MAKUBWA HAYA: BIBI AMCHOMA MOTO MJUKUU | BONGOJAMII

MAKUBWA HAYA: BIBI AMCHOMA MOTO MJUKUU

Bonyeza HAPA kudownload applicationi ya Bongojamii Blog kwenye simu yako ili kupata habari zetu Haraka
BONYEZA HAPA KU-DOWNLOAD
MTOTO Elizabeth Musa (8) mkazi wa kijiji cha Azimio Kata ya Salawe, wilayani Shinyanga, amedaiwa kuchomwa moto mikono na bibi yake aliyekuwa akiishi naye kwa madai ya kumwibia Sh. 5,000.

Tukio la kuchomwa moto kwa mtoto huyo na kufungiwa ndani siku 11, lilitokea Agosti 13, mwaka huu, na juzi majirani kugundua mkasa huo na kutoa taarifa kwa uongozi wa kijiji, ambao walifika na kumchukua kwenda hospitalini kupatiwa matibabu.

Mwenyekiti wa Kijiji hicho, Twiga Mashimba, alisema mtoto huyo alichomwa mikono na bibi yake Felister Mdoshi, kwa kuvishwa mifuko ya plastiki na kisha kuwashwa kwa kiberiti, hivyo kumsababishia majeraha makubwa kwenye mikono yote miwili.

Alisema baada ya kumhoji bibi huyo ambaye kwa sasa yuko chini ya Jeshi la Polisi, alisema aliamua kumchoma mikono mjukuu wake huyo ili aache tabia ya kuiba fedha.

Kwa mujibu wa mwenyekiti huyo, bibi huyo alidai kuwa mjukuu huyo amekuwa akifanya hivyo mara kwa mara na amekuwa akimkanya bila mafanikio, hivyo kuamua kuichoma moto mikono yake.

Naye mama mzazi wa mtoto huyo, Eunice Mazinge ambaye alikuwa akiishi mbali na mwanawe baada ya kuolewa na mwanaume mwingine, alisema tukio hilo limemsikitisha sababu alimwamini mama yake na kumwachia binti yake.

Hata hivyo, Eunice alisema kutokana na kitendo hicho kufanywa na mzazi wake, hawezi kumfungulia kesi.

Mganga Mfawidhi Msaidizi wa Kituo cha Afya Salawe, ambako mtoto huyo anapatiwa matibabu, Anastazia Msabila, alikiri wamempokea akiwa na hali mbaya kutokana na vidonda kukaa muda mrefu bila kupatiwa tiba na kwamba vilikuwa vimeanza kuoza.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, Simon Haule, alikiri kutokea kwa tukio hilo na mtuhumiwa wanamshikilia, huku wakiendelea na uchunguzi zaidi na utakapokamilika, mtuhumiwa atafikishwa mahakamani kujibu shtaka linalomkabili

Bonyeza HAPA kudownload applicationi ya Bongojamii Blog kwenye simu yako ili kupata habari zetu Haraka

Featured Posts