TAKUKURU , DCI KUWATAFUTA POPOTE WALIPO VIGOGO WA MCHANGA WA MADINI | BONGOJAMII

TAKUKURU , DCI KUWATAFUTA POPOTE WALIPO VIGOGO WA MCHANGA WA MADINI

Bonyeza HAPA kudownload applicationi ya Bongojamii Blog kwenye simu yako ili kupata habari zetu Haraka
BONYEZA HAPA KU-DOWNLOAD
Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Kamishna Robert Boaz, na Mkurugenzi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambanba na Rushwa (Takukuru), Valentino Mlowola, wawameanza kazi ya kuwachunguza vigogo na Mafisadi mara moja, kama waliyoagizwa na Rais John Magufuli.

Jumatano, Rais John Magufuli alikabidhiwa ripoti ya kamati teule aliyounda kufuatilia kila kilichomo ndani ya makontena 277 ya mchanga wa dhahabu yaliyokuwa katika Bandari ya Dar es Salaam kwa ajili ya kusafirishwa kwenda ughaibuni.

Akiwasilisha ripoti hiyo kwa Rais, Ikulu jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa kamati hiyo ya wataalamu wanane, Prof. Abdulkarim Mruma, alisema kuwa kwa
ujumla, thamani ya madini yote katika makinikia kwenye makontena 277 yaliyozuiliwa bandarini jijini Dar es Salaam ni Sh. bilioni 829.4 kwa kutumia viwango vya wastani na Sh. trilioni 1.44 kwa kutumia viwango vya juu.

Kwa mujibu wa kamati, kiasi hicho cha fedha ni jumla ya thamani ya madini ya dhahabu, shaba na madini mengine ya metali mkakati (strategic metals) yakiwamo ya Sulfur, chuma, Iridium, Rhodium, Ytterbium, Beryllium, Tantalum na Lithium,

Kutokana na ripoti hiyo, ndipo Rais Magufuli alipotengua uteuzi wa Waziri wa Nishati na Madini, Prof. Sospeter Muhongo na kuviagiza vyombo vya ulinzi na usalama

viwachunguze na ikiwezekana viwachukulie hatua watumishi waliokuwa wakihusika kubariki usafirishaji wa mchanga huo wa dhahabu, kuanzia Kamishna wa Madini aliyepita, watumishi wa Wakala wa Ukaguzi wa Madini (TMAA) na kila mmoja.

Uchunguzi wa Nipashe umebaini kuwa katika kutekeleza agizo hilo la Rais, tayari Takukuru, DCI na vyombo vingine vya kiuchunguzi vimeshaanza kazi ya kuwanasa walengwa na kuwahoji mmoja baada ya mwingine.

Matokeo yake, kwa mujibu wa vyanzo vya Nipashe, ni kwamba maofisa mbalimbali wanaochunguzwa wamejikuta wakiwa katika hali ya taharuki, hasa kutokana na kutambua kwao kuwa matokeo ya uchunguzi huo yanaweza kuwakosesha kazi, kuwapeleka jela na pia baadhi yao kupoteza utiriri wa mali wanazomiliki.

“Kwakweli mambo ni magumu… kuna maofisa hivi sasa wanahangaika huku na huko kwa nia ya kulinda mali zao zisifikiwe na mkono wa dola na kupoteza utajiri walio nao,” chanzo kimojawapo kiliiambia Nipashe jana kwa sharti la kutoandikwa jina gazetini.

Chanzo kingine kilidai kuwa wapo baadhi ya maofisa waliojikuta wakipandwa presha kwa hofu, hasa kutokana na mali walizojilimbikizia kupitia ‘dili’ hizo za usafirishaji wa mchanga wa dhahabu.

Mali zinazodaiwa kumilikiwa na baadhi ya watu wanaotarajiwa kuchunguzwa zinatajwa kuwa ni pamoja na utitiri wa viwanja wanavyomiliki katika maeneo ghali yakiwamo ya ufukweni, nyumba za kifahari, nyumba za kulala wageni, baa, hoteli, maduka, magari ya kisasa na miradi mingine ya mitaji ya mamilioni isiyolingana na mishahara na marupurupu yao mengine kwa mwezi.

“Hofu imezidi kwa baadhi ya watu hawa kwa sababu zipo taarifa kuwa Takukuru na vyombo vingine vya uchunguzi vimeshitukia jitihada zinazofanywa za kuuza na pia kubadili umiliki wa mali ili zisiwaponze kwa kutumika kama vielelezo vya kuwatia hatiani,” chanzo kilidai na kuongeza:

“Kwa ufupi hali ni mbaya kwa baadhi ya wahusika wa dili hizi. Hii ni kwa sababu hakuna aliyetarajia kuwa ipo siku kutakuwa na uchunguzi kama huu. Wapo waliamini kuwa kila kilichokuwa kikifanyika kilikuwa sahihi na hivyo hawakuwa na tahadhari ya kutosha kuficha mali zao.”

DCI, TAKUKURU WAKIRI KUANZA KAZI
Wakati akizungumza na Nipashe juzi kuhusiana na taarifa kuwa baadhi ya wahusika katika usafirishaji wa mchanga wa dhahabu wameanza kunaswa, Mkurugenzi wa Takukuru, Mlowola, alikiri kwamba ni kweli wameshaanza uchunguzi wao, ikiwa ni utekelezaji bila kuchelewa wa maagizo ya Rais Magufuli.

Akifafanua, Mlowola alisema tayari vijana wake wako kazini tangu siku (Jumatano) Rais Magufuli alipotoa maagizo hayo Ikulu.

“ Rais anapoagiza kinachofuata ni utekelezaji, ila kwa sasa hatuwezi kuweka wazi kila kitu kinachofanyika maana tutaharibu uchunguzi. Ila ninachoweza kukwambia ni kwamba tayari tumeshaingia kazini kama tulivyoagizwa na Mheshimiwa Rais,” alisema Mlowola.

Aidha, DCI Boaz, alikiri pia kwamba ofisi yake imeshaanza kazi ya uchunguzi, lakini akikataa kuweka wazi juu ya majina na idadi ya watu ambao hadi sasa wameshawanasa.

“Sisi tumeshaanza kazi,” alisema alisema Kamishna Boaz kabla ya kuongeza:

“Tuko kazini, kazi inaendelea… kuhusu idadi ya watu na nani wamekamatwa ni masuala ya kiupelelezi, siwezi kuyaweka wazi kwa sasa. Ila jua kuwa kazi imeanza na inaendelea vizuri.”

Machi 29 mwaka huu, Rais Magufuli aliiteua Kamati Maalum ikiwa na wajumbe nane wenye taaluma za Jiolojia, Kemia, Uhandisi Kemikali na Uhandisi Uchenjuaji madini na Jumatano ndipo kamati hiyo iliwasilisha ripoti yake pamoja na mapendekezo kwa Rais.

Miongoni mwa maagizo aliyoyatoa Rais ni kuchunguzwa kwa watumishi wote waliohusika na mlolongo wote ambao wametajwa kwenye nyaraka za kusafirisha mchanga na hatua za kisheria zichukuliwe dhidi yao.

Bonyeza HAPA kudownload applicationi ya Bongojamii Blog kwenye simu yako ili kupata habari zetu Haraka

Featured Posts