BOMOABOMOA YAMFANYA MWENYEKITI AKIMBIE DAR | BONGOJAMII

BOMOABOMOA YAMFANYA MWENYEKITI AKIMBIE DAR

Bonyeza HAPA kudownload applicationi ya Bongojamii Blog kwenye simu yako ili kupata habari zetu Haraka
BONYEZA HAPA KU-DOWNLOAD
Nyumba zilizojengwa katika eneo tengefu lililopo Mbagala, Toangoma Wilaya ya Temeke jijini Dar es Salaam zimewekwa alama ya X kwa ajili ya kubomolewa kutokana na madai ya kujengwa kwenye eneo lisiloruhusiwa kisheria

Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Mtaa wa Masaki Kata ya Toangoma, Hassan Bakari anadaiwa kutoroka akiwa chini ya ulinzi wa Polisi wa Mkoa wa Kipolisi wa Temeke baada ya kukamatwa kwa tuhuma za kuwauzia wananchi wake viwanja ambavyo viko ndani ya hifadhi za Serikali na vingine vya watu.

Imeelezwa baada ya mwenyekiti huyo kuuza maeneo hayo likiwamo lililokuwa limetengwa na Serikali kwa ajili ya kuendeleza ukanda wa kijani linalojulikana kwa jina la Bonde la Makamba, zilijengewa zaidi ya nyumba 300 ambazo sasa zinatakiwa kubomolewa na manispaa ya Temeke.

Akizungumza jana kwa simu, Mkurugenzi Mtendaji wa Manispaa ya Temeke, Nassibu Mbaga alisema Mkuu wa Wilaya hiyo, Felix Lyaviva aliitisha kikao na wananchi hao juzi na kuwataka waondoke kabla ubomoaji huo haujaanza.

“Kikao hicho kikaonyesha aliyehusika kuwauzia viwanja wananchi hao ni mwenyekiti kitendo hicho kilisababisha akamatwe,” alisema.

Mkurugenzi huyo alisema baada ya kukamatwa, wananchi walizingira gari la DC huku wakiwa na jazba wakipinga nyumba zao kubomolewa kitendo ambacho kiliwafanya polisi waliokuwa wamemkata mwenyekiti kumwacha peke yake na kwenda kulinda usalama wa DC hivyo naye akatumia mwanya huo kukimbia.

“Mwenyekiti huyu alikuwa akipata asilimia kumi ya kila malipo ya kiwanja alichosimamia kuuza kwa wastani alikuwa anapata kati ya Sh700,000,” alisema.

DC azungumza

Lyaviva, ambaye pia ni mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya hiyo alisema amemuagiza Mkuu wa Polisi Temeke kumsaka mwenyekiti huyo.

“Ni kweli alikimbia na nimeshamuagiza RPC amtafute na akipatikana akamatwe mara moja. Mpaka sasa (saa tisa mchana) sijapewa taarifa yoyote kama ameshakamatwa,” alisema.

Baadhi ya viongozi wa mitaa ambao nyumba za wananchi wao zitabomolewa baada ya kuuziwa maeneo na mwenyekiti huyo wamesema wananchi hao wanawachukia na kuwaona hawafai.

Mwenyekiti wa Mtaa wa Changanyikeni Kata ya Toangoma, Gwaligano Mwakatobe ambaye pia wananchi wake wamekumbwa na bomoabomoa hiyo alisema Bakari alitumia madaraka yake vibaya kwa kushirikiana na wenye viwanja kuuzia watu maeneo ambayo si salama kwa makazi.

“Amefanya makosa makubwa sana kuwauzia wananchi eneo la Serikali wakati akijua kuwa ni la hifadhi ya Serikali. Wanaoumia sasa ni wananchi ambao nyumba zao zitabomolewa,” alisema.

Pia Mwakatobe aliomba Serikali kuangalia namna ya kuwasaidia wananchi hao kwa kuwapatia maeneo mbadala na kuwaadhibu waliohusika kuuza maeneo hayo.

Mwenyekiti mwingine wa Mtaa wa Malale ambaye pia wananchi wake waliuziwa viwanja na Bakari, Salama Maletter alisema kumekuwa na tabia hiyo ya baadhi ya wenyeviti kuwauzia wananchi maeneo ya wazi.

“Mitaa ambayo inaongoza kwa kuwa na wenyeviti na wajumbe wa matawi ni Vikunani, Kibonde Maji, Mgeni Nani, Mbagala Kuu na Masaki na baadhi ya hawa watu wameuza mpaka maeneo ya makaburi, viwanja vya watu na hifadhi za Serikali,” alisema.

Ofisi ya Mtaa wa Masaki

Waandishi wa Mwananchi walifika Mtaa wa Masaki kwa lengo la kuonana na uongozi lakini walikuta ofisi ikiwa imefungwa huku baadhi ya wananchi waliokuwa jirani wakikataa kuzungumza lolote kuhusu kufungwa kwake.

“Sisi hatujui chochote kuhusu hii ofisi. Mimi hapa ni mgeni nimetoka Msumbiji juzi jioni kwa hiyo sielewi chochote,” alisema mmoja wa wananchi ambao walikuwa wakichomelea mageti jirani na ofisi hiyo.

Wakati waandishi wakizungumza na wananchi hao, alijitokeza mtu mmoja aliyejitambulisha kuwa ni mjumbe wa Serikali hiyo na kuwataka waandishi wasifanye chochote kwa wananchi mpaka watakapopata kibali kutoka kwa mwenyekiti wa mtaa.

Pamoja na zuio hilo, waandishi wetu walishuhudia nyumba kadhaa zilizowekewa alama ya X katika Mtaa wa Masaki ikimaanisha kwamba zinatakiwa kubomolewa. Katika moja ya nyumba hizo, waliwakuta kina mama waliokuwa wamewabeba watoto wao wakiwa wameketi kwa makundi huku wengi wao wakiwa wameshika mashavu.

Maeneo mengine, wanaume nao walionekana wakiwa wamesimama na wengine kukaa chini huku wakiwa wameinamisha sura zao, wengine walishika matawi ya miti yaliyokuwa karibu na maeneo waliposimama.

Bonyeza HAPA kudownload applicationi ya Bongojamii Blog kwenye simu yako ili kupata habari zetu Haraka

Featured Posts