Bonyeza HAPA kudownload applicationi ya Bongojamii Blog kwenye simu yako ili kupata habari zetu Haraka
BONYEZA HAPA KU-DOWNLOAD
MAHAKAMA Kuu Kanda ya Dar es Salaam imepanga leo kutoa uamuzi mdogo dhidi ya zuio la muda la kuapishwa kwa wabunge wapya wa viti maalum wa Chama cha Wananchi (CUF), baada ya kusikiliza hoja za pande zote mbili.
Uamuzi huo pia unahusu pingamizi la Mwanasheria Mkuu wa Serikali dhidi ya maombi ya wabunge 8 na madiwani wawili wa nafasi hizo waliofukuzwa uanachama CUF.
Uamuzi huo utasomwa mbele ya Jaji Lugano Mwandambo aliyepangiwa kusikiliza kesi hiyo.
Awali, wabunge na madiwai hao wameomba maombi ya zuio la kuapishwa kwa wabunge hao wapya, hadi kesi yao waliyoifungua kupinga kufukuzwa uanachama itakapotolewa uamuzi.
Jana Wakili wa walalamikaji, Peter Kibatala, aliiomba mahakama iamuru hali hiyo iendelee hadi siku ya uamuzi wa pingamizi hilo.
Maombi ya wabunge na madiwani hao yalitarajiwa kusikilizwa jana mbele ya Jaji Mwandambo, lakini jopo la mawakili wa Serikali likiongozwa na Wakili wa Serikali Mkuu, Vincent Tango, alidai wamewasilisha pingamizi la awali.
Jaji Mwandambo alisema pingamizi hilo liwasilishwe kwa njia ya maandishi, upande wa walalamikiwa wawasilishe hoja zao Agosti 18, upande wa walalamikaji uwasilishe majibu Agosti 21 na Agosti 22 upande wa AG nao utajibu na uamuzi utatolewa Agosti 25.
Kibatala alidai kifungu cha sheria kilichopingwa hapo awali wamekibadilisha na kuja na kifungu cha 95 Cha Sheria ya Mwenendo wa Madai.
Walalamikaji, wanapinga kuapishwa kwa wabunge nane walioteuliwa na kutangazwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC)
Wabunge walioteuliwa na NEC katika kikao chake cha Julai 27 mwaka huu ni Rukia Ahmed Kassim, Shamsia Aziz Mtamba, Kiza Hussein Mayeye, Zainab Mndolwa Amir, Hindu Hamis Mwenda, Sonia Juma Magogo, Alfredina Apolinary Kahigi na Nuru Awadh Bafadhili.
Awali katika maombi hayo Jaji Mwandambo ,alisema mahakama imeamua kutupilia mbali maombi hayo kutokakana na kuwapo kwa mapungufu ya kisheria.
Alisema maombi yaliyotolewa na waliokuwa wabunge nane wa viti maalum waliovuliwa uanachama na CUF na kupoteza ubunge wao hayajajitosheleza kisheria.
Jaji Mwandambo alisema wabunge hao waliwasilisha mapingamizi manne, lakini kati ya hayo mahakama imejibu pingamizi moja lilokuwa na hoja na kusema kifungu kilichotumika kufungua maombi hayo sio sahihi hivyo mahakama imetupilia mbali.
Alisema maombi mengine matatu hayawezi kusikilizwa kutokana na pingamizi hilo moja lenye hoja kuwa na mapungufu ya kisheria.
Wabunge hao nane waliovuliwa ubunge walipeleka maombi yao wakiomba mahakama itoe amri ya zuio dhidi ya wabunge nane wateule kuapishwa.
Katika maombi hayo madogo namba 447 ya mwaka huu ilieleza mdaiwa wa kwanza ni Katibu wa Bunge, huku mdaiwa wa pili akiwa Mwenyekiti wa NEC, na mdaiwa wa tatu ikiwa ni Bodi ya wadhamini wa CUF pamoja na wabunge nane wateule.
Wabunge hao walifungua maombi katika mahakama hiyo wakiomba mahakama itoe amri ya zuio kwa Bunge ili wabunge walioteuliwa baada ya wao kuvuliwa uanachama wasiapishwe kusubiri kusikilizwa na kutolewa maamuzi ya kesi waliofungua kupinga kuvuliwa uanachama.
Uteuzi huo wa wabunge hao wateule wa CUF ulifanyika baada NEC kupokea taarifa kutoka kwa Spika wa Bunge ambaye kwa mujibu wa Kifungu cha 37(3) cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, Sura ya 343 aliitaarifu NEC kuwapo kwa nafasi wazi nane za Wabunge wa Viti Maalum kupitia CUF.
Bonyeza HAPA kudownload applicationi ya Bongojamii Blog kwenye simu yako ili kupata habari zetu Haraka