POLISI WATANGAZA DAU NONO LA MIL 60 KWA ATAKAE WAKAMATISHA WATUHUMIWA 12 | BONGOJAMII

POLISI WATANGAZA DAU NONO LA MIL 60 KWA ATAKAE WAKAMATISHA WATUHUMIWA 12

Bonyeza HAPA kudownload applicationi ya Bongojamii Blog kwenye simu yako ili kupata habari zetu Haraka
BONYEZA HAPA KU-DOWNLOAD
JESHI la Polisi mkoa wa Pwani limetangaza zawadi ya Sh. milioni tano kwa mwananchi ambaye atafanikisha kukamatwa kwa watuhumiwa 12 ambao limedai wanajihusisha na mtandao wa mauaji yanayoendelea katika Wilaya za Kibiti, Mkuranga na Rufiji.


Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Kamishna Msaidizi Mwandamizi Onesmo Lyanga, aliwaambia waandishi wa habari jana kuwa Jeshi hilo linaendelea kuwasaka watuhumiwa hao.


Alisema Polisi imepata picha za baadhi ya watuhumiwa na fununu za mahali wanapopenda kutembelea mara kwa mara.


MAJINA YA WATUHUMIWA
Kamanda Lyanga aliwataja watuhumiwa hao pamoja na mwanzilishi wa mtandao huo wa mauaji kuwa ni Abdurshakur Ngande Makeo, Faraj Ismail Nangalava, Anaf Rashid Kapera, Said Ngunde na Omary Abdallah Matimbwa.


Wengine ni Shaban Kinyangulia, Haji Ulatule, Ally Ulatule, Hassan Uponda, Rashid Salim Mtulula, Sheikh Hassan Nasri Mzuzuri na Hassan Njame.


“Jeshi letu limewabaini watuhumiwa hao kwa kushirikiana na wasiri wetu huku tukiendelea na uchunguzi zaidi," alisema Kamishna Lyanga.


Alisema polisi imegundua kuwa watuhumiwa hao hupendelea kutembelea maeneo ya kisiwa cha Simbaulanga, kisiwa cha Saninga katka kijiji cha Nchinga na kijiji cha Mfesini kata ya Nyamisati pamoja na maeneo mbalimbali ya wilaya za Kibiti, Rufiji na Mkuranga.


Kamishna Lyanga aliwataka wananchi kuendelea kutoa ushirikiano wa kuwafichua watuhumiwa wote wa mtandao ambao unahatarisha hali ya usalama mkoani hapa.


LHRC KUANIKA UKWELI
Jijini Dar es Salaam, Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu(LHRC), kimesema hakijaridhika na hatua ambayo inachukuliwa na serikali chini ya Wizara yake ya Mambo ya Ndani katika kushughulikia mauaji yanayoendelea nchini na kuitakata kutafuta njia madhubuti ya kudhibiti mauaji hayo.


Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Kaimu Mkurugenzi wa LHRC, Anna Henga, alisema kumekuwa na matukio ya mfululizo katika kipindi kifupi hususani katika Mkoa wa Pwani, lakini mpaka sasa hawaoni njia mbadala ambayo imefanywa na serikali kuhusu mauaji hayo.


Alisema kupeleka askari wengi Mkoa wa Pwani na maeneo mengine kunakotokea mauaji hayo hakutasaidia endapo hakutafanyika uchunguzi wa kina kujua chanzo chake.


“Kinachotakiwa hapa ni kuhakikisha inatafutwa njia madhubuti ambayo itasaidia kuja na majibu ya kutatua tatizo hili, wafanye uchunguzi wa kawaida wa kijamii, kukaa na wananchi, tunaamini watapata tu sababu zake na hapo ndipo itakuwa mahali pazuri pa kuanzia na hii pia itasaidia wao kujua ni mbinu gani watumie kuwashughulikia,” alisema.


Alisema LHRC ilipeleka timu yake mkoani Pwani kwa ajili ya kufanya uchunguzi juu ya matukio hayo ya mauaji na kwamba hivi sasa wako katika hatua za mwisho za mapitio ya ripoti ya uchunguzi na itasomwa hadharani ikikamilika.


Mauaji ya raia na hasa viongozi wa kisiasa katika wilaya hizo za mkoa wa Pwani yalianza kama utani Aprili 30 mwaka jana alipopigwa risasi mwenyekiti wa kijiji, Said Mbwana kabla ya kushika kasi na kupoteza maisha ya watu zaidi ya 30 wakiwamo polisi.


Kiongozi wa mwishoni kuuawa ni aliyekuwa Katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kata ya Bungu wilayani Kibiti na mkoani Pwani, Arife Mtulia wiki iliyopita.
Mtulia aliuawa nyumbani kwake na watu wasiojulikana ambao hawakuchukua chochote wakati akienda kuoga usiku.


Kifo cha Mtulia kimekuja huku kukiwa na operesheni kabambe ya kusaka majambazi yaliyoua polisi nane katika eneo la Mkengeni, Kata ya Mjawa katikati ya mwezi uliopita.


Polisi inaendesha kimyakimya operesheni hiyo kwa hofu ya kuanika kinachofanywa na kikosi cha operesheni katika kuchunguza tukio hilo.
Polisi hao waliuawa saa 12:15 jioni wakati wakitoka lindo kuelekea kambini.


Waliouawa ni Mrakibu Msaidizi wa Polisi, Peter Kigugu, askari mwenye namba F.3451, Koplo Francis, F.6990 Konstebo Haruna, G. 3247 Konstebo Jackson, H.1872 Konstebo Zacharia, H.5503 Konstebo Siwale, H. 7629 Konstebo Maswi na H. 7680 Konstebo Ayoub.


Majambazi hao walipora bunduki saba ambazo ni SMG nne na Long Range tatu zikiwa na risasi zake.


Operesheni hiyo inayoendelea kwenye mapori na maeneo mengine inahusisha vyombo vya ulinzi na usalama.


Imeandikwa na Robert Temalilwa na Magreth Malisa, KIBAHA na Elizabeth Zaya, DAR

Bonyeza HAPA kudownload applicationi ya Bongojamii Blog kwenye simu yako ili kupata habari zetu Haraka

Featured Posts