UKATA WA FEDHA WAPELEKEA MRADI KUTOENDELEA | BONGOJAMII

UKATA WA FEDHA WAPELEKEA MRADI KUTOENDELEA

Bonyeza HAPA kudownload applicationi ya Bongojamii Blog kwenye simu yako ili kupata habari zetu Haraka
BONYEZA HAPA KU-DOWNLOAD
MRADI wa umwagiliaji Mtawatawa unaojengwa katika Wilaya ya Liwale Mkoa wa Lindi, umekwama kwa zaidi ya miaka minne kwa kukosa fedha.




Mradi huo wenye thamani ya Shilingi bilioni 4.5 na wa pili kujengwa wilayani humo, unagharamiwa na serikali kwa kushirikiana na wafadhili. Mpaka sasa umeshatumia Shilingi milioni 739.

Mradi mwingine uliokwama ni wa Ngongowele wenye thamani ya Shilingi bilioni 1.3, ambao hata katika bajeti ya sasa haujakumbukwa kutengewa fedha.

Ingawa mradi wa Mtawatawa umeanza kutumiwa na wakulima licha ya kwamba hata nusu ya fedha zilizopangwa kugharamia hazijatumika.

Msimamizi wa mradi huo, Mhandisi Ramadhan Kazimoto anasema, lengo la mradi ni kuzifikia hekta 600 ambazo ni sawa na ekari 1,500 za ardhi na kwamba tayari ujenzi wa mabanio mawili, mfereji mkuu mmoja na vigawa maji 25 umekamilika.

"Kadhalika, Ujenzi wa karavati tatu na daraja dogo moja umekamilika, vyote vikigharimu Shilingi milioni 739," amesema.

Anasema kuwa kampuni za Eima General Supplies Co.Ltd, Kipera Company na Masaho General Supplies & Construction Co.Ltd, ndizo zimejenga mradi huo hadi ulipofikia.

Hata hivyo, wakulima wanaotumia skimu hiyo kwa kilimo cha mpunga, wanasema kuwa bado hawajaanza kunufaika kwa sababu inatumika nyakati za masika tu, hivyo kuambulia mavuno kidogo.

Kiongozi wa wakulima wa skimu ya Mtawatawa, Asia Junguli anasema kuwa hadi sasa ni wakulima 191 tu ndio wanaolima mpunga kati ya 275 waliojiandikisha.

Anasema kama ilivyo kwa wenzake, walianza kutumia skimu hiyo msimu wa kilimo wa 2014 na kwa misimu yote mitatu, alivuna kati ya gunia nane na 10 tu mpunga katika ekari moja aliyopewa.

"Kwa kipindi chote cha misimu mitatu tuliyolima,mradi huu bado haujatupa tija, labda kama ungekuwa unatumika hadi nyakati za kiangazi," anasema.

Mkulima mwingine anayetumia miundombinu ya mradi huo Sokomoko Kambona anasema alianza kilimo mwaka 2014, lakini hajawahi kuvuna zaidi ya gunia 10 za mpunga kwa ekari moja badala ya kati ya gunia 25 na 40.

Anasema hawalimi nyakati za kiangazi kwa sababu skimu haina bwawa la kuhifadhia maji.

"Skimu ya Mtawatawa ipo katika bonde linalounganisha mito miwili ya Mihumo na Kipure na wakulima waliojitokeza ni wachache kwa sababu bado haijaleta tija na wakulima hawajahamasishwa ipasavyo," anasema.

Rehema Nachima ni mkulima wa mpunga katika skimu hiyo, anasema licha ya kuwa katika umoja wenye wakulima sitaki kila kikundi, kuna uwezekano wanakikundi kupungua misimu ijayo kwa sababu mradi haujanufaisha wengi.

Anasema, ukiondoa skimu kutotumika hadi kiangazi, wataalam wa kilimo hawafiki katika mashamba yao kwa wakati ili kuwapa utaalam, hivyo kuchangia wakulima kulima, kupanda na kupalilia bila maelekezo ya kitaalam.

"Wakati mwingine wataalam wakitutembelea na kutupa maelezo, bado upatikanaji wa mbegu bora na pembejeo za kilimo hasa vijijini huwa ni mgumu. Tunaomba serikali iyape umuhimu mambo hayo," anasema Nachima.
Ofisa Ugani wa kata ya Mlembwe wilayani Liwale, Mwenye Navaranga, anakiri kuwa kuna changamoto nyingi zinazowakabili wakulima wa wilaya hiyo wakiwamo wqnaotumia skimu ya Mtawatawa.

"Baadhi ya changamoto hizo ni utayari wao katika kupokea maelezo ya kitaalam ya jinsi ya kupata mbegu, wakulima na kuyafanyia kazi. Kadhalika upatikanaji wa pembejeo ni changamoto nyingine,hasa ikizingatiwa wengi Hawa hawana uwezo wa kuzununua," anasema.

Navaranga anasema kwa kutambua changamoto hizo, Ofisi yake ya kata kwa kushitikiana na wilaya ya Liwale, wameanza kutekeleza mpango mahsusi wa serikali wa kuhakikisha inasambaza pembejeo za kilimo kwa wakati hadi vijijini.

Kaimu Ofisa Kilimo Wilaya ya Liwale (Daico), Salvatory Kalokola anakiri kuwa, kukwama kwa mradi huo na ule wa Ngongowele, kimefifisha ndoto za wakulima wengi ambao walijipanga kuzalisha mazao mengi hasa ya mpunga.

"Kama mradi huu ungekamilika na kuanza kazi, wakulima wangezalisha mpunga hadi kufikia gani 5,351.3 kutoka tani 2,351 za sasa kwa msimu wa kilimo uliopita wa mwaka 2015/16," anasema.

Kalokola anaongeza kuwa matarajio ya wilaya ilikuwa ni kuzalisha mpunga gunia 3,753.8 lakini kutokana changamoto mbalimbali ikiwamo upatikanaji wa pembejeo kwa wakati na ukosefu wa mvua za kutosha imeishia tani 2,395.9 tu.

"Kwa upande wa zao la mahindi, lengo la wilaya ni kuzalisha lilikuwa tani 16,295.9 na badala yake mavuno yaliyopatikana ni tani 13,286.7 na endapo mradi ungeanza uzalishaji ungeongeza mahindi hadi kufikia tani 26,671.2 kwa msimu mmoja," amesema Kalokola.

Kaimu Mkitugenzi Mtendaji wa Halmashauri wa Wilaya ya Liwale, Damas Mumwi amesema inafanya kila jitihada kuhakikisha wakulima wanaotumia skimu hiyo wananufaika licha ya kwamba Ujenzi wake umekwama.

"Kama wilaya tunachofanya kwa sasa ni kuhamasisha wakulima wanatumia miundombinu ya mradi iliyojengwa kulima mpunga kwa sababu tumebaini kwamba, bado wanaweza kunufaika badala ya kusubiri hadi ukamalike kabisa," anasema.

Mumwi anasema sababu za kukwama kwa mradi huo hakutofautiani sana na ule wa Ngongowele kwa sababu yote imesimama kwa kukosa fedha.

Kaimu Mkurugenzi wa Uendeshaji wa Miundombinu Taifa, Mhandisi Pascal Shayo anasema serikali inatambua changamoto zinazoukabili mradi wa Mtawatawa na mingine kadhaa nchini, sababu ni ukosefu wa fedha.

Shayo anasema hata katika bajeti kuu ya serikali ya mwaka wa 2017/18 serikali haijatenga fedha zozote kwa ajili ya kumalizia miradi hiyo, zaidi ya kutegemea wafadhili watoe fedha.

"Skimu ya Mtawatawa na Ngongowele ni baadhi tu ya miradi zaidi ya 62 mikubwa ya umwagiliaji inayoendelea kijengwa nchini, lakini imekosa fedha za kumalizia kwa sababu sehemu kubwa ya fedha hizo zinatolewa na wafadhili, wakiwemo Jica Tanzania.

Tukipata fedha tutaendelea na ujenzi hadi itakapokamilika," anasema Mhandisi Shayo.

Bonyeza HAPA kudownload applicationi ya Bongojamii Blog kwenye simu yako ili kupata habari zetu Haraka

Featured Posts