Bonyeza HAPA kudownload applicationi ya Bongojamii Blog kwenye simu yako ili kupata habari zetu Haraka
BONYEZA HAPA KU-DOWNLOAD
AMA kweli hujafa hujaumbika! Kile kilichomtokea Hassan Rajabu (70), ndicho kinachothibitisha ukweli wa msemo huo wa wahenga.
Ni kwamba, baada ya kuishi na upofu kwa miaka takribani 20, hatimaye Hassan, mkazi wa Kijiji cha Majani Mapana kilichopo katika Wilaya ya Muheza mkoani Tanga, amefunguka macho na kusimulia mengi asiyowahi kutarajia hapo kabla.
Akizungumza kwa kwikwi itokanayo na furaha ya kutoamini hadi sasa juu ya kile kilichomtokea, Mzee Rajabu alisema kuwa kuna mengi yalimtokea katika kipindi chote cha kutowahi kuiona nuru ya jua kwa miaka 20, lakini mojawapo kati ya mengi aliyokuwa akiwazia kupata fursa yake walau siku moja ni kuwaona walau pichani, marais wawili walioingia madarakani wakati yeye akiwa kipofu -- ambao ni Jakaya Kikwete maarufu kama JK na John Magufuli (JPM).
“Nakumbuka nilipatwa na upofu mwaka 1997. Tangu hapo sijawahi hata kuuona mwanga wa jua. Ni maisha yaliyokuwa na giza nene kwangu,” alisema Mzee Rajabu, kumueleza mwandishi katika mahojiano yake maalumu juzi.
Rais wa awamu ya tatu, Benjamin Mkapa ndiye aliyekuwa madarakani wakati Rajabu akipatwa na upofu mwaka 1997, kabla ya kufuatiwa na Kikwete (2005) na Magufuli aliyeapishwa Novemba 5, 2015 baada ya kushinda katika uchaguzi mkuu uliofanyika Oktoba 25, 2015.
Mzee Rajabu ni miongoni mwa wananchi takribani 500 waliokuwa wamejitokeza katika kampeni ya upimaji wa macho na kutoa huduma ya upasuaji wa mtoto wa jicho kwa kila aliyekutwa na tatizo hilo.
Huduma hiyo ya matibabu ya bure ya macho, iliratibiwa katika katika Kituo cha Afya cha Ubwani na kufanikishwa na madaktari wa Taasisi ya Afya ya Medewell iliyopo Kibaha mkoani Pwani.
Mbunge wa zamani wa Jimbo la Muheza, Hebert Mtangi, alisaidia kwa kiasi kikubwa ujio wa huduma hiyo ya bure kutoka Medewell wilayani Muheza, wengine wakiwa ni Diwani wa Kata ya Misozwe, Jestina Mntangi na Mratibu wa Huduma ya Magonjwa ya Macho Wilaya ya Muheza, Aderina Swai.
“Kiukweli hadi sasa ni kama siamini. Najiona ni kama mtoto mchanga. Hata fimbo yangu ya kutembelea nilishaachana nayo na sijui ilipo,” alisema Rajabu kabla ya kuongeza:
“Baadhi ya majirani pia wananishangaa kuona nikiwa na uwezo wangu wa kuona kama wao. Nimeishi na upofu kwa miaka mingi,” alisema Rajabu aliyekuwa akiangaza macho yake muda wote.
Rajabu alisema enzi zake alikuwa dereva, lakini baada ya kupatwa na upofu, alijikuta akibaki kuwa ombaomba na maisha yake yakiwatumai zaidi watoto zake sita wanaoishi katika maeneo tofauti nchini, ikiwamo jijini Dar es Salaam.
Mbali na kueleza kuhusu namna alivyojawa na shauku ya kuona sura za JPM na JK wakiwa tayari marais, Mzee Rajabu alisema kuna vitu vingi vimebadilika katika miaka yake 20 ya kutowahi kuliona jua, mojawapo ikiwa ni nyumba yake ambayo sasa imechakaa zaidi kulinganisha na vile ilivyokuwa awali wakati akipoteza uwezo wa kuona.
Mengine yaliyomshangaza tangu alipofungua macho yake ni pamoja na kuwapo kwa majengo mapya mazuri asiyowahi kuyaona kwenye eneo lao hapo kabla, barabara safi na pia majengo yaliyoboreshwa zaidi ya Kituo cha Afya cha Ubwari.
“Kuna mambo mengi yamebadilika…nimebaki kushangaa kila mara. Furaha bado imenijaa,” alisema Mzee Rajabu.
ALIVYOPATA UPOFU
Akisimulia vile ilivyokuwa hadi akawa miongoni mwa walemavu wa macho kwa kipindi cha miaka 20, Rajabu alisema tatizo la macho lilimuanza kitambo, labla hata kabla ya mwaka 1997.
Alisema jicho lake lake la upande wa kushoto ndilo lililoanza kumletea shida baada ya kuwa na kawaida ya kumuwasha kila mara.
Akisimuliza zaidi, Rajabu alisema kuwa baada ya kuona hivyo, alikwenda hospitali kwa nia ya kutafuta tiba na awali, matokeo ya uchunguzi wa madaktari yalionyesha kuwa anasumbuliwa na ugonjwa wa trakoma.
Baadaye, jicho la pili (upande wa kulia) nalo likaanza kumuwasha, hivyo akajikuta akishindwa kuendelea na kazi yake ya udereva wa malori katika katika kampuni mbalimbali.
“Matatizo yalinianza kama mzaha. Wakati nikiendelea kuhangaika huku na kule kutafuta tiba, ghafla nikapoteza kabisa uwezo wa kuona,” alisema.
Rajabu aliongeza kuwa hali hiyo ilimpa wakati mgumu kwa sababu kuanzia wakati huo ambao ni mwaka 1997, akawa tegemezi. Akawapoteza baadhi ya wapendwa wake kwa sababu wapo waliochoshwa na hali yake ya kuwategemea kwa mambo mengi kiuchumi.
Mzee Rajabu alizitaja hospitali mbalimbali maarufu nchini alizowahi kwenda mwenyewe na pia kupelekwa na watoto wake, ili kutibiwa, lakini kote huko ilionekana kuwa njia pekee ni kumchuna macho, lakini hilo kushindikana kwa sababu ya kile alichodai kuwa ni kusumbuliwa pia na tatizo la ‘presha ya macho’.
“Mwanzoni nilipata tabu sana katika kupata huduma za msingi kama kwenda msalani na kuoga…baadaye nikaizoea hali ya upofu na kuikubali. Hakukuwa na namna nyingine,” alisema.
NI KAMA MUUJIZA
Katika namna asiyoitarajia, Rajabu alisema kuwa hivi karibuni, akapata mgeni nyumbani kwake, ambaye alijitambulisha kwa jina la Judith, ambaye ni mmoja wa wauguzi.
Alisema muuguzi huyo alimpa taarifa za ujio wa madaktari wa Medewell waliofika Muheza kutoa huduma ya upimaji na upasuaji wa jicho la motto na hivyo kumtaka naye ajumuishwe ili afanyiwe uchunguzi na pengine, kwa uwezo wa Muumba, anaweza kupona.
Akieleza zaidi, alisema kuwa awali alikataa wazo hilo kwa sababu alishahangaika sana na kukata tamaa.
“Nilishakwenda katika hospitali kubwa karibu zote na pia wengine walishanipeleka kwa waganga wa kienyeji…kote huko sikufanikiwa,” alisema Rajabu.
Alisema licha ya kueleza msimamo wake, muuguzi huo (Judith) aliendelea kumbembeleza na kumjia tena na tena kumsihi aende akajaribu bahati yake mbele ya madaktari bingwa wa macho, jambo lililomlazimu kukubali hatimaye kwa nia tu ya kumridhisha huyo muuguzi.
Alisema baada ya hapo, alichukuliwa na bodaboda na kufikishwa katika Hospitali Teule ya Wilaya ya Muheza ambako alionana na madaktari. Alipopimwa, majibu yakawa mazuri kwake baada ya kuambiwa kuwa ataweza kuona tena baada ya kufanyiwa upasuaji wa mtoto wa jicho.
Mwishowe yale aliyokuwa akiyachukulia kuwa ni mambo ya kimiujiza kwake yakatokea kuwa kweli baada ya kuhamishiwa katika Kituo cha Afya Ubwari ambako alifanyiwa upasuaji na kurejewa na uwezo wake wa kuona katika siku ya pili tu baada ya kushinda wodini siku moja akiwa na bandeji usoni.
“Nilipoondolewa bandeji niliyowekwa baada ya kufanyiwa upasuaji, nikashangaa kila nilichokiona jirani yangu,” alisema Rajabu, huku akikiri kumsahau mtoto wake aitwaye Mariam, aliyekuwa naye hospitali wakati wa kufanikisha harakati za upasuaji.
MIKASA AKIWA NA UPOFU
Rajabu alisema kuwa kati ya matukio mengi yaliyomkuta katika changamoto za miaka 20 ya kuishi na upofu, ni pamoja na kutomuona mtoto wake mmojawapo aitwaye Hassan wakati alipofariki na kuzikwa na pia kuibiwa vitu vyake vingi nyumbani bila ya kuwa na uwezo wa kuwakabili wahalifu. Pia janga jingine asilosahahu ni kukimbiwa na baadhi ya wapendwa wake.
Aidha, miongoni mwa ukarimu aliowahi kuupata kutoka kwa watu walio karibu naye ni pamoja na kusaidiwa fimbo ya kutembelea aliyopewa na jirani yake aitwaye Kwasemwaliko.
Mikasa mingine asiyosahau ni fedha na vitu alivyovipoteza kila mara alipokwenda kwa waganga wa kienyeji ili kutibiwa upofu, baadhi ikiwa ni mbuzi na majogoo ya rangi mbalimbali kulingana na maelekezo aliyokuwa akipewa ambayo mwishowe alibaini kuwa yote yalijaa uongo.
“Namshukuru Mwenyezi Mungu kwa rehema zake, nawashukuru madaktari (kutoka Medewell) walionipatia huduma hii bila gharama yoyote na pia wale waliowaleta huku kwetu,” alisema Rajabu.
Bonyeza HAPA kudownload applicationi ya Bongojamii Blog kwenye simu yako ili kupata habari zetu Haraka