MAZISHI YA NDESAMBURO NI YA KIHISTORIA | BONGOJAMII

MAZISHI YA NDESAMBURO NI YA KIHISTORIA

Bonyeza HAPA kudownload applicationi ya Bongojamii Blog kwenye simu yako ili kupata habari zetu Haraka
BONYEZA HAPA KU-DOWNLOAD
NI mazishi ya karne: Hivyo ndivyo unavyoweza kuelezea hali ilivyokuwa jana kwenye shughuli ya kuaga mwili wa aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Moshi Mjini kwa miaka 15, marehemu Phillemon Ndesamburo ambaye anazikwa leo.

Ndesamburo alifariki dunia Jumatano, majira ya saa 4:45 asubuhi kwa maradhi ya moyo, baada ya kufikishwa katika Hospitali ya Rufani ya KCMC akiwa amezimia.

Jeneza lenye mwili wa Ndesamburo liliwasili katika Uwanja wa Majengo majira ya saa 6:15 mchana lilikuwa limebebwa na gari jeusi aina ya Toyota Landcruiser V8 na kusindikizwa na pikipiki zaidi ya 600 na magari zaidi ya 1,000, yakitokea KCMC na kupitishwa barabara ya YMCA kuelekea Majengo.

Wakati mwili huo ukipelekwa Uwanja wa Majengo kwa ajili ya shughuli za kumbukizi za maisha ya kisiasa ya Ndesamburo, mamia ya wananchi walijipanga kando kando ya barabara wakitaka kuligusa kwa mkono gari lenye mwili wa Ndesamburo.

Wananchi hao walianza kufurika kando ya barabara kati ya saa 2:30 asubuhi na saa 3:50 asubuhi ili kushuhudia msafara huo ukipita, huku Polisi wakiwa wamejipanga kuimarisha ulinzi katika Barabara ya Majengo/Kiborloni.

Askari wengine walikuwa wameweka kambi uwanjani wakisubiri kuona shughuli za kuuaga mwili wa mwanasiasa huyo.

GWAJIMA ALIAMSHA
Katika kile kinachoonekana kuwa ni kuchukizwa na tabia ya kuingiza siasa misibani, Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima jana alijikuta akishangiliwa na maelfu ya waombolezaji baada ya kuhoji ni nani aliyezuia Ndesambauro asiagwe katika Uwanja wa Mashujaa kama ilivyokuwa imepangwa awali.

“Kama kiongozi wa kiroho, nataka nitoe matibabu ya dakika chache kwenye siasa za Moshi na za Arusha," alisema Askofu Gwajima ambaye anafahamika kwa kutoka nje ya neno kidogo pindi 'dude' linapoamshwa. "Usiniulize kwa nini natoa matibabu msibani. Nasikitishwa sana.

"Nilipata taarifa za msiba kwamba unafanyika viwanja vya Mashujaa, lakini kwa sababu zisizoeleweka nikasikia ama kiongozi mmoja anayeongozwa na kiongozi mwingine, lakini tetesi tetesi nasikia Mkuu wa Mkoa wa Arusha ametoa maelekezo haiwezekani kufanyia kwenye uwanja huo kwa sababu sauti ni kubwa kuna mahakama na shule.”

Askofu Gwajima alisema alipokuja Moshi alifanyia mkutano uwanja huo na vyombo vyake vilikuwa vikubwa kuliko vinavyotumika kwenye msiba huo.

“Unapoanza kuleta siasa msibani unaongezea msiba mwingine na mimi ninahakika mheshimiwa Rais (John Magufuli) hakumtuma hilo alilofanya," alisema Askofu Gwajima.

"Naona Mheshimiwa Rais hajamtuma, jambo hili liachwe mara moja nataka Rais anisikie kama hujamtuma mchukulie hatua ili jambo hili lisitokee tena.
"Jambo alilolifanya halitoi taswira nzuri kwa umoja wa nchi na usalama wa nchi, jambo hili halifai na likemewe na watu wote.”

Shughuli hizo za kuaga mwili wa Ndesamburo pamoja na kumbukizi za maisha ya mwasiasa huyo mkongwe, zimewakutanisha pamoja wanasiasa wengi wa vyama vya upinzani nchini, kwa mara ya kwanza tangu kumalizika kwa Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani wa Mwaka 2015 na tangu serikali ilipotangaza marufuku ya mikutano ya vyama vya siasa.

Viongozi wa vyama vya siasa waliohudhuria ni Mwenyekiti wa Taifa wa Chama cha NCCR-Mageuzi, James Mbatia, Mwenyekiti wa Chadema Taifa, Freeman Mbowe, mwakilishi wa Chama cha Wananchi (CUF), Chama cha SAU, Wabunge, Wajumbe wa Kamati Kuu za vyama hivyo, viongozi wa vyama wa mikoa na kanda pamoja na wananchama na makada kutoka mikoa mbalimbali nchini walionekana jana kwenye shughuli hiyo.

Jeshi la Polisi lilizuia utaratibu wa kutoa heshima za mwisho kwa kuupitisha mwili wa marehemu katika mitaa na viunga vya barabara za Manispaa ya Moshi.

Polisi ilisema ilizuia jeneza lenye mwili wa Ndesamburo kupitishwa mitaani kwa sababu jana ilikuwa siku ya kazi na kuwapo kwa shughuli mbalimbali zilizokuwa zikiendelea.

Pia Polisi ilidai kwamba upitishaji wa mwili huo kwenye mitaa ya Moshi kungesababisha msongamano mkubwa ambao ungekuwa chanzo cha usumbufu kwa watumiaji wengi wa barabara.

LOWASSA SHANGWE
Katika hali isiyo ya kawaida, maelfu ya waombolezaji waliokuwa wamefurika katika uwanja huo walianza kupiga miluzi na kushangilia kwa sauti, baada ya Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowasa kuingia uwanjani hapo akiwa nyuma ya gari lililobeba mwili wa marehemu Ndesamburo.

Baadaye shangwe zililipuka zaidi wakati Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema na Mbunge wa Iringa Mjini, Mch. Peter Msigwa walipoingia uwanjani hapo wakionyesha vidole viwili juu.

Akizungumza katika zoezi hilo la kuaga pamoja na kumbukizi za maisha ya marehemu Ndesamburo, Msaidizi wa Askofu wa Dayosisi ya Kaskazini ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Mch. Elingaya Saria alisema hakuna ubishi kwamba Ndesamburo alikuwa baraka katika Mji wa Moshi na mkoa wa Kilimanjaro.

“Kama kanisa tumeguswa sana na msiba huu wa marehemu Phillemon Ndesamburo Kihwelu ambaye kwa kweli alikuwa baraka kwa Moshi na mkoa wetu wa Kilimanjaro na Watanzania wote," alisema Mch. Saria.

"Alikuwa na utu, mtu wa watu na jasiri kutetea wanyonge na kupigania watu wote. Tumwombee apokelewe na Mwenyeni Mungu.”

Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania, Sheikh Rajab Katimba akizungumza katika shughuli hizo, aliwataka wanasiasa na viongozi wa umma wasiutumie msiba huo kama mtaji wa kisiasa.

“Sisi Waislamu tunamjua vizuri mzee huyu... hakuwa na makuu, alijali wenzake na alitumika kama vile ambavyo Mwenyezi Mungu anataka. Analisha yatima, amejenga misikiti na amesaidia wengi. Msiba huu mtu yeyote asichukue kama mtaji wa kisiasa, hatutamtendea haki,” alisema Sheikh Katimba.

Bonyeza HAPA kudownload applicationi ya Bongojamii Blog kwenye simu yako ili kupata habari zetu Haraka

Featured Posts