Bonyeza HAPA kudownload applicationi ya Bongojamii Blog kwenye simu yako ili kupata habari zetu Haraka
BONYEZA HAPA KU-DOWNLOAD
Dar es Salaam. Kauli ya Waziri wa Mambo ya Ndani, Mwigulu Nchemba kuwa wataendelea kupata misukosuko hadi watakapowataja wahusika wa mauaji mfululizo, haijapita kirahisi; imepingwa vikali.
Mwigulu alitoa kauli hiyo katika mkutano wa wakazi wa Bungu alipofanya ziara katika moja ya wilaya za mkoani Pwani ambazo zimekumbwa na mauaji ya wenyeviti na watendaji wa vijiji na vitongoji.
Mwigulu amesema wanaofanya mauaji hayo hawatoki mbali na kuwatuhumu baadhi ya wakazi kuwa wanawafahamu watu wanaofanya unyama huo.
“Haiwezekani wauaji wakatoka Kigoma au Kagera wakaja Rufiji na kumuua kiongozi wa CCM na kuondoka salama. Sasa kama mnaishi na wauaji au na wanaoshirikiana na wauaji, watajeni vinginevyo mtapata misukosuko,” amesema Mwigulu.
Tayari takriban watu 31, wakiwamo viongozi na askari wa Jeshi la Polisi, wameshauawa katika wilaya za Rufiji, Kibiti na Mkuranga kwa mujibu wa taarifa ambazo Mwananchi imezifuatilia kuanzia Mei mwaka jana.
Jeshi la Polisi limeweka kambi maalumu maeneo hayo na kupiga marufuku mizunguko kuanzia saa 12:00 jioni, huku wananchi wakilalamikia kukamatwa, kupigwa na kuwekwa mahabusu bila ya maelezo.
Mratibu wa Mtandao wa Wapigania Haki za Binadamu (THRD), Onesmo Ole Ngurumwa amesema kauli hiyo haikupaswa kutolewa na kiongozi wa Serikali kwa kuwa si lazima wauaji wakawa wanashirikiana na wenyeji.
Amesema kama kiongozi mwenye dhamana, Mwigulu alitakiwa kuzungumza kwa utaratibu na wakazi wa eneo hilo kujadiliana ili kupata namna ya kukabiliana na mauaji hayo.
“Tunakemea kauli hiyo,” amesema Ole Ngurumwa.
Maoni hayo yanashabihiana na yaliyotolewa na kaimu mkurugenzi wa Kituo cha Haki za Binadamu LHRC, Anna Henga ambaye amesema vitisho hivyo kwa wananchi havina sababu.
Bonyeza HAPA kudownload applicationi ya Bongojamii Blog kwenye simu yako ili kupata habari zetu Haraka