MSIBA SIKU YA EDI EL HAJJ | BONGOJAMII

MSIBA SIKU YA EDI EL HAJJ

Bonyeza HAPA kudownload applicationi ya Bongojamii Blog kwenye simu yako ili kupata habari zetu Haraka
BONYEZA HAPA KU-DOWNLOAD
KAMANDA WA POLISI MKOANI PWANI, JONATHAN SHANA,

NI majanga! Hivyo ndivyo unavyoweza kusimulia kisa kilichomkuta mwanamke mmoja akiwa na watoto wake watatu waliokuwa wakielekea kwenye sherehe ya sikukuu ya Idd el Haj kupata ajali mbaya iliyowafikisha wodini huku mama mwingine akifariki dunia.

Ajali hiyo ilitokea jana baada ya basi la abiria aina ya Toyota Coaster kuparamiwa ubavuni na lori aina ya Fuso lililokuwa likiendeshwa na dereva aliyedaiwa kuwa wakati huo alikuwa amelewa chakari na pembeni yake akiwa na miskoto kadhaa ya bangi.

Kwa mujibu wa mashuhuda, ajali hiyo ilitokea majira ya saa 12:00 asubuhi, eneo la Ujenzi kwenye barabara ya Morogoro wilayani Kibaha, Pwani wakati basi hilo lililojaza abiria likielekea jijini Dar es Salaam.

Mama mwenye watoto watatu, Mwajuma Mbaraka (29), ambaye ni mkazi wa Mlandizi, alikuwa akisafiri na watoto wake watatu kuelekea kula sikukuu yao eneo la Mbande, Dar es Salaam, ni miongoni mwa majeruhi katika ajali hiyo, wengine wakiwa ni pamoja na watoto wake watatu ambao wote wameishia kulazwa katika Hospitali ya Tumbi iliyopo Kibaha. Mtoto mmoja wa mama huyo, aitwaye Ibrahimu Jafari (7), alihamishiwa Hosptali ya Taifa Muhimbili (MNH) baada ya hali yake kuonekana kuwa mbaya huku majeruhi wengine wakipata matibabu na kuruhusiwa.

Kamanda wa Polisi mkoani Pwani, Jonathan Shana, alithibitisha kutokea kwa ajali hiyo na kumtaja aliyefariki kuwa ni Janeth Jackson (40), mkazi wa Mlandizi ambaye alifariki papo hapo.

Akieleza zaidi, Kamanda Shana alimtaja dereva wa Fuso lililosababisha ajali hiyo lenye namba za usajili T235 DET ni Yusuf Said (28), aliyekuwa akitoka Mlandizi kuelekea Dar es Salaam.

Alisema dereva huyo aliligonga gari la abiria aina ya Coaster lenye namba za usajili T. 198 BMG lililokuwa likiendeshwa na Masumbuko Zakaria (40), likitokea Mlandizi kuelekea Mbezi jijini Dar es Salaam.

Alisema chanzo cha ajali hiyo ni mwendokasi wa juu wa lori na ulevi wa dereva huyo wa Fuso ambaye alikuwa akinuka pombe na hata alipopimwa, alikutwa kiasi cha pombe 105 ambacho ni cha juu mno, hasa ikizingatiwa kuwa kwa kawaida, kipimo hicho hakipaswi kuzidi kiwango cha 20.

Alifafanua kuwa dereva huyo wa lori alikuwa kwenye mwendokasi wa juu na alipofika eneo la Ujenzi, ilitokea pikipiki ambayo alipotaka kuikwepa, alirudi kushoto upande wa Coaster na kuigonga ubavuni, hivyo kusababisha ajali hiyo.

Shana alisema baada ya ajali, polisi walimkuta dereva huyo akiwa na chupa za bia na pia dawa za kulevya aina ya bangi misokoto mitano. Hivi sasa anashikiliwa na polisi na atafikishwa mahakamani mapema iwezekanavyo.

“Nataka huyu dereva achukuliwe hatua kali na nitaiomba mahakama imfutie leseni yake maisha… ikiwezekana afungwe ili iwe fundisho kwa madereva kama hawa. Natoa onyo kwa madereva wote kuwa wafuate sheria za usalama barabarani,“ alisema na kuongeza:“Ni vyema wakatambua kuwa usalama wa maisha ya abiria wanaowabeba uko chini yao na kuhakikisha wanawafikisha salama huko wanakokwenda,” alisema Shana.

MAMA NA WANAWE WATATUAkizungumza huku akimwaga machozi jana, mama aliyejeruhiwa akiwa kwenye basi hilo aliwataja wanawe watatu aliokuwa akienda nao kusherehekea Iddi kuwa ni Amina Mohamed (10), Iqram Jafary (3) na Ibrahim Jafari (7).

Alisema waliondoka nyumbani kwao eneo la Janga Mlandizi, mapema alifajiri wakielekea kula Idd kwa mdogo wake aitwaye Swaiba Mbarak anayeishi Mbande.

“Tulichukua boda boda kutoka Janga na tulifika Mlandizi na kupanda Coasta, lakini hadi ajali inatokea sikujua nilishtukia tu imetokea na mwanangu Ibrahim akawa amelegea ghafla, ndiyo tukaletwa Tumbi baadae hali yake ikazidi kuwa mbaya, sasa yuko Muhimbili anauguzwa na baba yake”, alisema.

Bonyeza HAPA kudownload applicationi ya Bongojamii Blog kwenye simu yako ili kupata habari zetu Haraka

Featured Posts