuni shambulio la mbunge Lissu,” lilisema baraza hilo katika tamko lake.

TEC ilieleza katika taarifa hiyo kwamba vurugu na mashambulizi ya aina yoyote ile yanalifedhehesha Taifa kwa kuwa matendo hayo ni dhambi, uhalifu na si utamaduni wa Mtanzania, hivyo vyombo vinavyohusika havina budi kuyakomesha mara moja.

Juzi, baadhi ya viongozi wa kidini waliungana na watu wengine kuendelea kulaani shambulio hilo na kumuombea Lissu arudi katika hali yake.“Naomba tusimame kidogo nizungumze jambo, nimesema leo nitakuwa na ibada maalumu ya kumuombea Lissu,” alisema Askofu Josephat Gwajima wa Kanisa la Ufufuo na Uzima wakati wa mahubiri yake.

Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Askofu Fredrick Shoo aliwataka watu waovu watambue kumuondoa Lissu mmoja, kutazalisha wengine maelfu.

Akizungumza na gazeti hili kwa simu kutoka Bonn, Ujerumani, Askofu Shoo alitoa wito kwa Serikali kuhakikisha wote waliohusika wanakamatwa.

“Tundu Lissu amekuwa mstari wa mbele kufunua ufisadi unaoendeshwa na wababe wachache. Hawa sasa wanaona wameanza kutikiswa na kwa kuwa kwao wingi wa mali na pesa ndio mungu wao. Hatushangai wakitumia kila njia kuzuia ufisadi wao usianikwe hadharani. Watajaribu kila njia kuzuia ukweli, lakini wanasahau kuwa ukweli hauzuiliki milele, kuna siku utajitokeza tu.

Mwinjilisti kiongozi wa Mtaa wa Saranga ulio chini ya Usharika wa Temboni KKKT, David Kawesa aliongoza maombi kumuombea Lissu.

Bonyeza HAPA kudownload applicationi ya Bongojamii Blog kwenye simu yako ili kupata habari zetu Haraka

Featured Posts