POLISI WAMKAMATA MBUNGE MSUKUMA GEITA | BONGOJAMII

POLISI WAMKAMATA MBUNGE MSUKUMA GEITA

Bonyeza HAPA kudownload applicationi ya Bongojamii Blog kwenye simu yako ili kupata habari zetu Haraka
BONYEZA HAPA KU-DOWNLOAD

Polisi mkoani Geita wanamshikilia Mbunge wa jimbo la Geita vijijini Joseph Kasheku (Musukuma) kutokana na vurugu zilizotokea eneo la mgodi wa GGM Septemba 14 mwaka huu.


Mbunge Msukuma na madiwani wa wilaya ya Geita walifunga barabara zinazoingia kwenye mgodi wa GGM wakishinikiza kulipwa dola 12 milion zinazotokana na kodi ya huduma.


Kamanda wa polisi mkoani hapa Mponjoli Mwabulambo jana alithibitishwa kukamatwa kwa Msukuma na kusema askari walimkamata katika eneo la CCM mjini Geita.


Kamanda amesema kukamatwa kwa Musukuma ni mwendelezo wa Polisi kuwakamata watu wote waliohusika katika vurugu zilizotokea Septemba 14.


Amesema tayari wamekamata madiwani wengine wawili na wananchi watano na kwamba jeshi hilo bado linaendelea na uchunguzi na msako wa kuwakamata wote walioshiriki.


“Bado tunaendelea na msako na hawa ni wahalifu kama wahalifu wengine na sheria lazima ichukue mkondo wake na Musukuma tumemkamata sio kwamba amekuja mwenyewe ”amesema


Kamanda amesema kwa sasa wanaendelea na mahojiano na wakikamilisha sheria itachukua mkondo wake na kwamba kosa la jina halina kikomo na wote walioshiriki vurugu za kufunga barabara lazima wakamatwe na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria .


Hadi sasa jeshi la polisi mkoani Geita linawashikilia madiwani kumi wa halmashauri za wilaya ya Geita waliofunga barabara zinazoingia mgodi wa GGM na kuharibu miundo mbinu ya maji yaliyotengenezwa na GGM kwa ajili ya shughuli za mgodi na wananchi wa mji wa Geita katika kijiji cha Nungwe jambo ambalo ni kinyume na sheria.


Mgogoro wa madiwani na GGM
Madiwani wa halmashauri mbili za wilaya ya Geita juzi walifunga barabara za kuingia katika mgodi wa dhahabu wa GGM wakishinikiza kulipwa dola 12milion zinazotokana na ushuru wa huduma kuanzia mwaka 2004 hadi 2013.


Madiwani hao wanadai fedha hizo ni haki yao kwa mujibu wa sheria kwasababu mgodi ulipaswa kulipa ushuru wa huduma wa 0.03 toka mwaka 2004 hadi 2013 na hawakulipa na badala yake walilipa dola 200,000 kwa kipindi chote kinyume na sheria.


Msimamo huo wa madiwani unapingwa na uongozi wa mgodi wanaodai kuwa mgogoro uliopo unasababishwa na kupingana kwa sheria ambazo zote zimetungwa na bunge.


Meneja mawasiliano ya jamii Manase Ndoroma amesema sheria ya madini iliwaruhusu kulipa dola 200,000 kwa mwaka huku sheria ya baraza la madiwani ikiwa imepitisha malipo ya 0.3 jambo ambalo limesababisha mgogoro na kwamba suluhisho pekee ni kwenda mahakamani.


Tayari serikali mkoani hapa imewataka madiwani hao kuwa watulivu na kumsubiri Naibu Waziri wa Wizara ya Nishati na Madini, pamoja na kamishna wa madini kufika mkoani hapa leo Jumatatu kwa lengo la kutafuta ufumbuzi wa mgogoro huo.

Bonyeza HAPA kudownload applicationi ya Bongojamii Blog kwenye simu yako ili kupata habari zetu Haraka

Featured Posts