RAIS MAGUFULI: MTANIKUMBUKA | BONGOJAMII

RAIS MAGUFULI: MTANIKUMBUKA

Bonyeza HAPA kudownload applicationi ya Bongojamii Blog kwenye simu yako ili kupata habari zetu Haraka
BONYEZA HAPA KU-DOWNLOAD
RAIS Dk. John Magufuli amesema Watanzania watamkumbuka pamoja na awamu ya tano ya uongozi wake, ambayo imejielekeza kufanya kazi kwa bidii.

Kauli hiyo ya Dk. Magufuli imekuja mapema katika kipindi cha miaka miwili ya awamu ya kwanza ya utawala wake, tofauti na watangulizi wake, marais wastaafu Benjamin Mkapa na Jakaya Kikwete ambao waliitoa katika kipindi cha mwisho cha uongozi wao.

Februari 30, 2015, Rais wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete, alitoa kauli inayofanana na ya Dk. Magufuli, wakati akizungumza katika Ofisi Ndogo za Makao Makuu ya CCM Lumumba, Dar es Salaam.

Kikwete alisema yeye anaondoka, lakini Dk. Magufuli ataendeleza kwa kasi kuanzia pale alipoishia.

“Naondoka mie tumeleta chuma hiki, pale nilipochoka mie yeye sasa anakwenda kwa kasi, anazo nguvu za kutosha kuliko mie.

“Na mlikuwa mnasema mie mpolepole, hivi sasa mabadiliko kuleta mkali… na ameanza kutema cheche,” alisema.

Jana wakati akizindua ujenzi wa reli mpya ya kisasa ya Standard Gauge (SGR), ambayo itatumiwa na treni ya umeme Pugu, Dar es Salaam, Dk. Magufuli alisema Watanzania wataikumbuka Awamu ya Tano ambayo ni ya kazi.

Alisema wakati wa kuomba kura, aliahidi mambo mengi ikiwamo kuimarisha miundombinu ikiwa ni pamoja na reli ya kisasa ambayo ilitakiwa ijengwe mwaka 1961.

“Uchumi unakua na ushahidi ni miundombinu tunayojenga, tumebana fedha za mafisadi, tumebana fedha za wapigadili, tumenunua ndege mpya sita, zitakuza utalii, biashara na kulifikisha lori letu linakotaka kwenda.

“Nawaambia siku moja mtaikumbuka awamu ya tano ya kazi, lakini nafahamu katika usafiri wowote unapopakia abiria uhitaji kuwauliza watasimama kuangalia sehemu gani wakati lori linaondoka.

“Wako watakaotazama nyuma, ubavuni, kule lori linakoelekea, kama ukipakia wasukuma wanaweza kuimba kwenye lori.

“Dereva mzuri hutakiwi kusikiliza nyimbo, kuangalia watu walikotazama, angalia unakolipeleka lori ili lifike salama. Kwa hiyo nawahakikishia mimi najiamini ni dereva mzuri na kwenye lori langu limepakia watu wa aina hiyo, wako wanaoimba, wanaopiga stori, wanaotazama nyuma wakati lori linakwenda mbele, walioangalia mbele, ubavuni, lakini lori litafika kule linakokwenda na hili ni lori la maendeleo.

“Na katika kazi tunazofanya, wanaopiga kelele ni wale waliozoea kupiga dili, waendelee, lakini lori litakwenda hadi linakotaka,” alisema Dk. Magufuli.

Alisema kuwa wapo watu wanacheza michezo michafu kwa lengo la kuvuruga amani nchini na aliwatahadharisha kwamba anajua anakokwenda, hivyo pasitokee mtu wa kubadilisha ajenda halafu waanze kuzungumzia ajenda ambazo haziko katika ilani ya uchaguzi.

“Katika nchi nyingi walizojaribu kupiga hatua, walichonganishwa na kugombana wenyewe kwa wenyewe, nawaomba tutangulize Tanzania kwanza siasa baadaye, Watanzania wanataka maendeleo, hakuna Mtanzania anayekula siasa… iacheni Serikali ya CCM itekeleze wajibu wake tutakutana 2020, sasa ni kazi tu,” alisema.



VITA YA UFISADI

Akizungumzia vita ya kupambana na ufisadi, Dk. Magufuli, alisema ni ngumu na ina mlolongo mwingi, hasa unapowabadilisha watu waliozoea maisha fulani kwa miaka 50.

“Samaki mkunje angali mbichi, akishakomaa mvunje tu. Na fisadi mkunje angali mbichi, akishakomaa mvunje na wakati wa kumvunja ni lazima atalalamika.

“Ni nafuu walalamike wachache, lakini wafaidike wengi. Ninapozungumzia mchanga, ningeweza kusema watangulize makontena yangu mawili Ulaya, lakini kutoka moyoni nafanya kazi kwa niaba yenu.

“Mlinituma nifanye, haya yote ninayofanya kweli ni mabaya? (wananchi wakaitikia mazuri).”

Akauliza tena: “Wangapi wanasema mazuri (wananchi wakanyoosha mikono), … kwahiyo niendelee? (wananchi wakaitikia)

“Tulionewa sana, tumechezewa sana, tumedharauliwa mno, Tanzania ni tajiri, hatutakiwi kuwa ombaomba. Tuna ubaya gani kwa Mungu, dhahabu zipo, wanyama wapo, lakini sisi ni masikini, ni lazima tujitambue,” alisema.

Kuhusu ujenzi wa reli hiyo, alisema yako mambo mengi aliyoahidi wakati alipokuwa akiomba kura kama kuimarisha miundombinu, ikiwamo ujenzi wa reli hiyo ya kisasa.

Alisema Watanzania wanapaswa kujivunia kujenga reli hiyo kwa fedha zao kwani sehemu kubwa ya reli ya kati ilijengwa na wakoloni (Wajerumani na Waingereza) kwa miaka 30 na reli ya Tazara iliyojengwa miaka ya 1970 ambayo ilijengwa kwa ufadhili wa China.



UJENZI WA RELI

Dk. Magufuli alisema awamu ya kwanza ya ujenzi wa reli hiyo itakuwa ni ya kilomita 300 ya kutoka Dar es Salaam – Morogoro na itagharimu Sh trilioni 2.7 na kwamba tayari mkandarasi amelipwa malipo ya awali wiki iliyopita Sh bilioni 300.

“Reli hii itarahisisha usafiri wa mizigo na abiria, itakuza biashara kati ya Tanzania na nchi nyingine, itakuza sekta zingine, itakuza utalii, itarahisisha usafirishaji wa malighafi na kutunza barabara. Barabara zetu nyingi zimekuwa zikiharibika ndani ya muda mfupi kutokana na kusafirisha mizigo mizito,” alisema Dk. Magufuli.

Kwa mujibu wa Dk. Magufuli, reli hiyo itaongeza fursa za ajira nchini ambapo watu 600,000 wanatarajiwa kuajiriwa zikiwamo ajira 30,000 za moja kwa moja.

Pia alisema Benki ya Dunia (WB) imetoa Sh bilioni 300 kukarabati reli ya zamani na Rais wa Uturuki amekubali kutoa mkopo wenye masharti nafuu kwa ujenzi wa awamu ya pili ya Morogoro hadi Dodoma.

Dk. Magufuli pia ameziagiza mamlaka husika kuhakikisha wananchi wa Pugu wanapewa kipaumbele katika fursa za ajira zitakazopatikana kwenye ujenzi huo.

Naye Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa, alisema reli hiyo itakuwa na uwezo wa kusafirisha tani milioni 17 za mizigo kwa mwaka, tofauti na reli iliyopo sasa ambayo ina uwezo wa kusafirisha tani milioni tano.

Alisema baada ya ujenzi kukamilika, mtu ataweza kusafiri kati ya Dar es Salaam na Morogoro kwa saa 1:15, Dar es Salaam na Dodoma saa 2:50 na Dar es Salaam na Mwanza saa 7:40.

“Tutamsimamia mkandarasi afanye kazi kwa uaminifu na kuhakikisha anajenga reli ya kisasa kwa viwango vya kimataifa,” alisema Profesa Mbarawa.



WAKANDARASI 40 WAOMBA KAZI

Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni Hodhi ya Rasilimali za Reli nchini (Rahco), Masanja Kadogosa, alisema wakandarasi 40 waliomba kazi ya kujenga reli hiyo na kwamba kampuni za Yapi Merkezi ya Uturuki na Mota-Engil ya Ureno ndizo zilikidhi vigezo.

Reli hiyo itakayokuwa na urefu wa kilomita 1,219 itajengwa kwa awamu tano na kwamba awamu ya kwanza ya kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro yenye urefu wa kilomita 300 itagharimu Sh trilioni 2.7 na itajengwa kwa miezi 30.

Alisema kati ya kilomita hizo, 205 zitakuwa za njia kuu na 95 za reli ya michepuo ya treni kupishana na kupanga mabehewa.

Pia alisema kutakuwapo na vituo sita vya abiria na vituo vidogo sita vya kupishana treni.

“Reli hii itakuwa na urefu wa kilomita mbili, yenye mabehewa 100 yenye uwezo wa kusafirisha tani 10,000 kwa mara moja sawa na malori 500 yenye uzito wa tani 20 kila moja.

“Kutakuwa na mifumo ya mawasiliano ambapo dereva akiendesha kwa mwendo kasi atapewa onyo, akikaidi mwendo utapunguzwa kwa lazima ama treni itasimamishwa,” alisema Kadogosa.

Alisema zabuni za awamu nyingine nne za ujenzi wa reli hiyo zinatarajiwa kufunguliwa Aprili 19.

Awamu hizo ni za ujenzi kati ya Morogoro na Makutopora, Makutopora na Tabora, Tabora na Isaka na Isaka na Mwanza.

Kwa mujibu wa mkurugenzi huyo, awamu ya kwanza ya ujenzi pia itahusisha kutolewa mafunzo maalumu kwa Watanzania 300 kwa lengo la kuwapa ujuzi katika ujenzi, ukarabati na uendeshaji wa reli na treni zitakazotumika.

Naye Mwakilishi wa Kampuni ya Yapi Merkezi, Emre Aykar, alimuhakikishia Dk. Magufuli kuwa ujenzi huo utakamilika katika muda uliopangwa.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Bajeti, Hawa Ghasia, alisema bajeti ya miundombinu ya 2017/18 itapita bila matatizo na kwamba kwenye kamati ilishapita.

Bonyeza HAPA kudownload applicationi ya Bongojamii Blog kwenye simu yako ili kupata habari zetu Haraka

Featured Posts