Okwi atupia 2, Bocco 1, Mambo yalikuwa hivi Simba Vs Mwadui Fc | BONGOJAMII

Okwi atupia 2, Bocco 1, Mambo yalikuwa hivi Simba Vs Mwadui Fc

Bonyeza HAPA kudownload applicationi ya Bongojamii Blog kwenye simu yako ili kupata habari zetu Haraka
BONYEZA HAPA KU-DOWNLOAD

SIMBA SC imewapa burudani ya nafsi mashabiki wake leo baada ya ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Mwadui FC ya Shinyanga katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.


Nyota wa mchezo wa leo kwa mara nyingine amekuwa mshambuliaji Mganda, Emmanuel Okwi aliyefunga mabao mawili na kufikisha mabao matano katika mechi mbili tu za Ligi Kuu alizocheza msimu huu, kufuatia kufunga mabao matatu katika ushindi wa 7-0 dhidi ya Ruvu Shooting kwenye mchezo wa kwanza.


Katika mchezo huo uliochezeshwa na marefa Emmanuel Mwandembwa, aliyesaidiwa na Joseph Masija na Michael Mkongwa, hadi mapumziko Simba walikuwa mbele kwa bao 1-0.


Bao hilo lilifungwa dakika ya saba na Okwi aliyekosa mchezo uliopita wa Simba ikitoa sare ya 0-0 na Azam Jumamosi iliyopita Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam kutokana na kuchelewa kurejea baada ya kwenda kuichezea timu yake ya taifa, Uganda dhidi ya Misri mechi ya kufuzu Kombe la Dunia mwakani Urusi.


Okwi alifunga bao hilo kwa shuti la umbali wa mita 25 baada ya kumchungulia kipa wa Mwadui, Arnold Massawe aliyekuwa amesogea mbele kidogo kufuatia pasi ya winga Shiza Kichuya aliyekuwa anacheza kama kiungo zaidi leo.


Mwadui pamoja na kumiliki vizuri mpira walipopata nafasi, lakini hawakuwa na mipango kabisa ya kuipenya ngome imara ya Simba chini ya mabeki wa timu za taifa za Uganda na Tanzania, Juuko Murshid na Salim Mbonde.


Kipindi cha pili nyota ya Simba iliendelea kung’ara na dakika ya 67, Okwi tena akawainua vitini mashabiki wa Wekundu wa Msimbazi kwa kufunga la pili kwa shuti la umbali wa mita zisizopungua 20 baada ya pasi ya beki Mohammed Hussein ‘Tshabalala’.


Mashabiki wa Simba walizomea mabadiliko yaliyofanywa na kocha Mcamroon, Joseph Marius Omog mara mbili kwanza akimtoa Mghana Nicholaus Gyan na kumuingiza Mwinyi Kazimoto dakika ya 61 na baadaye akimtoa Kichuya na kumuingiza Mrundi, Laudit Mavugo dakika ya 65 wakionekana kabisa kutaka mshambuliaji John Bocco ndiye atolewe.


Bocco akawaonyesha mashabiki wa Simba kwamba Omog alikuwa sahihi katika mabadiliko yake kwa kufunga bao la tatu dakika ya 72 kwa shuti la umbali wa mita 20 na zaidi pia.

Bonyeza HAPA kudownload applicationi ya Bongojamii Blog kwenye simu yako ili kupata habari zetu Haraka

Featured Posts