VURUGU ZATIBUA UCHAGUZI WA CCM SIMANJIRO | BONGOJAMII

VURUGU ZATIBUA UCHAGUZI WA CCM SIMANJIRO

Bonyeza HAPA kudownload applicationi ya Bongojamii Blog kwenye simu yako ili kupata habari zetu Haraka
BONYEZA HAPA KU-DOWNLOAD
Wanachama wa CCM, Kata ya Endiamtu, Simanjiro mkoani Manyara wakizozana mbele ya polisi baada ya kushindwa kufanya uchaguzi jana. Picha na Joseph Lyimo 

Mirerani. Uchaguzi wa viongozi wa CCM Kata ya Endiamtu mji mdogo wa Mirerani wilayani Simanjiro mkoani Manyara uliokuwa ufanyike jana, umeahirishwa baada ya kutokea vurugu za wanachama waliokuwa wakipinga majina ya wagombea wanaowaunga mkono kukatwa.

Vurugu hizo zilizotokana na madai ya wanachama hao kwamba majina ya wagombea makini yalikatwa na badala yake kupitishwa ambayo walidai kuwa ni watu dhaifu wasioweza kukivusha salama chama hicho kilichopoteza nafasi ya udiwani na ubunge kwa wapinzani wao Chadema.

Hali ya hewa ilianza kuchafuka baada ya wasimamizi wa uchaguzi huo, mjumbe wa kamati ya siasa ya CCM wilaya hiyo, Awadhi Omari na katibu wa UVCCM wa wilaya hiyo, Bakari Mwacha kusoma majina ya waliopitishwa kugombea nafasi mbalimbali.

Mwacha alitaja majina matatu yaliyopitishwa kugombea uenyekiti wa CCM wa kata hiyo kuwa ni Claudia Dengesi, Paul Kiula na Sifael Saitore na kuzusha sintofahamu baada ya kukosekana kwa jina la Elisha Mnyawi ambaye ni mfanyabiashara maarufu wa madini ya tanzanite.

Mwenyekiti wa Kitongoji cha Tupendane, Isaya Abayo alihoji sababu za jina la Dengesi kurudishwa ilihali alishachaguliwa kuwa mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake (UWT) wa kata hiyo na kukata majina ya wagombea wengine wenye uwezo mkubwa wa kiutendaji.

“Mwenyekiti wa CCM, Rais John Magufuli alishatoa maagizo kuwa kwenye CCM mpya ni mtu mmoja nafasi moja, sasa inakuwaje huyu mama anapatiwa nafasi nyingine ya kugombea wakati ni mwenyekiti wa UWT?” alihoji.

Mwenyekiti wa Kitongoji cha Tanesco, Justin Abraham aliunga mkono kauli ya Abayo na kusema CCM ni chama cha wanachama wote na kila mmoja ana hisa moja hivyo kisigeuzwe kuwa kundi la familia.

“Mimi sina imani na hawa wasimamizi kwani ndiyo wanasababisha migogoro kwenye hizi kata za Mirerani na Endiamtu, badala ya kutufanya tuungane ili kuwaondoa Chadema kwenye kata na wilaya,” alisema Abraham.

Mwanachama mwingine Japhary Matimbwa alisema ni jambo la kushangaza kukatwa kwa majina ya watu makini wenye ushawishi mkubwa kwa jamii na viongozi, huku majina ya watu dhaifu na mengine ya familia moja yakipitishwa kwa upendeleo.

“Haiwezekani jina la Meya wa Mji mdogo wa Mirerani, Adam Kobelo na mtu makini kama Elisha Mnyawi na Oscar Gunewe yanakatwa, kisha yanapitishwa mengine ambayo hayana ushawishi kwa jamii, hawa hawawezi kukipitisha chama kwenye huu wakati mgumu,” alisema Matimbwa.

Akijitetea Mwacha aliwaambia wanachama hao kuwa wao walikuwa wasimamizi tu wa uchaguzi huo na suala la kupitishwa kwa majina, linahusu uongozi wa CCM ngazi za wilaya na mkoa.

Baada ya majibu hayo, baadhi ya wanachama walianza kuzozana wakinyan’ganyana simu kwa madai ya wengine kurekodi sauti na picha hali iliyosababisha waanze kurushiana viti.

Kutokana na vurugu hizo zilizodumu kwa zaidi ya dakika 10, Mwacha alimtumia ujumbe mfupi wa maandishi (sms), Mkuu wa Polisi Kituo cha Mirerani, ASP Evarest Makala ambaye alifika na kuamuru uchaguzi huo usitishwe mara moja.

Kutokana na hali hiyo, Katibu wa CCM Wilaya ya Simanjiro, Ally Kidunda alisema uchaguzi huo utarudiwa baada ya kupata maelekezo kutoka ngazi ya mkoa.

Kidunda alisema kata za Mirerani na Endiamtu, ndizo zilizokuwa zimepangiwa kuanza uchaguzi huo na kufuatiwa na nyingine. Wilaya hiyo ina kata 18.

Bonyeza HAPA kudownload applicationi ya Bongojamii Blog kwenye simu yako ili kupata habari zetu Haraka

Featured Posts