BOMOABOMOA YAACHA VILIO NA SIMANZI DAR | BONGOJAMII

BOMOABOMOA YAACHA VILIO NA SIMANZI DAR

Bonyeza HAPA kudownload applicationi ya Bongojamii Blog kwenye simu yako ili kupata habari zetu Haraka
BONYEZA HAPA KU-DOWNLOAD
NI vilio na jasho! Mamia ya waathirika wa bomoabomoa inayoendelea katika eneo la kuanzia Kimara Stop Over, kando ya barabara ya Morogoro -

Wameendelea kukumbana na adha za operesheni hiyo huku wengi wao wakilazimika kuuza vifaa mbalimbali vya ujenzi kwa bei ya chini isiyowahi kutokea katika maeneo mengi nchini.

Nyumba na majengo yaliyokumbwa na bomoabomoa hiyo inayoendeshwa na Wakala wa Barabara (Tanroads) mkoa wa Dar es Salaam, ni zile zilizomo ndani ya umbali wa mita 121.5 kwa kila upande kutoka usawa wa barabara kuu ya kutoka Dar es Salaam kwenda Morogoro.

Vifaa mbalimbali vya ujenzi vinavyookolewa vikiwa salama na baadhi ya waathirika wa operesheni hiyo, vinauzwa kwa bei ya chini kiasi cha kuwavutia wengi. Vifaa hivyo ni pamoja na matofali ambayo baadhi huuzwa kwa Sh. 400 kwa kila moja.

Aidha, vifaa vingine vinavyouzwa kwa bei ya kutupa katika eneo hilo baada ya kuvunjwa kwa utaratibu na kuwa salama ni nondo, mawe, vifusi vya masalia ya matofali yaliyovunjika, madirisha na milango ya chuma, vipande vya mbao na mabati yaliyo katika hali nzuri.

Ubomoaji wa nyumba hizo unaendelea wakati kukiwa na taarifa kuwa wakazi zaidi ya 300 wa eneo hilo 300 wamefungua kesi kuzuia utekelezaji wake katika Mahakama ya Ardhi, hoja ikiwa ni kupinga hatua ya kubomolewa nyumba zao bila fidia ilhali wana hatimiliki ya maeneo yao.

Mwandishi wa Nipashe alifika eneo hilo jana na kushuhudia harakati mbalimbali zinazofanywa na baadhi ya wananchi hao katika kuokoa vifaa vya ujenzi ili kuambulia chochote na kuwapunguzia machungu ya hasara kubwa wanayopata, huku baadhi wakimwaga machozi wakati akizungumza kuelezea hali ngumu wanayokabiliana nayo kwa sasa.

Hata hivyo, wakati mwandishi alipofika eneo hilo jana, hakukuwa na tingatinga za ubomoaji zilizofika kuendelea na kazi hiyo.

Hiyo jana, alifika mama mmoja aliyetajwa kuwa mke wa mmoja wa wabunge wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, akiwa na lori kubwa la mizigo na kununua vifaa mbalimbali kwa bei poa ikiwamo matofali 2,000 aliyokuwa mbioni kuyalipia Sh. 400 kila moja na pia vifaa vingine vya ujenzi kama nondo na mawe.

“Wenye fedha zao wanakuja hapa kujizolea vitu kwa bei karibu na bure… tunapata hasara, lakini ni bora kuuza hivi tunavyoviokoa na kuambulia senti kidogo kuliko vipotee kabisa.

Huyu mke wa mbunge (jina linatajwa) ni mmoja wa wateja waliofika kuchangamkia fursa hii,” alisema mmoja wa waathirika kwenye eneo hilo jana.

MAMA MCHOMA MAHINDI
Akizungumza na Nipashe, mkazi mmojawapo wa Stopover, Halima Abbas, alisema nyumba yake bado haijafikiwa na tingatinga lakini iko mbioni kubomolewa na ilijengwa mwaka 1990 na marehemu baba yake.

Halima ambaye shughuli zake ni biashara ndogondogo ikiwamo ya kuuza mahindi ya kuchoma, alisema nyumba yao hiyo iliyopo maeneo ya stendi amekuwa akiishi na wadogo zake watano na watoto wake watatu, lakini sasa hawajui wapi waende.

“Eneo hili sijui lina ukubwa kiasi gani kwa sababu marehemu baba yetu ndiye alilinunua mwaka 1989 likiwa ni pori na mwaka 1990 alijenga nyumba hii kabla ya kufariki dunia mwaka 2003,” alisema Halima, akiomba wasamaria wafike kumsaidia.

Huku akibubujikwa machozi, Halima aliongeza: “Mtaji wangu ni Sh. 50,000… nanunua mahindi 40 hadi 50. Nikiuza ndiyo napata faida Sh. 6,000 hadi 7,000 ambayo naitumia kulisha familia yangu. Mahindi yakibaki nakosa faida kabisa hivyo kipato changu si cha uhakika… sina pa kwenda, nimebaki na watoto wangu tukisubiri kubomolewa wakati tukiendelea kutafuta msaada wa kwenda pa kujihifadhi.”

DIWANI AZUNGUMZA
Wakati wakazi wengine wa mtaa huo, wakiomba hifadhi kwa ndugu jamaa na marafiki, wananchi zaidi ya 14 hawana makazi baada ya nyumba zao kuvunjwa huku wakiwa hawana sehemu za kwenda.

Diwani wa Kata ya Sangara, Efrem Kinyafu, alilieleza Nipashe jana kuwa wananchi hao ni wale walioanza kuvunjiwa nyumba zao kuanzia Agosti 23 mwaka huu.

Alisema nyumba 50 za wakazi hao zilivunjwa kuanzia siku ya kwanza na wananchi 14 hawana mahali pa kuishi, hali ambayo imeilazimu ofisi ya kata kufungua kambi kwa ajili ya kuwahifadhi.

“Tayari tumeanzisha kamati ya maafa kwa ajili ya kambi ya wananchi hao. Changamoto iliyopo ni kuwa hakuna chakula na tumepata mahema mawili… hayatoshi lakini tunayokodisha kwa Sh. 30,000 kila moja, hali ambayo inatugharimu sana,” alisema.

Kaimu Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa huo, Jumanne Jumaa, alisema mbali na kuwa na zuio la Mahakama ambalo hukumu yake ilikuwa inatoka Agosti 30 mwaka huu, Tanroads walianza kuwabomolea nyumba wakazi hao bila kutoa taarifa serikali ya mtaa huo.

VIBAKA TATIZO WAJIPATIA ULAJI
Juma anasema mbali matatizo waliyopata wananchi ya kubomolewa bila ya taarifa, kumekuwapo na changamoto ya kuongezeka kwa wimbi la vibaka katika mtaa huo.

Juma alisema vibaka hao huiba nondo, matofali, mbali na vifaa vingine vyenye thamani kwenye nyumba zilizobomolewa.

Fredy Kavishe, ambaye amevunjiwa nyumba tano ikiwamo ya kuishi na familia yake na pia nyumba zilizokuwa na wapangaji 27, alisema kuwa sasa analazimika kukodi walinzi wa kulinda mabaki ya nyumba zake ili mwishowe aambulie chochote.

MAUZO YA VIFAA
Mbali na kuuzwa vifaa vya ujenzi kwa bei poa, ipo pia biashara ya kuuza nyumba nzima zinazosubiri kubomolewa kwa bei poa, lengo likiwa ni lilelile la wanunuzi kujitwalia vifaa kama madirisha, mabati, nondo, vifusi nyaya za umeme na matofali ambavyo huviondoa polepole wakitumia mafundi wenye ujuzi wa kazi hiyo. Bei ya nyumba hizo huwa kati ya Sh. milioni moja hadi milioni tatu kutegemeana na ukubwa na hali yake.

Bonyeza HAPA kudownload applicationi ya Bongojamii Blog kwenye simu yako ili kupata habari zetu Haraka

Featured Posts