HAYA SASA, MAASKOFU WATOA WARAKA MZITO | BONGOJAMII

HAYA SASA, MAASKOFU WATOA WARAKA MZITO

Bonyeza HAPA kudownload applicationi ya Bongojamii Blog kwenye simu yako ili kupata habari zetu Haraka
BONYEZA HAPA KU-DOWNLOAD

Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT) imetoa waraka uliojumuisha mambo mbalimbali, ikiwa ni pamoja na kuwataka viongozi kutenda haki, kutokuwa na upendeleo, kuheshimu Katiba na sheria za nchi.


Pia jumuiya hiyo imewataka Watanzania kwa ujumla kuliombea taifa na viongozi wake, ili wawe walinzi wa Katiba na sheria za nchi kama walivyoapa.


Waraka huo ulisambazwa jana katika vyombo vya habari, ukiwa umetiwa saini na Askofu Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dk. Fredrick Shoo na Askofu Mkuu wa Kanisa la Anglikana Tanzania (KAT), Dk. Jacob Chimeledya.


Wengine ni Askofu Mkuu wa Kanisa la Moravian Tanzania (KMT), Dk. Isaac Nicodemo na Askofu Mkuu wa Kanisa la African Inland Church in Tanzania (AICT), Silas Kezakubi.


“CCT inatoa maelekezo kwa Wakristo wa makanisa wanachama na Watanzania wote kwa ujumla, kuendelea kulinda na kuheshimu misingi ya haki za binadamu na kuliombea taifa na viongozi wake ili waendelee kuwa na hofu ya Mungu na waadilifu.


“Watende haki, wasiwe na upendeleo na waheshimu na kuwa walinzi wa Katiba na sheria za nchi kama walivyoapa,” ilisema sehemu ya waraka huo.


CCT ilieleza pia kusikitishwa na vitendo vya ujambazi na matumizi ya silaha katika jamii na kukemea matukio ya ukatili na yale ya watu kupotea katika mazingira ya kutatanisha.


“CCT inasikitishwa na vitendo vya ujambazi na matumizi ya silaha katika jamii yaliyofikia kiwango cha kuua askari polisi."


Aidha, CCT inakemea matukio ya ukatili unaondelea katika jamii.


“Yapo matukio ambayo yamedhihirisha ushirikiano hafifu kati ya polisi na wananchi na kuendelea kujitokeza kwa matukio yanayoashiria chuki za kidini na kikabila.


“CCT inatoa wito kwa Serikali kuhakikisha misingi ya umoja na mshikamano wa kitaifa inaheshimika na utawala wa kisheria unafuatwa,” ilisema taarifa hiyo.

Dawa za Kulevya

CCT ilisema ili vita dhidi ya dawa za kulevya ifanikiwe, ni muhimu Serikali ikalenga kutokomeza kiini cha tatizo kwa kuwapata wahusika wakuu wa biashara hiyo bila kujali wasifu wao na nafasi walizonazo katika jamii.


Kutokana na hilo, CCT ilisisitiza kuwa Serikali izingatie misingi ya sheria, haki na usawa katika kuwakamata, kuwapekua na kuwafikisha katika vyombo vya sheria bila kuonea mtu wala kusukumwa na misingi yoyote ya imani au itikadi ya mtu.


“CCT inaunga mkono vita dhidi ya matumizi ya dawa za kulevya na viroba iliyoanzishwa na Serikali. Hata hivyo, CCT inasisitiza kuwa ili vita hii ifanikiwe, ni muhimu sana Serikali ilenge kutokomeza kiini cha tatizo kwa kuwapata wahusika wakuu wa biashara hii bila kujali wasifu wao, nafasi zao wala nafasi walizo nazo katika jamii.


“Katika kufanya hivyo, ni muhimu Serikali izingatie misingi ya sheria, haki na usawa katika kuwakamata, kuwapekua na kuwafikisha katika vyombo vya sheria bila kuonea wala kusukumwa na misingi yoyote ya imani au itikadi ya mtu.


“Ni muhimu kwa Serikali kuendelea kuweka mazingira wezeshi kwa vijana kupata ajira na kuendesha shughuli za ujasiriamali ili kujiepusha na vitendo viovu vikiwemo matumizi ya dawa za kulevya na unywaji wa pombe kali.


“CCT inayaelekeza makanisa wanachama, wazazi na walezi kuendelea kuwalea vijana wao katika misingi ya kidini ili wasijiingize katika matumizi ya dawa za kulevya na pombe kali.


“Wakati huu wa Kwaresma, tunawaombea na kuwaomba wale wote ambao kwa njia moja au nyingine wanajihusisha na dawa za kulevya au unywaji wa pombe kali, watubu na kuyaacha maovu yao na Mungu atawarehemu,” walisema maaskofu hao.


Hali ya Chakula
Kuhusu hali ya chakula nchini, CCT ilisema kuwa pamoja na mvua kuanza kunyesha, Serikali na wengine wawezeshe usambazaji wa chakula kutoka mikoa yenye ziada kwenda mikoa yenye uhaba wa chakula ili bei ya chakula iweze kushuka.


“Tunaiomba Serikali kupitia idara yake inayohusika, iratibu na kusaidia utekelezaji wa jambo hili, ili wananchi waweze kumudu bei, mfano mahindi hayo yakisambazwa, bei ishuke kutoka zaidi ya Sh 100,000 ifikie angalau Sh 60,000.


“Pia tunawaomba wakulima wasitumie njaa hii kutekeleza usemi ya kwamba ‘kufa kufaana’, hivyo kwao kipindi hiki kigumu kwa Watanzania wengine wakakifanya kipindi cha kupandisha bei ili kupata faida kubwa.


“Sambamba na wito huu, tunawaekeleza wanachama wetu kupitia vitengo vya maafa na misaada ya kibinadamu, waendelee kuwasaidia wananchi wenye upungufu mkubwa wa chakula wakipate kwa bei nafuu kwenye maeneo yao,” ilisema.


CCT iliwataka Wakristo wote kuendelea kumwomba Mungu ili mvua zinazoendelea kunyesha ziwe za neema na zisilete madhara.


Katika hilo, wameiomba serikali kutoa unafuu wa bei ya gesi ya kupikia ili wananchi wengi wapunguze au kuachana kabisa na matumizi ya kuni na mkaa.


Elimu
CCT ilisema pamoja na nia njema ya Serikali kutoa elimu bure, lakini iangalie masilahi ya walimu na kuwe na mpango mkakati unaotekelezeka wa kuimarisha miundombinu ya kufundishia.


“Serikali haina budi kuendelea kutoa elimu ya kutosha kwa wananchi kuhusu dhana ya elimu bila malipo, ili kuepusha migogoro inayokabili sekta ya elimu kwa dhana hiyo kutoeleweka kwa vizuri kwa baadhi ya wananchi.


“Pia mabadiliko ya mitaala na miongozo mingine ya kufundishia ya mara kwa mara imekuwa ikiathiri elimu ya Tanzania kwa kila awamu ya uongozi na kuwafanya wahitimu wetu kukosa ushindani kikanda na kimataifa,” ulisema waraka huo.


Kupitia waraka huo, maaskofu waliishauri Serikali kuwa na serĂ¡ ya elimu isiyobadilika badilika kila uongozi mpya unapoingia madarakani.

Bonyeza HAPA kudownload applicationi ya Bongojamii Blog kwenye simu yako ili kupata habari zetu Haraka

Featured Posts