SERIKALI HAIFAHAMU ALIPO BEN SAANANE | BONGOJAMII

SERIKALI HAIFAHAMU ALIPO BEN SAANANE

Bonyeza HAPA kudownload applicationi ya Bongojamii Blog kwenye simu yako ili kupata habari zetu Haraka
BONYEZA HAPA KU-DOWNLOAD
MWANASHERIA Mkuu wa Serikali, George Masaju, amesema taarifa kwamba kada wa Chama cha Demokrasia (Chadema), Ben Saanane ametekwa hazina ukweli kwa sababu hakuna ushahidi wowote.

Kauli hiyo aliitoa jana bungeni wakati wa kuhitimisha hotuba ya bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu.

Alisema ili kuthibitisha kuwa mtu amekufa kwa mujibu wa sheria ya ushahidi lazima iwe imepita miaka mitano.

“Hatuna taarifa za Ben na haijulikani kama ametekwa au amejificha au yupo wapi. Huwezi kusema Ben Saanane ametekwa wakati huna ushahidi, inawezekana watu wasiokuwa na nia njema na Serikali hii wanafanya uhalifu kwa sababu huwezi kusema kwamba Ben Saanane amekufa.

“If you have serious information juu ya mambo ya uhalifu, pelekeni kwenye vyombo vya dola… hatuwezi kufanya hivi, sheria yetu ya ushahidi inasema ili kuthibitisha kuwa mtu amekufa miaka mitano iwe imepita, kifungu cha 100 cha sheria ya ushahidi kinaeleza hilo,” alisema Masaju.


MWIGULU

Wakati wa kupitisha bajeti ya Waziri Mkuu, kifungu kwa kifungu, baada ya Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe kutaka suala la usalama na watu kutekwa lijadiliwe, Waziri wa Mambo ya Ndani, Mwigulu Nchemba, alisema maneno yanayosemwa kwamba kuna kikosi maalumu cha kutesa watu ni jambo la uongo.

Alisema hayo ni mambo yanayotokea sasa kwa sababu Serikali imetangaza mapinduzi ya maendeleo.

Mwigulu alisema pia kuwa suala la kuwapo kwa orodha ya wabunge ambao wanataka kutekwa si jambo la kweli.

“Hiyo orodha haina ukweli kwa sababu kama hicho kikosi kina polisi na polisi wako chini yangu, alafu na kwenye orodha na jina langu likawepo, nadhani ni yaleyale watu wanaandika orodha zao kwenye mitandao.

“Hakuna kitu kama hicho na orodha hiyo siyo kweli, kama orodha hiyo ingekuwa sahihi, nadhani kwa mazingira kama haya sidhani kama ingekuwa inatoka kama inavyotoka, kwa mazingira hata ya kijijini tu, mtu anayekuloga hawezi kukwambia, na kwanini ateke hao wanaotajwa, wana kipi kikubwa?

“Lakini suala kubwa hapa ni suala la usalama wetu, na kwenye suala la usalama hakuna haja ya kutofautiana, inatakiwa kushauriana namna ya kukabiliana nayo.

“Tutakuwa wa ajabu sana tukianza kubishana suala la usalama wa nchi yetu. Hakuna Serikali duniani iliyoweka rehani usalama wa raia wao, mara kwa mara wakati mwingine tunakuwa kwenye mazingira yenye utata, kusingekuwa na usalama sijui ingekuwaje.

“Tusichukue kesi moja moja, kesi moja moja duniani kote zipo za maisha ya watu kuwa hatarini na siyo za Serikali, ni za watu waovu na sisi kazi yetu ni kupambama na watu waovu ili watu wetu waishi salama.

“Duniani kote Serikali inavyotangaza mapinduzi ya kiuchumi, kunakuwepo na vita ya kiuchumi, vinapokuwepo vitu vya namna hiyo, kunakuwepo na vitu vingi vinatokea na nadhani hivyo ndivyo vinatokea kwenye mazingira haya,” alisema Mwigulu.

Kwa upande wake Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Utumishi wa Umma, Angela Kairuki alisema: “Kwanza kabisa niseme chombo hiki (Idara ya Usalama wa Taifa) ni chombo muhimu, ni chombo ambacho kipo kisheria, ni chombo ambacho kimeanzishwa kwa majukumu maalumu, hivyo basi ni vyema tukaweza kukilinda, kukithamini na kukiheshimu.

“Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa, mtu anaposema kwamba kina kikosi cha kutesa watu, siyo kweli, ni maneno ya ufitinishi, ni maneno ya uchochezi, na sote tunafahamu nchi hii kuna kosa pia la uchochezi,” alisema Kairuki.

Alisema kwa mujibu wa sheria, Idara ya Usalama wa Taifa ina majukumu yake na kwamba inaruhisiwa kushirikiana na vyombo vingine vya dola.

“Majukumu yake yapo wazi, ni kwa sababu wao (wapinzani) wameamua kuwa kwenye masuala wanayoyataka, wameamua kuchagua mambo machache kuepuka tafsiri yenyewe ya sheria.

“Unaposema kukamata, uthibitisho huna, hata kidogo kwa sababu hakuna kitu kama hicho. Ni fikra mliyojijengea kwa sababu mnataka kuwaaminisha watu kwamba kuna kitu kama hicho, ni lazima kwenye masuala kama haya tufike mwisho, tusitake kujenga kukubalika kwa kufitinisha watu,” alisema Kairuki.



MAJALIWA NA UCHUNGUZI

Awali akihitimisha mjadala wa bajeti yake, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, alisema Serikali inalifanyia kazi suala la vitendo vya utekaji watu na kwamba itatoa taarifa baada ya kufanyika uchunguzi juu ya matukio hayo.

Kauli hiyo aliitoa jana bungeni wakati akihitimisha majumuisho ya hotuba ya bajeti ya makadirio ya mapato na matumizi ya ofisi yake kwa mwaka 2017/18.

“Wabunge wamezungumzia suala la usalama. Ninaomba niwahakikishieni kwamba Serikali inalifanyia kazi na baadaye tutatoa taarifa kwenu… tuache vyombo vyetu vifanye kazi ya uchunguzi, kwamba ni nani anayefanya haya na je, matukio haya yanakubalika? Tunajua ni matukio yasiyokubalika,” alisema Majaliwa.

Baada ya Waziri Mkuu kumaliza hotuba ya majumuisho hayo, Mbowe alieleza kutoridhishwa na maelezo hayo akimtaka atoe tamko juu ya matukio hayo yanayoendelea.

“Ni bahati mbaya tunafanya jambo hili kuwa jepesi kwa sababu ninyi hamjaguswa au familia zenu hazijaguswa. Mngesema tulete ushahidi tungeleta kuhusu walioteswa. Hatuna tatizo na idara hii, lakini inapogeuka vibaya au baadhi ya watu wanapogeuka kutesa watu, haikubaliki.

“Bado sijaridhika na jambo hili. Watu wanatesa raia ambao hawana makosa, tuko tayari kutoa ushahidi. Lissu (Mnadhimu wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Tundu Lissu) kasema hapa anatetea vijana 18 ambao waliteswa na wako tayari kutoa ushahidi, lakini ninyi mnasema hamjui jambo hili liko very serious. Clouds imevamiwa na askari, Nape ambaye alikuwa waziri alitolewa bastola mchana kweupe, lakini hakuna kauli ya Serikali.

“Tunataka nchi yetu irudishiwe amani kama tulivyozoea, wengine wanauawa kisirisiri ndio maana tunataka Serikali itupe kauli juu ya jambo hili,” alisema Mbowe.

Kwa upande wake, Lissu, alisema Watanzania wametekwa, wameteswa na kudhalilishwa, lakini Serikali imekuwa kimya.

“Watanzania wametekwa, wameteswa wamedhalilishwa wala si vitu vya kufikirika, Lema aliondolewaje hapa bungeni hadi akapelekwa Arusha na kukaa gerezani kwa miezi minne, mimi nilitolewaje hapa na kupelekwa Dar es Salaam.

“Halafu mnadiriki kutetea ujinga huu? Nilishesema hapa bungeni na narudia kwamba mnashughulikia wapinzani, kumbukeni Nape, Bashe, Msukuma kesho ni wewe,” alisema Lissu.

Bonyeza HAPA kudownload applicationi ya Bongojamii Blog kwenye simu yako ili kupata habari zetu Haraka

Featured Posts