CCM YATANGAZA KUFUTA UCHAGUZI KATA 41 | BONGOJAMII

CCM YATANGAZA KUFUTA UCHAGUZI KATA 41

Bonyeza HAPA kudownload applicationi ya Bongojamii Blog kwenye simu yako ili kupata habari zetu Haraka
BONYEZA HAPA KU-DOWNLOAD
Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimeanza kupeleka salamu kwa wagombea wa nafasi mbalimbali, wanaokiuka Katiba na Kanuni za Uchaguzi, baada ya kufuta uchaguzi wa ndani ya chama hicho katika kata 41 kati ya kata 4,420 zinazoshiriki katika uchaguzi huo, kutokana na kubaini mchezo mchafu na kuagiza mchakato kurejewa upya.


Hayo yalibainishwa jana Dar es Salaam na Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) wa Itikadi na Uenezi, Humphrey Polepole alipozungumza na waandishi wa habari. 


“Hii ni awamu ya kwanza tunapeleka ujumbe kwa sababu wanaCCM wanataka CCM mpya inayosimamia haki, haya ni maelekezo na yanapaswa kuzingatiwa ili kurejesha hali ya uchaguzi katika eneo husika katika namna inayoheshimu Katiba na Kanuni ya Uchaguzi na Uongozi na Maadili,” alifafanua Polepole.


Polepole alibainisha kuwa kufutwa kwa uchaguzi huo ni agizo la viongozi wa juu wa chama hicho akiwemo Mwenyekiti wa CCM Taifa, Rais John Magufuli na Katibu Mkuu, Abdulrahman Kinana baada ya kusikiliza kwa kina kero na malalamiko ya kiuchaguzi ya wanachama wa CCM.


Akifafanua kuhusu suala hilo, alisema baada ya kusikiliza malalamiko hayo, Dk Magufuli alimuelekeza Kinana kuchukua hatua na kwa mamlaka aliyopewa, ameagiza kufutwa na kurejewa upya hivyo wanachama na viongozi wanatakiwa kufuata maagizo hayo.


Alizitaja kata hizo ambazo ni 20, ni za Mkoa wa Dar es Salaam na nafasi zinazotakiwa kurejewa katika mabano ni Kata ya Buguruni (Mwenyekiti na Katibu), Kata ya Liwiti (Katibu), Kata ya Kariakoo (Mwenyekiti, Katibu na Katibu Mwenezi), Kata ya Manzese (Mwenyekiti, Katibu na Katibu Mwenezi), kata za Makuburi, Mabibo na Kigamboni.


Nyingine ni Kiburugwa, Mchafukoge, Gerezani, Segerea (Mwenyekiti na Katibu), Pugu Stesheni (Mwenyekiti, Katibu na Katibu Mwenezi), Kata ya Mianzini, Kata ya Pugu (Katibu Mwenezi), Kata ya Ndugumbi, Kata ya Kilungule, Kata ya Makumbusho, Kata ya Kitunda (Katibu na Katibu Mwenezi), Kata ya Ukonga na Kata ya Msasani.


Polepole alieleza kuwa kata nyingine ni kutoka mikoa mingine ni 18 kutoka kata zote za Wilaya ya Simanjiro Mkoa wa Manyara, Kata ya Seria kwa vijana Wilaya ya Kondoa Mjini Mkoa wa Dodoma nafasi ya Katibu pamoja na Kata ya Mapinga wilayani Bagamoyo mkoani Pwani.


Alizitaja changamoto zilizojitokeza katika maeneo hayo na kusababisha uchaguzi huo kufutwa ni: Kuwepo kwa wanachama wanaoendeleza makundi yaliyokuwepo wakati wa Uchaguzi Mkuu, ambao wamekuwa wakipanga safu za uongozi na kuamua nani atakuwa kiongozi wa chama, jambo ambalo halikubaliki.


Pia alisema wapo viongozi ambao walishindwa kutoa usimamizi mzuri wa mali za chama na kusababisha upotevu mkubwa wa fedha na mali, lakini wamerejea katika nafasi hizo, jambo ambalo pia halikubaliki.


Aidha, alisema wapo wanachama waliokiuka misingi ambayo inamtaka mgombea kuwa mkazi wa eneo ambao unaomba dhamana ya uongozi, lakini kama siyo mkazi wa eneo hilo hupaswi kugombea, lakini wapo ambao si wakazi wameomba dhamana katika maeneo hayo, jambo ambalo halikubaliki.


Katibu huyo wa Itikadi na Uenezi CCM aliongeza kuwa katika uchaguzi huo, pia kumebainika kuwepo kwa vitendo vya uonevu na kutokutenda haki katika mchakato wa uchaguzi, kama ambavyo Katiba ya CCM inavyosema kuwa haki ni asili ya chama hicho.


Alisema changamoto nyingine ni kukiukwa kwa Katiba na Kanuni, baada ya maeneo mengine kutokutoa taarifa sahihi kuhusu wagombea, jambo ambalo limetajwa kama kupotosha vikao.


Machi mwaka huu, Rais Magufuli alionya kuwa mwanachama yeyote atakayebainika kutumia rushwa kwenye uchaguzi wa ndani wa chama hicho, jina lake halitarudi. Aliwataka wanachama wa chama hicho, bila ya kujali uwezo wao kifedha, wajitokeze kwa wingi kugombea nafasi mbalimbali.


Alisema chama kitafuatilia kwa ukaribu mchakato wa uchaguzi wote kuanzia ngazi ya chini ili kujihakikishia kuwa watakaoshiriki kwenye vitendo vya rushwa, watachukuliwa hatua kali kwa mujibu wa Katiba, Kanuni za Uchaguzi na Kanuni za Uongozi na Maadili za CCM.

Bonyeza HAPA kudownload applicationi ya Bongojamii Blog kwenye simu yako ili kupata habari zetu Haraka

Featured Posts